Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon Sagini Jumanne Abdallah

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Butiama

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. JUMANNE A. SAGINI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri, dada yangu Ummy na wadogo zangu Manaibu Waziri, nawafahamu ni wachapakazi kweli kweli, tuna imani na ninyi, mtafanya mambo makubwa. Imempendekeza Rais aweke Waziri na Manaibu wawili; ameweka Katibu Mkuu na Naibu Makatibu Wakuu wawili. Nadhani nia ni kuhakikisha kwamba TAMISEMI inachemka kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nawashukuru kabla sijaanza kuchangia moja kwa moja kwa namna mlivyo wasikivu na wasaidizi; miezi miwili iliyopita shule zangu mbili kule Butiama ziliungua moto; Shule ya Chief Ihunyo na Shule ya Bumangi Sekondari zote za A’ level, kwa kweli wepesi wenu wa kutatua tatizo lile umewatia moyo sana wananchi wa Butiama, walimu na wanafunzi wa shule zile. Endeleeni kufanya hivyo kwa Watanzania wengine. Mbali tu na kutimiza wajibu wenu, pia mnapata baraka za Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukisoma hotuba hii ya TAMISEMI, jukumu lao la kwanza walilolitaja ukurasa wa tisa inaendelea mpaka ukurasa wa 10, ni kusimamia utekelezaji wa Sera ya Ugatuwaji wa Madaraka D by D kutoka Serikali Kuu kwenda Serikali za Mitaa. Sera hii D by D wakati mwingine inazungumzwa, pengine nifafanue kidogo. Bahati nzuri ni- declare interest kwamba nimekaa kwenye sekta hiyo kwa miaka kadhaa, D by D inayotajwa inaweza ikatafsiriwa kama Decentralization by Delegation, Decentralization by Deconcentration and Decentralization by Devolution.

