Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Ummy Ally Mwalimu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

WAZIRI NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nianze Mwenyezi Mungu kwa kunipa kipali cha kusimama tena mbele ya Bunge lako Tukufu, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuhitimisha hoja yangu kuhusu makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu pamoja na Taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2021/2022. Kwa kutoa ufafanuzi kuhusu michango ya Waheshimiwa Wabunge ambao wametoa katika mjadala wetu wa siku tatu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Waheshimiwa Wabunge ambao wameweza kupata fursa ya kuchangia hoja yangu, hoja yangu imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 103 ambapo Wabunge 89 wamechangia kwa kuongea na Wabunge 14 wamechangia kwa maandishi, lakini pia Wabunge 46 wamechangia kupitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee ninawashukuru sana, Waheshimiwa Wabunge kwa maoni na ushauri wenu na katika hatua hii, niseme kwamba tumepokea maoni na ushauri wenu na tutaufanyia kazi. Kipekee nitambue mchango mkubwa wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambao uliwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati Mheshimiwa Humphrey Polepole. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kweli tumepitia mchango wa Kamati umesheheni madini, mazito ya kwenda kuimarisha utendaji kazi wa Mikoa na Tawala za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, tunajibu tu kwa kifupi, lakini naomba niwahakikishie Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Pamoja na wajumbe wa Kamati yetu yote ambayo mmetushauri tutayafanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapokea pia pongezi ambazo mmetupatia mimi pamoja na Manaibu Mawaziri, tunawashukuru sana na niseme pongezi hizi hazitatufanya tukapandisha mabega juu, bali litakua ni deni kwetu la kuhakikisha changamoto zilizopo katika mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa, tunakwenda kuzitatua. Tunaweza tusizimalize zote, lakini nataka kuwadhibitishia Waheshimiwa Wabunge, pia kuilinda imani kubwa na heshima kubwa ambayo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amenipa pamoja na Manaibu Mawaziri tutakwenda kufanya kazi na Waheshimiwa Wabunge mtaona matokeo ya kazi zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunafahamu kwamba wizara hii ikifanya vizuri basi tutakua tumeboresha maisha ya watanzania kwa sababu tunagusa maisha ya Watanzania katika ngazi zote, kwenye vitongoji takribani 64,384, vijiji 1,2319, mitaa 4,263, kata 3,956, tarafa 570, halmashauri 184, wilaya 139, pamoja na mikao 26. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Waheshimiwa Wabunge tunatambua jukumu ambalo tunalo la kuhakikisha kwamba tunaenda kuboresha shughuli za utawala na maendeleo katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hususani katika masuala ya elimu, Afya ya msingi, barabara, pamoja na Utawala Bora ikiwemo usimamizi wa rasilimali fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge zilihusu mambo mengi, lakini makubwa ambayo tumeyabaini ni matano, la kwanza ni miundombinu ya barabara chini ya wakala wa barabara vijijini na mijini TARURA; la pili ni masuala ya afya katika upande wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika zahanati, vituo vya afya, na hospitali zetu, za halmashauri kuna masuala ya watumishi upatikanaji wa dawa vifaa, na vifaa tiba, bima ya afya ya jamii iliyoboreshwa, pamoja na matumizi ya force account katika ujenzi wa miundombinu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hoja ya tatu ni elimu ikiwemo pia miundombinu, mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia ikiwemo uhaba wa watumishi; eneo la nne ni Utawala Bora na Ukusanyaki na usimamizi wa mapato kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa, lakini kubwa ambalo limejitokeza pia ni posho za Waheshimiwa Madiwani, madeni ya Madiwani kutokana na dhamana na mifumo ya ukusanyaji mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la tano ni masuala ya kuwawezesha wananchi kiuchumi hususani wanawake, vijana na watu wenyeulemavu. