Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Maida Hamad Abdallah

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ya kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kwa namna ya pekee, kwa vile nimesimama kwa mara ya kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia nimpongeze kwa hotuba anazoendelea kuzitoa tokea kuapishwa kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kwa namna ya pekee nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa hotuba yake ya juzi, Mei Mosi, kwa kuongeza umri wa wategemezi kutoka miaka 18 hadi miaka 21. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikiendelea, nataka nizungumzie kuhusu suala la upungufu wa askari. Moja kwa moja nataka nijielekeze katika Mkoa wetu wa Kaskazini Pemba. Tunafahamu kwamba askari wanafanya kazi kubwa sana na wanatusaidia kwa njia moja au nyingine katika kulinda raia na mali zao.

Mheshimiwa Spika, katika mkoa wetu, askari ni wachache na uchache huo umetokana na kwamba wengi wamestaafu, wengine wamepandishwa vyeo, wengine wamefariki na wengine wamepata uhamisho kutoka kituo kimoja kwenda kituo kingine, na hata nje ya Zanzibar.

Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu wa askari hawa, kutokana na umuhimu wa mahitaji tuliyonayo ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, ingawaje wengi wamechangia katika maeneo au kwa nchi nzima kwamba askari ni wachache, lakini kwasababu nimejielekeza Mkoa wa Kaskazini Pemba, niseme tu kwamba tunaomba tuongezewe askari katika maeneo yetu kwa sababu askari ni wachache.

Mheshimiwa Spika, suala la nyumba za watumishi; naipongeza sana Serikali kwa kuongeza bajeti ya kuendelea kujenga nyumba za watumishi. Ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba, yapo majengo ambayo Serikali kupitia Wizara hii imeendelea kujenga lakini bado askari wetu wana upungufu wa makazi; askari wetu wengi wanakaa uraiani. Niiombe sana Serikali kuongeza bajeti au kuweka uharaka katika kuendelea kujenga majengo haya ili askari wetu waendelee kuondokana na changamoto hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la OC; OC bado ni ndogo, lakini hata hiyo inayotengwa bado haiwafikii walengwa. Niiombe sana Serikali kwa vile kupitia Wizara ya Afya pamoja na Elimu, fedha zinaelekezwa moja kwa moja kwenye vituo, basi niiombe sana Serikali fedha hizi za OC ziende moja kwa moja kwenye vituo husika ili kuondosha changamoto kwa sababu madeni yamekuwa ni mengi.

Mheshimiwa Spika, wana madeni mengi ya mafuta, hawawezi kutekeleza majukumu yao kutokana na uchache wa mafuta, uchache wa vifaa. Kama OC itakwenda moja kwa moja na itakwenda kwa wakati, basi wataweza kulipia madeni yao kwa wakati, lakini pia wataweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kuhusiana na suala la fedha ambazo zilikuwa zinatengwa kwa ajili ya kuwahudumia askari hawa, zile shilingi laki tatu kwa miezi mitatu, na hii ni kutokana na uanzishwaji wa maduka ya duty free. Askari hawa walikuwa wanapatiwa huduma katika maduka haya kuweza kujikimu kimaisha.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi Serikali imesitisha lakini kutokana na hilo Serikali ikawa imetenga kila mwezi angalau askari hawa waweze kupewa laki moja kwa ajili ya kujihudumia kiuchumi. Pamoja na hilo, fedha hizi zikawa zinatengwa shilingi laki tatu kwa miezi mitatu, yaani ili kufidia kwamba hatuwezi kuwapelekea kila mwezi lakini tuwe tunawapelekea kwa miezi mitatu; hata hilo pia limekuwa na changamoto. Muda mrefu hawakuwa wakipokea fedha hizi, naomba sana Serikali askari hawa tunajua kazi wanazozifanya, hizi lakini tatu ziweze kuwafikia kwa haraka ili waweze kutekeleza majukumu yao.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah.

MHE. MAIDA HAMAD ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante, nashukuru.