Mheshimiwa Spika, Tanzania tuliamua kuchukua mwelekeo wa Decentralization by Devolution ambapo unapeleka madaraka kikamilifu kwenye ngazi za chini kwa maana ya watumishi, fedha, ujenzi wa uwezo, lakini na kurekebisha mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Hizo nyingine tulizijaribu Tanzania kwa nyakati tofauti na hazikufanya vizuri sana, ndiyo maana Serikali ikaamua kwenda kwenye D by D ya devolution. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kwenye usimamizi wa rasilimali watu, inatakiwa tupeleke wa kutosha na wenye weledi. Ukiziangalia Halmshauri zetu, karibu kila Mbunge aliyezungumza ameongea kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi. Ukienda kwangu Butiama, nilishaieleza pale TAMISEMI; Idara ya Mipango, Idara ya Utumishi, Maendeleo ya Jamii, Ujenzi, Usafi wa Mazingira, vitengo vya ukaguzi wa ndani, TEHAMA, Ugavi, Uchaguzi, Sheria na Nyuki vyote vina makaimu; na bahati mbaya wengine wanaokaimu hawana hata sifa za kuja kudhibitishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hali iko hivyo kwenye upande wa Utumishi. watumishi wanatakiwa wawe wanne, yuko mmoja; Katibu Muhtasi wanatakiwa sita, yuko mmoja Halmashauri nzima; Idara ya Fedha wanatakiwa 11, wapo sita na kadhalika. Unaweza ukatoa mifano mingi, ukishuka kutoka Makao Makuu ya Halmashauri ukaenda ngazi ya chini. Sasa kama kweli tunataka Local Government ziweze kutoa huduma stahiki kwa wananchi, ukishakuwa na upungufu wa rasilimali watu wa kiasi hiki, itaathiri tu. Ndiyo maana sikushangaa Butiama kupata hati yenye shaka, kwa sababu ina watumishi wachache sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka juzi, 2018 TAMISEMI na Serikali kwa ujumla ilikubali walimu wapandishwe madaraja. Kwa sababu ya kuwa na Afisa Utumishi mmoja tu na mdogo, hana hata uzoefu, hakuna kilichofanyika. Walipandishwa watumishi 50, watumishi zaidi ya 348 walibaki bila kupandishwa madaraja. Hii yote ni udhaifu unaotokana na upungufu mkubwa wa rasilimali watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni suala la fedha. Ukiangalia duniani kote, property tax ni jukumu la msingi la local authorities, yaani wanakusanya mapato yale na wanatumia huko huko. Sisi hapa tumebadilisha equation, mapato ambayo ni ya msingi duniani kote ya local authorities yamepelekwa Serikali kuu halafu TAMISEMI na Local Government wanaanza tena kuomba.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesikia Idara ya Bajeti inajadili labda one third irudi, wakishakusanya irejeshwe. But what is justification? Hawa ndio wanaohudumia hiyo mitaa, ndio wanasafisha mazingira yale, lakini fedha zile za property zinakwenda juu halafu kurudi kwake ndiyo kama hivyo mnavyosema kwamba hazienei. Hatueleweki kwa wananchi. Nadhani ifike hatua tusaidie TAMISEMI ipate fedha stahiki iweze kutimiza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia bajeti ya Serikali, vis-à-vis bajeti ya TAMISEMI. Bajeti Kuu ya Serikali ni shilingi trilioni 36.258 na bajeti ya TAMISEMI ni shilingi trilioni 7.683. Maana yake shilingi trilioni 28.575 inabaki Serikali Kuu wakati TAMISEMI inahangaika na mikoa 26, Local Government 185. Hivi katika mazingira haya TAMISEMI inawezaje ikatoa huduma fanisi kwa wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninajua tuna deni la Taifa ambalo ni shilingi trilioni 10.663 ukizitoa pale, bado Serikali Kuu inabaki na shilingi trilioni 17.912. Hawa ni Wizara ambao ni occasionally kugusa wananchi ni kwa nadra, labda miradi mikubwa ya Kitaifa. Wanaohangaika na mazingira ya wananchi, usalama wao, barabara zao, maji yao ni local authorities, lakini bajeti walionayo inahuzunisha sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, athari zake ni nini? Ndiyo hapo tunajadili TARURA kupata kupata fedha kidogo, barabara hawezi kuzitengeneza. Ukirejea kwa mfano kule Butiama, ukienda Kata ya Buswahili, barabara ya Kiagata – Wegero - Kongoto, ukienda Bwiregi – Masuhura - Lyamisanga mpaka Kirumi kupitia Mang’ora, ukienda Kukirango – Kyabakari - Kamgegi mpaka Mugango, ukienda Butiama – Muriaza – Kibubwa - Mwikoko - Masurura ni maeneo yasiyopitika kabisa. Sasa watawezaje hao TARURA kufanya kazi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati inaanzishwa hii Taasisi ya Road Board, kilometa za barabara zilikuwa 58,000, leo wana zaidi ya 100,000 lakini equation ya location ya resource ya Road Board Fund ni thirt by seventy, justification iko wapi? Tutamlaumu TARURA, tutamgawana, lakini kwa uwezo alionao hawezi akarekebisha hizi barabara zetu, labda kutokee miujiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utaona kuna maboma mengi ya madarasa, zahanati, ofisi kutokamilishwa, ni kwa sababu ya under financing. Ukienda head quarter za local authorities, kwa mfano Butiama, Makao Makuu hayajakamilika, certificate wanaleta, inachukua muda kuleta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Makao Makuu. Nyumba za viongozi angalau ya DC imekamilika pale Butiama, lakini hana ofisi, Halmashauri jengo halijakamilika na viongozi hawana hata nyumba na ni wilaya mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, malalamiko ya posho za Madiwani ni rampant every where, posho zenyewe ni kidogo. Tungekuwa tunajenga hoja kwenye posho za Madiwani, Wenyeviti vya Vijiji, Wenyeviti wa Vitongoji zifikiriwe kuwekwa. Kwa kiwango hiki, ni shida kabisa! Ushauri wangu kwenye hili, Serikali iangalie vigezo vya kugawa financial resources kwa ngazi zake zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni yale mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Naomba kushauri, TAMISEMI ikubali kujenga uwezo wa Wizara nyingine wajue dhana ya D by D ili waweze kuwa-support kwenye utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, nakushukuru sana na ninaunga mkono hoja. (Makofi)