Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Madini

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Nianze kuipongeza Wizara kwa bajeti yao nzuri, nampongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri na Watendaji wote katika Wizara hii kwa kufanya kazi nzuri ambayo imeleta mapinduzi makubwa kwenye Wizara hii ya Madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naipongeza Wizara kwa kusimamia vizuri suala la malipo ya mipasuko kwenye Jimbo langu la Geita. Tulikuwa na tatizo la mipasuko ambalo lilidumu kwa takribani miaka 20, lakini Mheshimiwa Waziri alikuja akaweka mguu chini na sasa GGM wamewalipa wale wananchi. Naomba kuwapongeza GGM na kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa maelekezo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nashukuru sana juhudi za Wizara. Pale Geita Mjini tumekamilisha refinery ya kisasa kabisa ambayo imejengwa na mwananchi Mtanzania na ninaamini kwamba Mheshimiwa Waziri atakuja na mpango mzuri ili kuhakikisha kwamba ile refinery yao ya Serikali isije ikawa inachukua mzigo wote Geita na kuupeleka kule, kwa sababu tunataka kuona ile refinery inaendelea kufanya kazi Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kilichosababisha mafanikio makubwa kwenye Wizara ya Madini ni baada ya Wizara hii kukaa na wadau na kuondoa utitiri wa kodi na kufanya watu kuwa walipa kodi wa hiari. Jambo hili limetufundisha kwamba kumbe siyo lazima kutumia nguvu nyingi, sheria nyingi, tozo nyingi ili tuweze kukusanya kodi. Sasa ni kwa mtazamo huo huo naiomba sana Serikali kuangalia maeneo yote ambayo wananchi wanalalamikia kuhusu tozo na kodi nyingi kuziondoa ili kufanya mazingira ya kufanya biashara kuwa mepesi Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema hapa wakati wanachangia kwenye Mpango kwamba shida kubwa tuliyonayo sasa kwenye wachimbaji wadogo wadogo ni investment vis-a-vis production inayofanyika kwenye madini, kwamba uwekezaji ambao wachimbaji wadogo wanaweka ni mkubwa sana kuliko faida ambayo wanaipata. Watu wengi wanaweza kuona mauzo yameongozeka, lakini katika wachimbaji wadogo 100 wanaoweka pesa zao, ni wachimbaji watano au 10 ndiyo wanaoweza kurudisha gharama, the rest wote wanakula hasara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini? Kwa sababu wanachimba kwa kubahatisha, wanachimba kwa kupiga ramli, wanachimba kwa kufuata mkumbo. Jambo hili limezungumzwa vizuri na Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tuwape uwezesho GST wawe na league za kutosha. Hizi league nne ambazo wanazo, Tanzania ina madini kila mkoa na kila wilaya. Wawe na league za kutosha, tuajiri manpower za kutosha tuache kupeleka watu kwenda kupiga ramli na ndiyo maana msishangae kuona kwamba katika maeneo mengi ya machimbo ya madini Waganga wa Kienyeji wana soko sana kwa sababu wanapiga ramli sana na hii ni hatari sana katika nchi ambayo imepiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Geita pale mitaa yangu na Vijiji vya Magema, Nyamalembo, Katumaini, Mizingamo na Katoma imekuwa kwenye mgogoro mkubwa na mgodi wa GGM kwa takribani miaka 20. Eneo la GGM ni Square kilometer 192, eneo wanalochimba ni kama asilimia 10 ya eneo hilo. Eneo hili la vijiji hivi limewekewa ulinzi sasa wa Polisi. Wananchi wakienda shambani wanakutana na Polisi, wakienda kukata kuni wanakutana na Polisi, akichimba choo, anakutana na Polisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sidhani kama Mheshimiwa Waziri, kule kwao Bulangwa wananchi wakiwa wanakutana na Polisi kila siku wanaweza kuishi kwa raha. Lile eneo wananchi wanasubiri fidia. Eneo lile ni kilometa zaidi ya 15 kutoka kwenye pit ya mgodi. Kama eneo lile ni potential kwa mgodi hakuna sababu ya kulundika Polisi pale kulinda raia wanaoenda kulima na kukata kuni, wawalipe wale wananchi waondoke pale. Hakuna sababu ya watu kuishi kwa tension wakiamka asubuhi kwa tension kwa sababu tu lile eneo lipo ndani ya leseni. Leseni ya mgodi ni kubwa lakini hawaja tayari kulitumia eneo lile. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, wananchi hawa wanaendelea kuishi kama vile ni wakimbizi wapo kwenye nchi ya vita. Hatuhitaji sisi kuja kuona Polisi wanajaa kwenye mitaa yetu, waje wakamate kama kuna wahalifu, hatuvamii eneo linalochimbwa, hatuna shida na kule na tunaunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme ukweli, kama kuna mtu anafaidika na uwepo wa wachimbaji wakubwa ni Geita. Nasi tunataka waendelee kuwepo, tunawaunga mkono, tunawaomba wananchi waache kuvamia maeneo yao, lakini kwenye makazi yao ambayo hawajalipwa fidia. Mheshimiwa Waziri tunaomba sana wananchi wapewe uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, Mheshimiwa Musukuma amezungumza hapa kuhusu CSR. Nilizungumza wakati nachangia Mpango kwamba tulitunga sheria nzuri sana, tukasema kwenye eneo la Service Levy 0.3 percent inalipwa Halmashauri. Haijulikani kwenye CSR ni percent ngapi? Shida kubwa nyingine tuliyonayo ni kwamba pesa hizi za CSR, sheria imebaki kimya kwenye manunuzi na kwenye matumizi. Sawa zinabaki kule GGM, tunashirikiana na Local Council, lakini matokeo yake zimekosa usimamizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale kwangu supervision peke yake nilikuwa nacheki, imegharimu zaidi ya shilingi milioni 250 ambazo zinalipwa kwa viongozi wanaokuja kuangalia kazi zilizofanywa na CSR. Sasa Mheshimiwa hii ni pesa ambayo inakuwa declared kwenye kodi, kwa sababu anapotoa hii pesa mwisho wa siku anasema kwenye kodi nimepeleka hizi pesa kwa wananchi. Huyu Mtumishi wa Umma anaenda kulipwa supervision shilingi milioni 250 akiwa ndani ya eneo lake? Anatumiaje zile pesa namna hiyo. Naomba hii sheria iwekwe vizuri, hizi pesa zibaki kwa wenye mgodi, lakini matumizi yake yafuate sheria za matumizi ya pesa za Umma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, amesema hapa Mheshimiwa Iddi, nilisema wakati ule Local Content wamekudanganya kwamba wamefuata sheria. Pale logistic wanazotoa, ni kazi ndogo ndogo, lakini sheria inasema zile bidhaa ambazo hazipatikani Tanzania, waingize ubia na Watanzania, lakini halifanyiki hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa tunapigwa pesa kwa sababu kupitia Local Content kuna transfer pricing. Kama hakuna Local Content, akija mtu anayeuza kutoka nje, kinachofanyika ni kufanya gharama ya manunuzi kuwa makubwa na matokeo yake pesa hizi zinarudi kule kule zilikotoka. (Makofi)

