Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Abdullah Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mahonda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. ABDULLAH ALI MWINYI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kuanza mchango wangu kwa kutoa shukrani na kwa kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi nzuri na kwa uwasilishaji mzuri wa report hii ndani ya Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, pili, ningependa vilevile kumpongeza Mheshimiwa Mhagama kwa uwasilishaji wake wa Report ya Kamati. Ameweka mambo vizuri kabisa, sina shaka yoyote kwamba, kuna mambo mengine makubwa zaidi yanakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Soud amenifilisi kidogo katika mchango wake sasa mimi nitajikita katika jambo moja, moja ameshalizungumza kwa kina na nisingependa kulirudia na yeye amekuwa mahiri zaidi katika sekta yake hiyo ya masuala ya mazingira.

Mheshimiwa Spika, ningependa kujikita katika masuala ya yale mambo ambayo tunaita kero za muungano. Kero za Muungano imekuwa jambo la msingi kabisa ambalo hata Mheshimiwa Rais amelizungumzia mara mbili, tatu na kukabidhi kwa Mheshimiwa Makamu wa Rais, masuala ambayo bado hayajafanyiwa kazi yafanyiwe kazi kwa kipaumbele. Hata hivyo, ningependa kuzungumzia jambo moja ambalo lilishatafutiwa ufumbuzi, suala la mafuta na gesi, extractive industry.

Mheshimiwa Spika, mnapo mwaka 2014 mpaka 2015 suala hili lilikuwa moto sana na tukatolea maamuzi kwamba, suala la mafuta na gesi lisiwe suala la Muungano, kila upande ujitegemee. Jambo hili ni jema katika uendelezaji wa tasnia hii na hivi karibuni kwa bahati mbaya Ndugu zetu wa Msumbiji Total imejitoa, imetangaza juzi wamejitoa kuwekeza Msumbiji kwenye project ya LNG. Bahati mbaya kwa Ndugu zetu kwa sababu ule mradi ulikuwa mkubwa ndio unasemekana ndio ulikuwa mradi mkubwa kabisa ambao ungeweza kutokea katika Sub Saharan Africa katika miaka yote iliyopita, lakini kwa sababu ya matatizo ya machafuko na ugaidi wameamua kujitoa na investment hiyo haitaendelea.

Mheshimiwa Spika, sasa msiba wa wenzetu ni faraja kwetu, lakini kuna changamoto moja ambayo lazima tuitazame. Ukiangalia yale makubaliano yetu ya ndani tuliyokubaliana kwamba, tasnia hii sio sekta ya Muungano na taasisi na sheria na asasi zikaundwa, huku upande wa bara zipo TPDC, PURA na mengineyo na Zanzibar zikafanywa hivyohivyo na sheria ikaundwa na kuna watu ambao tayari wameshaingia katika kufanya utafiti, lakini kuna changamoto moja.

Mheshimiwa Spika, ukiangalia Katiba yetu ukurasa wa 128 inazungumza, Mambo ya Muungano, jambo la 15. Naomba ninukuu kwa ruhusa yako, inasema ifuatavyo; “15. Maliasili ya mafuta pamoja na mafuta yasiyochujwa na ya motokaa na mafuta ya aina ya petroli na aina nyinginezo za mafuta au bidhaa na gesi asilia.”

Mheshimiwa Spika, hiyo ni mojawapo ya vitu ambavyo vipo katika orodha ya muungano, Kikatiba, japokuwa sisi wenyewe tumekubaliana kwamba kila upande unajitegemea. Sasa suala la mafuta na gesi ni suala linalohusisha fedha nyingi sana, Mabilioni ya dola yanawekwa pale ili kuyatoa hayo mafuta na gesi.

Mheshimiwa Spika, japo kuwa sisi wenyewe tumekubaliana kwamba kila upande unajitegemea, sasa suala la mafuta ya gesi ni suala linalohusisha fedha nyingi sana, Mabilioni ya dola yanawekwa pale ili kuyatoa hayo mafuta na gesi.

Mheshmiwa Spika, jambo la kwanza mwekezaji yeyote atakayefanya kama ataweka mabilioni yake anafanya legislative review anatazama Sheria, Katiba na Mikataba yote kuangalia anawezaje kufanya hivyo. Na mtu mwekezaji wa Kimataifa ambaye anataka kuweka mabilioni hata fanya hivyo kama kuna kuwa kuna tatizo kama hili. Kwasababu ukiangalia kikatiba suala hili bado ni la Muungano. Sheria zipo zinazosema kwamba inaruhusu upande wa pili na makubaliano ya Kiserikali mambo ya pili yaendelee.

Mheshimiwa Spika, sasa kuna mgongano hapo bila huu mgongano kuurejebisha hakuna mwekezaji wa fedha nyingi atakayeweza kuweka fedha upande wa pili wa Muungano wa Zanzibar. Huku ipo bayana upande wa pili itashindikana, ningependa tu kumuomba Mheshimiwa Waziri alitazame hili hasa katika kipindi hiki ambacho fursa hii itakuwa moto, alitazame ajue jinsi gani tutalifanyia ufumbuzi suala hili kwa haraka iwezekanavyo ili uwekezaji mkubwa ule ambao tunautaka uweze kufanyika upande wa pili wa Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache ningependa tu kumshukuru tena Mheshimiwa Waziri kwa uwasilishaji mzuri na ningependa atoe maelezo katika hili ambalo nimeliweka hapa hadharani, ahsante sana. (Makofi)