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge zile hoja binafsi tutazijibu kwa maandishi kuhusu majimbo yenu moja moja. Lakini hapa nitatoa ufafanuzi wa jumla katika masuala haya makubwa matano na nimshukuru sana Waheshimiwa Manaibu Mawaziri kwa kujibu baadhi ya hoja za waheshimiwa Wabunge na Waziri wa Afya kwa kujibu baadhi ya hoja. Kwa hiyo, nitajikita kwenye mambo makubwa mawili Utawala Bora na Usimamizi wa Rasilimali za Umma na pili ni suala la kuwawezesha wananchi kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, labda tu kwa ufupi nitowe msisitizo kuhusu miundombinu ya barabara kama alivyosema Naibu Waziri Dkt. Festo Dugange karibu asilimia 90 ya michango imegusa TARURA. Waheshimiwa Wabunge tumelipokea ili na kama alivyosema Naibu Waziri kwenye hotuba yangu tulisema mtandao wa barabara ambao umepitishwa ni kilometa laki moja na nane, habari njema tunamshukuru Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi wiki hii wameongeza mtandao wa barabara ambao utasimamiwa na TARURA kufikia kilometa 144,427, maana yake dada yangu Anne Kilango Malecela hata lile suala la vigezo vya kugawa, fedha za TARURA linaenda pia kupatiwa ufumbuzi kupitia suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatutaangalia tu ukubwa wa barabara, tutaangalia na masuala ya geografia ya eneo husika, kwasababu tukisema Tanga unipe kwa sababu ninakilometa labda 30 na mama Kilango ana kilometa 10 utupe fedha sawa siyo sahihi kwasababu yeye anamilima na mabonde na kuna mambo mengi ambayo tutazingatia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge naomba niwaahidi tutatenda haki kwa kila jimbo, tutatenda haki kwa kila halmashauri. Lakini jambo la pili ambalo mmeliongea ni kuhusu kuongeza fedha kwa ajili ya TARURA, Serikali imelipokea, Mheshimiwa Waziri Mkuu yuko hapa amewasikia, Waziri wa Fedha amewasikia tutaendelea kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la tatu kuhusu TARURA, Waheshimiwa Wabunge tumesikia maoni na ushauri wenu kwamba hakuna ushiriki mzuri wa Waheshimiwa Madiwani katika kupanga vipaumbele vya Ujenzi, matengenezo pamoja na maboresho ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumelitafakari ili na tumeamua kuanzia mwaka huu wa fedha vipaumbele vyote vya ujenzi, kuboresha na matengenezo ya barabara vitapitishwa na baraza la Madiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika zile siku tatu za Madiwani kukutana kwa ajili ya kujadili bajeti tunaongeza siku moja kabla itakuwa ni madiwani kujadili vipaumbele vya matengenezo, maboresho, pamoja na ujenzi wa barabara. Kwa hiyo, badala ya kikao cha siku tatu kitakuwa ni kikao cha siku nne na ikiwezekana waende site wakaone hizo barabara ambazo zinapendekezwa kujengwa na kufanyiwa maboresho. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwasababu na sisi tunakaa katika Mabaraza ya madiwani, tuzingatie pia ushauri wa wawataalamu wetu tusije tukarudi nyuma kila diwani anataka apewe mita 200 au 300 za barabara. Kwa hiyo, pale ambapo labda tutashindwa kupata consensus, barabara ipi, kwa hiyo, tutaomba baraza la madiwani watuandikie wizara alafu tutafanya maamuzi, lakini tumewasikia, kwakweli ni haki yao madiwani zile ni barabara zao ziko katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwasababu ya muda mradi wa TAKTIK na tumewasikia Wabunge kutoka Manispaa, Majiji na Miji upo kwenye maandalizi na tunaamini kwamba tutaukamilisha kwa wakati. Kwa hiyo, niwatowe hofu Wabunge hususani kutoka majiji, Mheshimiwa Naibu Spika ulisema, Mheshimiwa Mabula Mwanza, lakini na mimi pia Tanga ni mnufaika kwa hiyo kupata kwa Mbeya kutakua kupata kwa Tanga. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, siyo tu majiji sita ni majiji, manispaa na miji 45 tumeona manufaa ya mradi huu. Kuhusu DMDP II, watu wa Dar es Salaam tumewasikia na pia tuko katika maandalizi ya mwisho. Kwa hiyo, tunaamini pia kwamba mradi huu tutaukamilisha kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa nijikite katika hoja nyingine mbili; ya kwanza ni suala la utawala na usimamizi wa rasilimali fedha za umma. Tumepokea ushauri wa kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba tuzisimamie kikamilifu halmashauri nchini ili kuhakikisha kuongeza makusanyo kwa kuweka malengo halisia. Hili tumelipokea na nikweli halmashauri nyingi zina under bajet hazipangi malengo mahususi ya makusanyo, lakini hata yale makusanyo katika taarifa yangu nimeonyesha hadi mwezi wa pili mwishoni makusanyo ni asilima 58 tu.

