Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami nashukuru kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia Wizara ya TAMISEMI.

Mheshimiwa Spika, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri Ummy kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa TAMISEMI na wasaidizi wake wote. Nimekuwa hapa katika miaka yangu mitano, namjua uwezo wake na ninajua yupo sehemu sahihi. Kwa hiyo, nampongeza sana.

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba nichangie katika suala la TARURA. Katika Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2020 – 2025, ukurasa wa 71 - 82, Serikali imesema itajikita kuongeza fedha TARURA ili iweze kupambana na matatizo yake au kutatua matatizo yake kuhusiana na barabara.

Mheshimiwa Spika, kama walivyosema Wabunge wenzangu TARURA ni taasisi ambayo kwanza inafanya Wabunge wengi tuweze kuonekana kwamba hatufanyi kazi especially sisi Wabunge wa Mjini ambao tunatakiwa kuonekana kwamba barabara za mitaa zinatengenezwa, lakini pia barabara zingine. Kutokana na huu ufinyu wa bajeti wa TARURA na kwa sababu tumekuwa tukienda nao kila mahali, tunaahidi haya mambo na hayatokei.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hii imetufanya sisi Wabunge hasa wa mjini kuonekana kwamba hatufanyi kazi kabisa na tunakuja tu huku Bungeni kwa ajili ya kuuza sura. Sasa naomba Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mama Samia wakati anawaapisha Makatibu, alitoa kauli alisema kwamba, Manispaa ambazo zinakusanya pesa nyingi ziweze kutenga asilimia fulani kwa ajili ya kutengeneza barabara zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Dar es Salaam, Manispaa zote zinakusanya pesa nyingi. Ukianzia na Manispaa ya Ilala, lakini cha kushangaza pamoja na kwamba Manispaa ya Ilala ndiyo tunaongoza kwa mapato, lakini bado wananchi wetu wanaotuchangia wanatembea kwenye barabara mbovu sana. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Waziri Ummy, kwa sababu Mheshimiwa Rais wakati anatoa hii kauli nafikiri Wakurugenzi na Wataalam wetu walikuwa wameshakaa vikao vyao na wameshapanga bajeti. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy aweze kulitolea kauli hili jambo la Mheshimiwa Rais kwamba Wakurugenzi watatenga vipi fedha kuhusiana na barabara zetu za mitaa.

Mheshimiwa Spika, ufinyu wa bajeti umefanya Mkoa wa Dar es Salaam kuonekana barabara zake ni mbovu sana. Mfano Jimbo langu la Segerea, katika miaka mitano TARURA wameshindwa kujenga barabara ya Airport – Karakata ambayo ina urefu wa kilometa moja na nusu. Tumekuwa tunaahidi kila mwaka lakini barabara haijengwi na lile eneo la Airport ni eneo ambalo wageni wote wanaokuja, yaani ni kama mlango wa Tanzania. Wageni wanapofika tu pale ina maana wanakutana na barabara mbovu. Kwa hiyo kama Mheshimiwa Ummy atatoa kauli hii kwa Wakurugenzi wetu ili waweze kuangalia ni sehemu gani ambayo ni vipaumbele ambavyo sisi tumeviweka kwa ajili ya kuboresha mazingira basi itakuwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TARURA hao hao kuna barabara sasa hivi inajengwa; Barabara ya Vingunguti – Barakuda wameijenga kuanzia mwanzo mpaka katikati, wameishiwa na pesa, kwa hiyo barabara hii imefungwa. Hii inawasababishia wananchi matatizo makubwa, ina maana daladala haziwezi kupita pale, hakuna usafiri wowote ambao unaweza kupita pale na imekuwa pia ni changamoto kwetu sisi Wabunge, ina maana ukiamka tu asubuhi unakutana na hayo matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia TARURA hii hii pamoja na ukusanyaji mkubwa wa mapato wa Wilaya ya Ilala, kuna barabara ambazo za Kimanga, barabara ambayo ni kilometa mbili imejengwa kwa miaka mitano. Vile vile TARURA wameshindwa kumalizia Barabara ya Liwiti - Chang’ombe, mpaka sasa hivi haijawahi kumaliziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy na najua kabisa ana uwezo huo, aweze kuitolea kauli hasa Mkurugenzi wetu wa Manispaa ya Ilala. Kwanza napenda nichukue nafasi hii kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa kazi kubwa anayoifanya. Kwa kweli Mkurugenzi wetu ni mchapakazi, lakini pia anafanya kazi nyingi kwa ajili ya kutusaidia na tunaelewana vizuri. Kwa hiyo namwomba Mheshimiwa Ummy atoe kauli ili sisi sasa tuweze kutengenezewa hizo barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka kuliongelea ni jambo la kuhusiana na DMDP. Najua pia hii DMDP ipo TAMISEMI. Mheshimiwa Mama yetu Mama Samia alikuja katika Wilaya ya Ilala, ndiye aliyezindua kampeni na matatizo aliyoyakuta pale yalikuwa ni matatizo ya barabara. Pia kuna ahadi ambazo tumezitoa pale kuhusiana na Mradi wa DMDP naongea hivyo kwa sababu huu mradi wa DMDP kuna hati hati kwamba umefutwa. Kwa hiyo tuna ahadi pale ambayo tuliahidi na Mheshimiwa Mama Samia. Jimbo la Segerea kuna matatizo makubwa, kwanza tuna bonde la Mto Msimbazi ambalo tuliahidi kwamba ikifika mwezi Januari tutaanza kuweka kingo.

Mheshimiwa Spika, mpaka sasa hivi ni mwezi Aprili kingo hazijaanzwa kuwekwa na wananchi wanaendelea kupata mafuriko na wananchi wanaendelea kuhama. Kila mwaka wanahama zaidi ya wananchi elfu arobaini katika Jimbo la Segerea, kwa sababu ya hilo bonde la Mto Msimbazi. Kwa hiyo tunaomba Serikali iweze kuamua hili jambo na kuweka hizo kingo ili wananchi waweze kama tulivyoahidi kwamba tutalitengeneza hili Bonde la Msimbazi ili wananchi waendelee kukaa lakini pia na maji yaendelee kupita. Kwa hiyo tunaomba hicho kitu kisitolewe.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni barabara zetu za DMDP ambazo tumeziahidi tukiwa na Mheshimiwa Mama Samia kwamba barabara hizi kuna wananchi kule wanasubiri na wanajua kwamba tumeahidi kuna barabara ambazo zitajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika Wilaya ya Ilala hasa huku kwetu Mheshimiwa Zungu anapenda kusema maji matitu Segerea, water table yetu ipo juu sana, kwa hiyo mvua ikinyesha kidogo hata hizi barabara ambazo tunaziwekea changarawe zinakuwa haziwezi kufanya kazi. Kwa hiyo nilikuwa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Bonnah, tayari muda wako.

MHE. BONNAH L. KAMOLI: Mheshimiwa Spika, ahsante na naunga mkono hoja. (Makofi)