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Nusrat Hanje.

T A A R I F A

MHE. NUSRAT S. HANJE: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba ni kweli tuna tatizo kubwa sana la uelewa kuhusu Local Content kwa sababu hatuna sheria inayoitwa Sheria ya Local Content ambayo ita-define ni vitu gani na vitu gani sisi kama nchi tunavi-regard kama local content? Ndiyo maana kuna mwingiliano wa kila namna mtu anavyo-define. Kwa hiyo, nimpe taarifa hiyo, lakini pia tunahitaji kama inawezekana kupata sheria maalum kwa ajili ya local content. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Constantine John Kanyasu, malizia mchango wako.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, nimtaarifu tu Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria ipo na imeeleza vizuri sana na sheria ile shida yake kubwa ni kwamba hakuna compliance kwa wale wanaolengwa na sheria yenyewe, lakini sheria yenyewe ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jimbo langu lina wachimbaji wengi. Wafanyakazi wengi wa mgodi ni wa muda (contractual). Tulitunga sheria hapa tukasema kwamba mafao ya maeneo haya yanarudi kwenye mfumo ambao tulisema akishafutwa kazi anaanza kulipwa asilimia
80 sijui ya mshahara, lakini sehemu hii kubwa naiomba Serikali, wananchi wangu bado wanalilia sana Fao la Kujitoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kampuni nyingi zinafanya kazi kwa miaka miwili zinafunga na zikishafunga, wananchi hawa wanapoteza kazi kwa miaka mitatu mpaka minne. Hii fedha ilikuwa inawasaidia kwenda kuanzisha biashara na wengine walikuwa wanaweza kusomesha watoto wao. Sasa hivi muda wa kufuatilia mafao haya ni mrefu sana na kwa kweli wanakula hasara kubwa. Nilikuwa naomba sana maeneo haya yaangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)