Mheshimiwa Spika, na makusanyo hayo kadri tutakavyoyapata ndipo tunaenda kuboresha huduma za jamii katika halmashauri zetu. Kwa hiyo, tumeandaa mwongozo wa usimamizi wa mapato ya ndani revenue administration manual ambayo umeainisha namna bora ya kuandaa mipango na bajeti ukusanyaji na usimamizi wa mapato haya.

Mheshimiwa Spika, pia Ofisi ya TAMISEMI tutaendelea kuwajengea uwezo wataalam wa ngazi za mikoa na halmashauri jinsi ya kuandaa mipango na kufanya makisio ya mapato ya ndani yenye kuakisi uhalisia. Pia sasa hivi ndani ya Wizara tunakamilisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (Five Years Revenue Enhancement Strategic) ambapo lengo pia ni kufanya maoteo ya makusanyo kwa kila halmashauri kwa miaka mitano. Kwa hiyo, suala hili tumelipokea na tutaenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, suala la pili, Serikali itizame mwenendo wa ukusanyaji na udhibiti wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa kutumia machine za kielektroniki (POS). Hili pia tumelipokea na sasa hivi tumeongeza matumizi ya machine za kielektroniki kwa ajili ya kukusanya mapato, tuna takribani machine za POS 26,873. Ndani ya kipindi kifupi tutaongeza machine 2,129 ambazo tutazisambaza katika halmashauri 49.

Mheshimiwa Spika, naomba nikiri tunalo pia tatizo la uadilifu wa baadhi ya watendaji wetu hususani wanaohusika na ukusanyaji wa mapato. Kwa hiyo, hatutasita kuchukua hatua za nidhamu pamoja na kuboresha sheria ndogondogo za halmashauri katika kuhakikisha kwamba mapato yanakusanywa na yanaenda katika njia sahihi na iliyokusudiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha tunaboresha mfumo wa makusanyo unaotumika sasa hivi ili kuondoa kabisa mapokezi ya pesa taslimu kama Waheshimiwa Wabunge mlivyotushauri hapa lakini pia kutowasilishwa benki fedha zinazokusanywa na matumizi ya fedha mbichi kabla ya kuwasilishwa benki. Tunaamini kwamba mfumo huu utawawezesha pia walipa tozo, ushuru na kodi kujua wanachodaiwa, kupata control number na kufanya malipo kwa mtandao kwa wakati na tunategemea utaanza tarehe 01 Julai 2021.

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ni kuhusu kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuziwezesha halmashauri kutoa huduma bora. Nalo hili tumelipokea na ndiyo maana pia katika bajeti yetu moja ya kipaumbele tumeeleza pia tunaenda kuongeza nguvu ya kuhakikisha kwamba tunawekeza au tunaziwezesha halmashauri katika kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara pamoja na uwekezaji. Lengo letu ni kuhakikisha tozo, kero kwa wananchi zinaondoka, tujike kwenye vile vyanzo ambavyo tunajua kwa hakika kwamba vitaweza kutuletea mapato.

