Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Hamad Hassan Chande

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kojani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi hii ya kutoa mawili, matatu kwa zile hoja ambazo zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Pia niwashukuru sana wale wote waliochangia katika mada hizi mbili, suala la Muungano na Mazingira kwenye Ofisi yetu. Nawashukuru sana kwa michango yenu mizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa muda siyo rafiki, naomba kwa ruhusa yako niende tu moja kwa moja kwa baadhi ya hoja ambazo zimetolewa na Wabunge, hasa kuhusu Muungano.

Mheshimiwa Spika, hoja ya kwanza ambayo imetolewa na Mheshimiwa Khadija Hassan Aboud; Muungano umetimiza miaka 57. Pongezi zimepokelewa. Aidha, Serikali ya SMZ na Serikali ya SMT zinaendelea na jitihada za kutatua changamoto kumi za Muungano zilizobakia ambazo 15 tayari zimeshapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Spika, hoja yake ya pili ni ushauri; ametoa ushauri kuhusu kuimarisha na kudumisha Muungano. Ushauri umepokelewa. Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Hassan Mwinyi, zimeweka masuala hayo ya Muungano kwa nia moja vipaumbele vyake hivyo ni Serikali zote mbili kushirikiana katika kuzipatia ufumbuzi hizi kumi zilizobakia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja ambayo ameitoa Mheshimiwa Bakar Hamad Bakar kwamba kuenzi Muungano ni pamoja na kuwezesha viongozi wa Muungano huu, mfano Dkt. Omar Ali Juma; maoni yamepokelewa. Aidha, Serikali italifanyia kazi suala hili.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo ameitoa Mheshimiwa Kassim Hassan Haji ni kuhusu Muungano wa Taasisi zetu za Zanzibar na zile za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama vile TBS na ZBS kule Zanzibar. Suala hili ushauri huu tumeuchukua kwa mikono miwili na hatua zimeanza huko nyuma kwasababu mwenyewe nilikuwepo ZBS, tumeshakaa vikao tofauti, mbalimbali kujadili suala hili hapa. Kwa hiyo, ushauri umechukuliwa na tutaufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ipo hoja ya Mheshimiwa Mwanakhamis Kassim Said ambaye hoja yake alikuwa anatoa pongezi, pongezi hizo zimechukuliwa na zimezingatiwa na tutazifanyia kazi kwa kadri inavyowezekana.

Hoja nyingine ya Mheshimiwa Mwanakhamis, haikuwa zaidi nayo ni pongezi tu kwa Jamhuri ya Muungano na kudumisha Muungano wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Asia Abdukarimu Halamga, Mbunge Viti Maalum, pongezi zimepokelewa na tutazifanyia kazi. Suala linaloshughulikiwa na kamati ya pamoja ya SMZ na ya SMT zinashughulikiwa masuala ya muungano baada ya kukamilika Serikali itatoa taarifa kuhusu jambo hilo.

Mheshimiwa Spika, ipo hoja ya Mheshimiwa Omar Ali Omar Hafidh, yeye amesema tu Elimu ya Juu, sana sana alizungumzia suala la mitaala kwamba hakuna mlingano mzuri kati ya mtaaala unaotumika Zanzibar na ambao unatumika Tanzania Bara. Suala hili tumelichukua na tutalifanyia kazi, tutafuatilia kwa kadri inavyowezekana ili tuweze kulinganisha mitaala yetu hiyo, ili kusudi tija na mafanikio ya wanafunzi wetu yawe yanalingana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya summary hiyo ambayo imetolewa na Waheshimiwa Wabunge katika Bunge lako hili Tukufu naomba tu niseme zipo changamoto kumi na tano ambazo zimeshapatiwa ufumbuzi na zimebakia changamoto kumi nazo kwa hakika karibuni kadri vikao vitakavyokaliwa na Serikali ufumbuzi wake utapatikana moja baada ya nyingine.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze mambo mawili kuhusu muungano. Katika kipindi ambacho muungano unahitajiwa ama unahitajika zaidi Tanzania ni kipindi hiki. Hii ni kwasababu wapo maadui wengi wenye macho mabaya na makali wanaoutazama vibaya Muungano wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa hiyo, kipindi ambacho kinahitajika ni hiki, kwasababu hata wahenga wanasema Umoja ni Nguvu na Utengano ni Dhaifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na siku zote mbwa mwitu hula nyama ya kondoo aliyejitenga. Lakini jambo la pili, tuachane na wale watu ambao wana mawazo mgando ama fikra mgando kuhusu suala la muungano. Kwani hata ingekuwa ile tarehe 26 Aprili,1964 wangeulizwa kuhusu Muungano basi wangejibu hayo hayo kwamba kwao Muungano usingefaa.

Mheshimiwa Spika, naomba niombe kwa Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa jumla, mambo mawili tu; jambo la kwanza, kwa kuwa wapo watu wenye ujauzito wa mawazo kuhusu Muungano naomba tuwe madaktari wazuri sana wakuwafanyia tiba, upasuaji, taratibu kabisa ili wajifungue salama, wawe wanajua nini dhana ya muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili, ambalo naomba ni wale watu wenye degree zao, maarifa yao makubwa ambayo maarifa hayo tunatarajia yabakie ndani ya ubongo wao lakini kwa bahati mbaya maarifa hayo wanayahamisha na kuyapeleka kwenye matumbo yao. Ili kusudi kubomoa mwelekeo wa Jamhuri ya Muungano. Naomba watu hawa tuwaelimishe na naamini wataelimika inshallah.

Mheshimiwa Spika, baada ya hayo naomba nitoe shukrani kubwa kwa familia yangu, ambayo tulikesha pamoja katika kuandaa haya. Lakini pili nitoe shukrani kubwa sana kwa wapiga kura wangu wa Jimbo la Kojani kwa kuniwezesha kufika hapa leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)