Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nichukue fursa hii kuwapongeza akinamama wote waliokuwa wanaadhimisha siku yao jana na kipekee kabisa wanawake wa UKAWA kwa namna tulivyoshikamana dhidi ya dhuluma na dharau yoyote inayoweza kujitokeza kwa mwanamke. Pia, nitoe masikitiko kwa Naibu Spika ambaye ni mwanamke alionekana kindakindaki kutopenda kukemea kilichokuwa kinatokea na hata tulipoomba nafasi ya kuonesha hisia zetu, alionekana kuiminya, nitoe masikitiko sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, na-declare interest, mimi ni Mjumbe katika Kamati ya Viwanda na Biashara, kwa hiyo, nimeshiriki sana katika kipindi hiki cha Ubunge wangu katika Kamati husika. Nimeona kwa vitendo ni namna gani tunamaanisha tukisema tunataka kujenga uchumi wa viwanda na ni namna gani tunawahadaa Watanzania tukitaka kuwaeleza ukweli juu ya kuwa nchi ya uchumi wa kati ifikapo 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe masikitiko yangu kwa sababu watu wengi wamepongeza hotuba, ukiiangalia hotuba kwa maneno tu siyo mbaya, lakini ukienda kwenye money value ya kile wanachokisema kwamba wanaenda kukitekeleza, ni vitu viwili tofauti. Pia, kwenye Kamati nilimwambia Waziri nikasema ni bora tuseme ukweli kuliko kuwahadaa Watanzania kwamba tunaenda kwenye uchumi wa viwanda, ila tuseme siku moja tunaweza kwenda kwenye uchumi wa viwanda. Kwa bajeti ya mwaka huu ambayo ni shilingi bilioni 81 ukiisoma na uki-analyse kipengele kwa kipengele hatuwezi kwenda kwenye uchumi wa viwanda ila tunaweza kuanza kwenda kwenye uchumi wa viwanda pengine miaka 20 au 30 ijayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, je, tofauti yake na bajeti iliyopita ni ipi? Tofauti ya bajeti iliyopita ilikuwa ni shilingi bilioni 87. Kwa masikitiko kabisa bajeti ya maendeleo ilikuwa shilingi bilioni 35, lakini mpaka Machi ilikuwa imetoka shilingi bilioni moja tu ikienda kwenye viwanda. Hao hao ambao tukonao leo wanaosema kazi tu ndiyo walikuwa kwenye madaraka, je, nini kilitokea? Kama bajeti imepangwa kwa 100% ambayo ni shilingi bilioni 35 ya kuendesha viwanda, lakini inapatikana 5% tu ambayo ni shilingi bilioni moja ya kuendesha viwanda, je, tunaweza kwenda tunakotarajia kwenda?
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi nimesoma Dira na Dhima ya Wizara ya Viwanda, inaongea wazi kwamba inataka kutengeneza mazingira wezeshi ya ukuaji wa biashara. Ikaja kwenye Dhima inasema kutengeneza msingi shindani wa viwanda wenye kuwezesha biashara ulimwenguni na maeneo mengine. Unaona kwamba plainly Wizara imejikita katika kuandaa mazingira. Sasa kama tunaandaa mazingira, tunaandaa mazingira namna gani? Ni kwa kutengeneza sera ambazo ni rafiki kwa wawekezaji, ni kwa kutengeneza sera ambazo zitawezesha ushindani, ni kwa kutengeneza sera ambazo zitaweza kuwa-accommodate wawekezaji kuja kuwekeza katika nchi yetu. Kwa hiyo, sasa ambacho tungekuwanacho hapa ni kujadili sera ambazo zitasaidia kuleta viwanda. Hicho ndicho nilichokiona kwenye bajeti ya Viwanda na Biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama haitoshi sehemu kubwa ya ziara tuliyoifanya kilio kikubwa cha maeneo tuliyoenda ni maeneo ya uwekezaji hususan kupata maeneo ambayo tunaweza tukafanya uwekezaji kwa ajili ya maandalizi sasa ya viwanda. Tulienda EPZA wakatuambia kwamba katika bajeti ya mwaka jana walipaswa kulipa fidia ya shilingi bilioni 60 kwa ajili ya kupata maeneo ya uwekezaji lakini ni shilingi bilioni moja ilitoka na kwa inflation rate tunapaswa kulipa shilingi bilioni 190.9 almost shilingi bilioni 191. Ile iliyokuwa shilingi bilioni 60 mwaka jana inflation rate imeenda mpaka leo tunahitaji kulipa shilingi bilioni 191! Hiyo fidia tu inazidi bajeti ya Wizara ambayo ni shilingi bilioni 81! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunaweza kuwahadaa watu tunavyoweza, lakini uhalisia utabaki, tutarudi hapa mwaka kesho tutaanza kuogopa kuangaliana usoni kwa sababu hatuwaambii watu ukweli, ni usanii unaoendelea. Pesa iliyotengwa haiwezi kukidhi haja ya tunachotaka kufanya. Kwa hiyo, nasema ni bora tuseme uhalisia kwamba tuna plan, tunafikiria kutengeneza nchi ya viwanda, lakini bado hatujafika huko kwa sababu ya bajeti tuliyokuwanayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nimeangalia ile miradi ambayo itakuwa vichocheo ambapo moja kati ya miradi hiyo ni kilimo. Ukiangalia kilimo na bajeti ya kilimo husika huwezi kuona coloration between kuwa na viwanda na kuwa na bidhaa zitakazosaidia viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nilienda mbali zaidi kuangalia kweli nchi yetu iko serious inathamini kilimo? Nikaangalia ajira tu zilizoelekezwa katika sekta ya kilimo ilikuwa ni aibu kwa sababu Waziri, Mheshimiwa Angellah Kairuki alisema kwa mwaka jana kulikuwa na ajira takribani 3,000 ambapo kwenye kilimo ilikuwa ni robo ya ajira hizo 3,000 zilizokuwepo kwa mwaka jana. Kwa hiyo, unaweza ukaona ni kwa namna gani hatujajipanga wala kuwekeza kwenye kilimo ambapo tunataraji kilimo kiwe ni kichocheo kwenye viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kama hiyo haitoshi ukiangalia 80% ya wananchi wetu kwa maana ya Watanzania ni wakulima ambao wanaishi katika absolutely poverty, katika umaskini wa kiwango cha juu. Wakaenda mbali zaidi wanaonesha kwa miaka 15 iliyopita uchumi wa mkulima ambao ni 80% umaskini umepungua kwa 3.4% ambayo ni kidogo sana. Hawa wakulima maskini ndiyo tunawatarajia wawe catalyst katika kuendesha viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Kamati niliuliza, je, tumejiuliza ni kwa nini viwanda vili-fail? Ni kwa nini viwanda vilikufa? Takwimu ziko wazi! Viko viwanda 34 ambavyo vimekufa na vimegeuzwa kuwa maghala. Nilitaraji Waziri aje atuambie ni kwa nini vile vilikufa na tumeandaa mkakati gani kwa ajili ya kufufua tena hivyo viwanda? Mheshimiwa Waziri ameandika kwenye kitabu chake kwamba sababu kubwa ni kwamba watu walikopa pesa wakikopea hivyo viwanda na bahati mbaya vikageuzwa maghala lakini hiyo Serikali ya Hapa Kazi Tu ilikuwepo na hatujaona mkakati mahsusi wa kuzuia kurudi nyuma tulikotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nitaongelea kidogo hujuma za dhahiri tunazofanya au Serikali inazofanya dhidi ya hata vile viwanda vidogo ambavyo vinajitahidi kuchechemea. Kama Kamati tulitembelea kiwanda cha TANALEC, wale ni wazalishaji wakubwa wa transformer. Hiyo kampuni ya TANALEC Serikali ina hisa ya 30%. Cha kushangaza Serikali imewahi kutoa tenda ndogo sana ya kuzalisha transformer 3,000 ambayo wanadai kwamba ni 10% ya transformer zinazohitajika nchini na tenda zilizokuwa zinabaki wamepewa nchi za nje, India, China na wengine. Hivyo kile kiwanda wanalalamika kwamba kukosa tenda za Serikali wamelazimika kupunguza ajira. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wafanyakazi takribani 55 walilazimika kuacha kazi kwa sababu walishindwa kuwalipa kwa lengo la ku-stabilise, lakini kama haitoshi wameendelea kushindwa kujiendesha. Swali ni je, Serikali inajihujumu yenyewe? Kama sisi Serikali tuna hisa kwenye kiwanda kile kwa nini tunazidi kujihujumu? Moja kati ya hasara tunayopata tunashindwa kupata Pay As You Earn kwa sababu watu wametoka kazini. Tungewaajiri watu kwa sababu kile ni kiwanda chetu tungepata Pay As You Earn lakini pia tungeweza kusaidia familia mbalimbali za watu wale ambao wameajiriwa katika eneo hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kikubwa ambacho tulikiona ni mlundikano wa titiri za regulatory authorities. Ningependa Waziri atuambie nini tofauti ya TFDA na TBS? Wanafanya almost the same function! Kinachoonekana pale ni kuongeza mlolongo ili wale wafanyabiashara wakate tamaa. Nataka kujua pia tofauti ya OSHA na Fire! Kwa sababu OSHA wakifika kwenye kiwanda wanaangalia zile fire extinguisher, wale Fire wenyewe wakija wanaangalia fire extinguisher! Kwa hiyo, naishauri Serikali iangalie ni namna gani inaweza ikapunguza mlolongo wa zile regulatory authorities kwa lengo la kuongeza ufanisi kwa wafanyabiashara au wale wenye viwanda. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nimekiona ni changamoto, wale wafanyabiashara wanasema wanavyofika bandarini Serikali au mamlaka imekuwa ikipandisha bei kutegemea wao wanavyojisikia. Wanadhani kama mtu amechukua container la bidhaa fulani kutoka nchi jirani amekuja amepata punguzo kutokana na competition alivyoweza kupata, akifika bandarini wanamwambia kwa uzoefu wetu huwa inauzwa hivi. Kwa hiyo, imekuwa ni changamoto ya kuwapandishia bei wafanyabiashara kutegemeana na mahitaji ya yule anayefanya tathmini. Kama haitoshi vigezo haviko dhahiri ni kwa namna gani hiyo pesa imekuwa inaongezwa katika hizo bidhaa zao ambayo imeendelea kuwa changamoto.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.