Mheshimiwa Spika, taarifa ya CAG imeonyesha kwamba halmashauri zimeshindwa kukusanya takribani shilingi bilioni 31 katika mwaka wa fedha 2020/2021 wakati wenyewe wamesema hiki ni chanzo lakini wameshindwa kukusanya. Kwa hiyo, tumelipokea na hili tutalifanyia kazi ikiwemo pia kuweka miradi ya kimkakati katika halmashauri nyingi kwa sababu pia tumeona ni vyanzo vya mapato.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni katika utawala bora, Kamati na Waheshimiwa Wabunge wameshauri Ofisi ya Rais-TAMISEMI isimamie Sekretarieti za Mikoa kuandaa taarifa za mipago na bajeti za mafungu. Tunakubaliana na ushauri na mimi mwenyewe nataka nikiri nimeona tunalo tatizo. Juzi nilienda kwenye Sekretarieti ya Dodoma, kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa imeanzishwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa. Huyu Katibu Tawala wa Mkoa ana wataalam wote wa fedha, wahasibu, miundombinu including wahandisi, wanasheria, madaktari na watu wa elimu lakini nikawauliza katika huu mwaka wa fedha wa 2021 mlishakaa na halmashauri yoyote ya Dodoma mkachambua mipango yao ya maendeleo na makusanyo yao; internal auditors mlishawahi kuwaita mkawauliza mnafanya kitu gani hawajawahi kufanya. Kwa hiyo, tunakwenda kuzifumua Sekretarieti za Mikoa, tunakwenda kujenga uwezo wa Sekretarieti za Mikoa kwa sababu sheria inasema wao wana wajibu wa kuzisimamia, kuzishauri na kuzijengea uwezo halmashauri katika masuala mazima ya mapato na maendeleo katika halmashuri zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika ofisi ya RAS kuna watu wanaitwa Katibu Tawala Msaidizi wapo kama sita, nane au kumi, wale watu ni wakubwa kuliko Wakurugenzi wa Halmashauri kwa sababu ni Assistant Directors; DED yuko chini ya RAS lakini sasa tumegundua kuna baadhi ya Wakurugenzi hawawaheshimu hawa ambao ni Makatibu Tawala Wasaidizi. Kwa hiyo, pia natuma salama kwa Wakurugenzi wa Halmashauri unapofuatwa na Katibu Tawala Msaidizi kumbuka ni bosi wako unatakiwa kumsikiliza, kumheshimu na kutekeleza maelekezo yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tumeona upande wa pili wa shilingi, kuna baadhi ya hawa Makatibu Tawala Wasaidizi wenyewe hawajiamini na hawana uzoefu. Sasa unaenda vipi kukaa na Mkurugenzi wakati wewe mwenyewe hujiamini na huna uzoefu, ndiyo maana nasema tunaenda kuzifumua Sekretarieti za Mikoa kwa sababu sitegemei Waziri wa TAMISEMI ndiyo azunguke nchi nzima wakati kuna Katibu Tawala wa Mkoa na wataalam zaidi ya tisa katika ofisi yako ambao wana jukumu la kisheria kusimamia halmashauri zetu. Kwa hiyo, hili tunaenda kulifanyia kazi na tutasaini performance contract na Wakuu wa Mikoa kwa sababu wao ndiyo wanasimamia hizi Sekretarieti za Mikoa. Kwa hiyo, ushauri huu tumeupokea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la posho za Madiwani kuna hoja mbili; hoja ya kwanza ilikuwa ni kuongeza posho za Madiwani. Tumewasikia Serikali iko hapa itafanyia kazi suala hili. Hoja ya pili ni kwamba posho hizi zilipwe moja kwa moja kupitia ruzuku ya Serikali. Tumelipokea pia na tunakubaliana na maoni ya Waheshimiwa Wabunge kwamba Madiwani wamekuwa wakifanya kazi kubwa na nzuri ya kusimamia shughuli za maendeleo katika majimbo yetu. Mimi nataka kukiri hata mimi nikienda Tanga Mjini namtafuta Diwani yule ndiye mpambanaji wangu, ndiye askari wangu.

