Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia mchana huu. Nafikiri kwansababu nilikaa Zanzibar ndiyo maana nimefuatia kuchangia baada ya watu wa Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu kwamba hali ya mazingira katika nchi yetu imeendelea kuharibika sana. Takwimu za dunia zinaonyesha kwamba joto katika miji mikubwa limeendelea kuongezeka sana. Tanzania kwa sababu bado tuna misitu mingi hatujaona yale matatizo makubwa. Nilikuwa na mambo mengi ya kuzungumza lakini kwa sababu ya muda nijielekeze tu moja kwa moja katika ushauri.

Mheshimiwa Spika, ushauri ambao nataka kutoa katika eneo hili la kutunza mazingira, kwanza elimu ya kutunza mazingira kwa Watanzania naomba itolewe kwa wingi sana kwa sababu hali inazidi kuwa mbaya. Sehemu nyingi ambazo zimeanza kuwa kame ni kwa sababu mazingira yameharibiwa mno ndiyo maana unakuta kwamba mimomonyoko inakuwa mikubwa, maji yameacha mkondo yameenda kwa wananchi. Nashauri elimu itolewe kwa wingi kwa sababu sioni kama Serikali inatilia mkazo sana eneo hili.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa kuna hii kawaida kwamba Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya wanafanya zoezi la kupanda miti kama 100 au 500 halafu vyombo vya habari vingi vinatangaza lakini hatutaki popularity ya aina hiyo. Namshauri Waziri wa Mazingira kwamba katika KPA (Keep Performance Areas) kwa hawa Wakuu wa Mikoa wape malengo ya kupanda miti kila mwaka na wapimwe kwa namna hiyo. Tunaona pale Tabora Mkuu wa Mkoa aliyekuwepo Bwana Mwanri ameubadilisha sana kwa sababu ali-focus sana katika kupanda miti. Kwa hiyo, kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya iwe ni KPA yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo nataka kushauri katika kutunza mazingira tuongeze matumizi ya gesi lakini kama tutaweza tutoe ruzuku kwa vijijini. Kule vijijini tutoe ruzuku kidogo kwa sababu uwezo wa hawa watu wa vijijini kununua gesi ni kazi kubwa. Nashauri tufikirie kwa baadaye siyo sasa ili tutunze mazingira yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kumekuwa na ongezeko la kujenga kwenye miinuko katika miji, kwa mfano Iringa pale kuna miinuko lakini hata Morogoro pale Milima ya Uluguru unakuta watu wanajenga na Serikali ipo! Kwa nini Serikali isipige marufuku kwa sababu mazingira yanaendelea kuharibika na watu wanaangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia katika kutunza mazingira mashamba yaliyoko vijijini, kwa mfano kuna shamba pale Uyole wakati niko pale Mbeya nilisikia watu wanasema hili shamba tunataka tuishauri Serikali ibadilishe kuwa viwanja, hapana! Siyo lazima tufanye hivyo. Unajua maeneo makubwa kama yale ni ya makimbilio, inaweza ikatokea vurugu huko mjini eneo kama lile linakuwa ni eneo la makimbilio. Kwa hiyo, wazo la kusema kwamba ufute shamba lililopo mjini siyo sawa. Kwani nani alisema mijini hatuwezi kuwa na mashamba, ni eneo zuri sana la makimbilio lakini ni source kubwa ya oxygen. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo naliona sasa kumekuwa na ukataji mkubwa wa miti kiholela, watu wanachoma misitu lakini watu wanakata miti kiholela. Hawa Maafisa Misitu tumewaweka huko hawasimamii suala hili. Kwa hiyo, ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba Maafisa hawa wanasimamia maana vinginevyo haya maeneo yatakwisha. Kwa mfano, mimi nina Kata za Kihanga na Wasa, miti kule imekuwa ikikatwa hovyo hovyo, Mkuu wa Wilaya na Afisa Misitu yupo na usiku wanasafirisha. Sasa mimi kama Mbunge siko tayari kuona misitu yangu inaharibika niondoke niache wananchi wakiwa katika hali ya ukame. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine Serikali iongeze maeneo ya uhifadhi. Tukifanya hivyo kwa kweli tutaweza kutunza mazingira na uharibifu wa mazingira tutaweza kuudhibiti. Kumekuwa na ukuaji wa miji, vijiji vinageuka kuwa miji na shughuli za kiuchumi zinaongezeka, kilimo cha kisasa kinaongezeka; hivi vitu vyote vinaharibu mazingira.

Mheshimiwa Spika, naomba Serikali iyazingatie haya niliyoshauri, nafikiri tukienda hivi tutakwenda vizuri. Ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)