Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja na Wizara ipokee kwa makini sana mchango wangu ufuatao:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Nkasi Kusini lina matatizo ya kijiografia linalosababisha wakati wa kufanya mitihani ya darasa la saba watoto hulazimika kuhamia shule nyingine, karibuni shule zaidi ya kumi huathirika na suala hili. Kwa nini Wizara isisimamie kukomeshwa kwa adha hii au basi vyombo vya usafiri majini vinunuliwe ili vitumike kuwasafirisha wasimamizi ambao wanaogopa kutumia usafiri wa boat zinazotumiwa na wakazi wa eneo la Mwambao wa Ziwa Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa Walimu Wilayani Nkasi, hasa eneo la Mwambao wa Ziwa Tanganyika. Jimbo la Nkasi Kusini lina uhaba mkubwa sana wa Walimu wa shule ya msingi na sekondari na hasa eneo la Mwambao wa Ziwa Tanganyika ambako Walimu ni wachache kwa kila shule. Walimu hawa pia hawana nyumba za kuishi pamoja na ukosefu mkubwa wa madarasa katika shule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu maalum. Wapo watoto albino na walemavu wengine, mashuleni kwetu sekondari na hata shule za msingi pia. Naomba kuwapa msaada wa visaidizi ili waweze kumudu masomo, nina maana wakisajiliwa katika shule ifanyike assessment kujua mahitaji yao na shule zielekezwe kuwatimizia mahitaji hayo kutoka kwenye ruzuku hiyo hiyo inayotolewa mashuleni kote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za walemavu zitunzwe na tuhimize shule na vyuo walikosoma kufuatilia maendeleo yao ili hatimaye waje wapate ajira. Mtiririko huu uzingatiwe pia mara zinapotoka ajira mbalimbali ili kupunguza utegemezi wa walemavu walioendelezwa na kuwa na sifa za kuajirika, watengewe nafasi kabisa na ziwekwe wazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, albino walindwe, wapewe mafuta ya kuwasaidia na wajulikane walipo na Kamati za Ulinzi na Usalama. Wao au familia zao wapewe simu na Kamati za Usalama za maeneo yao ngazi ya wilaya kwa ajili ya mambo ya dharura kiusalama. Nao hawa wajulikane wanaoendelezwa ili kuwekwa kwenye akiba ili zitokeapo nafasi za ajira wajulikane kwa nafasi walizotengewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wanafunzi waliositishwa masomo kwa makosa yaliyofanywa na Board, haikubaliki na lazima Wizara itafute ufumbuzi mwingine na siyo hatua yake ya kuwafukuza vijana vyuoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya madawati katika shule za msingi ni kubwa na kuacha halmashauri au wilaya kutafuta wenyewe namna ya kumaliza upungufu kutaathiri miradi mingine mawilayani kama ilivyokuwa kwenye mpango wa ujenzi wa maabara. Ushauri; lazima Serikali itenge fedha kushughulikia tatizo hilo na siyo maagizo ya kutia hofu na kuwafanya Wakurugenzi na ma-DC kutafuta mbinu mbadala, hivyo fedha itafutwe Hazina.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo cha Maendeleo Chala, Wilayani Nkasi. Chuo hiki tangu miaka miwili iliyopita kilianza kutoa mafunzo ya VETA; naomba kiwe miongoni mwa chuo cha kutoa mafunzo hayo rasmi na kiendelezwe katika miundombinu yake na hasa ukizingatia Mkoa wa Rukwa hauna chuo chochote cha ufundi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya watoto wa kike shuleni. Nashauri, pamoja na changamoto zilizopo mtoto wa kike asinyimwe fursa ya kusoma kwa njia au mfumo rasmi pale anapopata mimba ili atimize malengo yake na pale inapotokea adhabu ya upande wa mwanaume anayesababisha mimba apewe adhabu ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shule za msingi ziendelezwe au kila kijiji kianzishe shule ya sekondari kwa sababu elimu ya sekondari itakuwa elimu ya lazima kufikiwa kumbe tujiandae mapema kuandaa majengo, uamuzi huu wa Serikali kuwa kila mtoto afikie form IV bila malipo utakuwa na matokeo ya kukosa vyumba vya madarasa na miundombinu ya kiwango cha sekondari. Nawasilisha.