Mheshimiwa Spika, tumefanya tathmini ya haraka haraka ya miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2017/2018 hadi 2019/2020 halmashauri 97 zimekusanya wastani wa mapato ya ndani chini ya shilingi bilioni mbili, halmashauri 71 zimekusanya wastani wa chini ya shilingi bilioni tano, ni halmashauri 17 tu ndizo zilizokusanya wastani ya mapato ya ndani ya shilingi bilioni tano kwa mwaka. Kwa hiyo, ni kweli kwamba halmashauri nyingi zinashindwa kulipa posho za Madiwani kikamilifu hali ambayo inasababisha kama alivyosema mtani wangu Mheshimiwa Kasalali kwamba Diwani anajiona ni dhaifu mbele ya Mkurugenzi kwa sababu ni Mkurugenzi atakavyoamua na kulipa posho anasema sina mapato. Kwa hiyo, hata ule usimamizi wa halmashauri maana mtu wa kwanza wa kusimamia fedha za Serikali kwenye halmashauri ni Baraza la Madiwani sio mtu mwingine ndiyo inakuja Regional Secretariat. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili naomba niseme tumelipokea na kwa kweli tunakubaliana na nyie kwamba ni sehemu ya kero, bugudha lakini pia kutoheshimisha kada ile ya Madiwani. Serikali imewasikia na tunaendelea kufanya uchambuzi. Tumeangalia tuna Madiwani takribani 5,275 inayojumuisha Madiwani 3,956 wa Kata na Madiwani 1,319 wa Viti Maalum. Niwaombe sana tulibebe hili twende tukafanye uchambuzi zaidi, ikiwemo posho ya Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, limezungumzwa suala la kuboresha mahusiano ya viongozi wa mikoa, wilaya ya halmashauri. Tunalipokea, tutaendelea kutoa elimu na mafunzo kwa viongozi wetu Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, ma-DAS, kuhusu kila mtu kutambua wajibu na mipaka katika kazi zake na majukumu yake na umuhimu wa kufanya kazi kama timu. Niseme tu tumekuwa pia tukishirikiana na Taasisi ya Uongozi kwa ajili ya kutoa mafunzo lakini pale ambapo kumekuwa na mgogoro pia tumekuwa wepesi wa kwenda kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, katika suala la utawala bora, kuna suala la matumizi ya force account, Wabunge wengi mmekubali kwamba ni utaratibu mzuri lakini pia ni kichaka cha upotevu wa fedha. Tunakuliana nanyi, tutaenda kuongeza nguvu ya kusimamia eneo hili lakini tukubaliane kwamba force account imetusaidia sana kwa sababu kuna maeneo Ofisi ya Jengo la Mkuu wa Mkoa tunaletewa bili ya bilioni 1.5 wakati sehemu nyingine inajengwa kwa shilingi milioni 300 au400. Kwa hiyo, tunakubali kwamba ipo haja ya kuimarisha ubora hususani kuwa na Wahandisi na watu wa QS katika halmashauri zetu. Habari njema kwa sababu tuna uhaba wa Wahandisi katika halmashauri zetu, tunao kama 80 katika halmashauri zote 184, tumeongea na Mkuu wa Majeshi ana Wahandisi katika Jeshi, kwa hiyo, tunamuomba ikiwezekana tuwashikize katika halmashauri zetu ili pia waweze kufanya kazi hii ya kutoa ushauri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la TAMISEMI isimamie na kuhakikisha fedha za uendeshaji katika ngazi za chini za kata na vijiji zinakwenda, hili tutalisimamia. Pia kuna masuala ya halmashauri zinazodaiwa na benki, mikopo ya Waheshimiwa Madiwani iliyotokana na dhamana ya posho za kila mwezi ikamilishwe, hili pia tumelipokea na madeni yameanza kulipwa, hadi Juni 30 madeni ya mikopo ya Madiwani yalikuwa shilingi bilioni 5.5 kati ya shilingi bilioni 10.9 ambazo zimelipwa.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la migogoro na kero za wananchi kwamba tuongeze jitihada za kuhakikisha kwamba tunatatua migogoro ya ardhi, wananchi kunyang’anywa mali zao lakini pia kuna mambo mengine ya mirathi. Nafurahi sana nimeongea na Waziri wa Katiba na Sheria simuoni hapa pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali tumeamua kuchukua hatua ya mpito tunakwenda kuwatumia Wanasheria katika Ofisi za Makatibu Tawala wa Wilaya ambao wapo tutawaongezea jukumu pia la kutoa huduma kwa wananchi katika halmashauri zao ambao wana matatizo ya kisheria hususani migogoro ya ardhi, mirathi pamoja na mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, masuala ya kiutawala yapo mengi Waheshimiwa Wabunge tumeyapokea, lakini kubwa ni kwenda kudhibiti makusanyo ya halmashauri pamoja na matumizi ya Serikali. Ukingalia bajeti hii shilingi trilioni tatu tunazipeleka kwenye halmashauri, maana yake ni lazima tuongeze nguvu ili fedha hizi ziweze kuleta matokeo yaliyokusudiwa.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, tumepokea maoni au ushauri wa Kamati pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwamba tuongeze umakini katika kusimamia sheria, kanuni na miongozo mbalimbali. Hili wala sihitaji kuchukua muda mrefu, tunakubaliana na ushauri na hususani kwanza kuhakikisha badala ya mikopo ile kuwa inatolewa kiduchukiduchu itolewe kwenye miradi mikubwa ambayo itaweza ku- generate ajira lakini pia itaweza kuleta mapato na faida kwenye halmashauri. Kwa hiyo, tutaweka mgao maana pia tusiwasahau hawa akina mama wangu wanaopika maandazi, wanaochoma mishikaki na vijana hawa wanaouza karanga, kwa hiyo, tunaweza tukasema katika kila hela ile inayotolewa kwa mikopo basi asilimia fulani iende kwa hawa wajasiliamali wadogowadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa kwenye mikopo tumeona ni marejesho kwa mfano katika bajeti hii ambayo tunaenda kuimalisha Juni zilitolewa karibu shilingi bilioni 26 lakini hakuna taarifa ya kiasi gani kimerudi. Kwa hiyo, hapo ndiyo tunaenda kupambana kwa sababu kama bajeti hii tumetenga shilingi bilioni 67 maana yake kwa miaka 5 tuna zaidi ya shilingi bilioni 120 maana yake itakuwa sasa tuna mfuko ambao ni endelevu utaweza kwenda kufanya kazi vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepokea ushauri kuhusu elimu kwa vikundi hivi pamoja na kuhakikisha tunawatumia vizuri Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii katika halmashauri zetu.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda nimalize hili la Mheshimiwa Munde Tambwe kuhusu kugawa Mikoa. Ni kweli tuna vigezo kwa ajili ya kugawa mikoa, majimbo, halmshauri na wilaya, niseme tu tumelipokea na tutalifanyia kazi kwa sababu hili pia lina gharama kwa kiasi fulani kwa upande wa Serikali, kwa hiyo, lazima pia tufanye tathmini. Kwa mujibu wa vigezo ambavyo nimeletewa, Mkoa wa Morogoro na Tanga unakidhi vigezo vya kuweza kupata Mkoa mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna hoja nyingine kama nilivyosema za Waheshimiwa Wabunge ambazo ni hoja moja moja tutazifanyia kazi hususani kwenye suala la elimu. Naomba niseme kwamba mimi ni mama na mnaonifahamu mnajua kwamba napenda sana Watoto. Kwa hiyo, katika kazi zangu asilimia kubwa nitasaidiana na Naibu Waziri Silinde kuhakikisha tunaboresha mazingira ya elimu kwa ajili ya watoto wetu. Hakuna urithi wowote wa maana ambao tunaweza kuwapa watoto wetu zaidi ya elimu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwenye hili tutalifanyia kazi kuhakikisha kwamba tunajenga madarasa na tumepokea ushauri wenu; Mheshimiwa Mzanva ndugu yangu Korogwe umesema pia tuangalie hata tunavyofanya mgao wa rasilimali fedha kwamba mwingine ana kata 15 mwingine anakata 35 wote unawapa maboma sawa. Kwa hiyo, hili tumelipokea tutaenda kulifanyia kazi, tutakuwa na minimum na maximum. Kubwa Waheshimiwa Wabunge naomba niseme angalau kila mtu apate, kila Mbunge aweze kwenda kwenye Jimbo lake aseme katika kipindi cha Ubunge wangu nimeleta moja, mbili, tatu, nne, tano. Kwa hiyo, hili tutakwenda kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kukushukuru wewe kwa kunipa fursa hii ya kuweza kujibu hoja za Waheshimiwa Wabunge siyo zote lakini zile za mojamoja Waheshimiwa Wabunge tumezipokea na tutaziletea ufumbuzi. Nimshukuru

Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini kusimamia Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Naamini Mwenyezi Mungu ataniongoza vema ili niweze kukidhi matarajio yake na matarajio ya Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango kwa ushauri na kufuatilia kwa karibu masuala ya mapato na matumizi ya halmashauri. Hata kama jana mliniona yale mambo mengine unakuta na Makamu wa Rais naye aliyapata, kwa hiyo, nami nayapata. Kwa hiyo, amekuwa akitupa msaada mkubwa katika kufuatilia masuala ya fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, nakosa maneno mazuri ya kumshukuru. Ukiwa na jambo lolote wakati wowote yuko tayari kukusilikiliza na kutafuta ufumbuzi wa jambo ambalo linakukabili. Mheshimiwa Waziri Mkuu mimi naamini Mawaziri wenzangu wengi tunajifunza kutoka kwako, kutojikweza, kuwa wanyenyekevu, kusikiliza na kutopandisha mabega katika utekelezaji wa majukumu yetu. Mwenyezi Mungu akuzidishie kheri Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimekushukuru wewe kwa kuongoza vema Bunge letu na hususani siku mbili umesimamia mjadala wa hoja yangu pamoja na Naibu Spika lakini kipekee kwa mchango mkubwa ambao umeutoa katika kuboresha huduma za elimu katika nchi yetu. Bunge High School itaendelea kuwa alama ya kazi yako kubwa na nzuri ambayo umeifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, labda sasa ndiyo changamoto tukatafute Bunge Boys School kwenye Bunge la Kumi na Mbili. Mimi nadhani Bunge la Kumi na Mbili tufanye mpango kwa ajili ya Bunge Boys School. Nataka kukuthibitishia na mimi ni mzazi tutahakikisha watoto wote wa kike na wa kiume wanapata haki sawa na huduma sawa za elimu na masuala mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru Naibu Spika kwa kusimamia vyema mjadala katika siku hizi tatu, lakini pia Waheshimiwa Mawaziri wenzangu nawashukuru kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Mbunge wa Kiteto TAMISEMI ni hati ya kila kitu. Kwa hiyo, sisi tunasikiliza miongozo na sera zenu, tuko tayari kutelekeza na tunawathibitishia hata mkituletea rasilimali fedha tutahakikisha zinatumika kikamilifu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango na ushauri lakini kwa ushirikiano mzuri mnaotupatia. Kipekee niishukuru Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, chini ya Mwenyekiti, Mheshimiwa Humphrey Polepole pamoja na Makamu Mwenyekiti, Mheshimiwa Abdallah Chaurembo kwa ushauri. Kama nilivyosema mafanikio ambayo TAMISEMI inapata ni kutokana na Kamati hii yenye watu wazuri wanaojikita na wako serious katika kuchambua hoja za Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitakuwa si lolote kama sitawashukuru wapiga kura wa Tanga Mjini. Nawashukuru sana kwa kunichagua kwa kura nyingi sana kuwa Mbunge wao. Ahadi yangu imekuwa ni kwamba badala ya kuifanya Tanga kuwa Jiji la mahaba na ukarimu linaenda kuwa Jiji la mahaba, ukarimu na maendeleo zaidi, kwa hiyo, ninawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee familia yangu nawashukuru kwa uvumilivu wao hususani napokosa muda wa kuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.