Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Anna Joram Gidarya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ANNA J. GIDARYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Elimu inakabiliwa na changamoto nyingi sana ikiwepo ya kuandaa miundombinu ya elimu yenyewe. Changamoto nyingine ni:-
(i) Ubora wa elimu kuanzia ngazi ya msingi hadi vyuo vikuu;
(ii) Uhaba wa madarasa na Walimu kwa shule nyingi hasa Walimu wa masomo ya sayansi;
(iii) Upandishaji wa madaraja mserereko kwa Walimu;
(iv) Uhamisho wa Walimu holela pasipo kulipwa haki zao stahiki na hata posho za uhamisho; na
(v) Uhaba wa nyumba za Walimu/mazingira magumu wanayoishi Walimu;
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu yetu Tanzania haina ubora kuanzia ngazi ya msingi kwa kuwa tunabadilisha mitaala ya elimu kila mara jambo ambalo ni kinyume na taaluma halisi ya Walimu waliyosomea. Hii ni changamoto kubwa kwa Walimu hata katika maandalio ya somo. Haya ni mazingira magumu sana kwa Walimu hata katika maandalio ya somo. Haya ni mazingira magumu sana kwa Walimu na wanafunzi wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Manyara ni mmojawapo ya Mikoa inayokabaliwa na changamoto ya uhaba wa Walimu na majengo ya nyumba za Walimu na madarasa ya kufundishia watoto. Walimu wengi wanaishi katika mazingira ambayo ni hatarishi na si rafiki kabisa kwa Walimu wetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia Wizara kuwapandisha Walimu madaraja kwa mkupuo (madaraja mserereko) bila kupandishiwa mishahara. Kwa muda mrefu na hadi sasa bado kero hizo zinaendelea na bado Wizara imekaa kimya bila kutoa tamko kama Walimu hawa watalipwa madai yao ya kupandishwa madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na tabia ya Wizara kuhamisha Walimu pasipo kuwa na sababu za msingi lakini pia Walimu hawa hawapewi posho za uhamisho wala disturbance allowance. Mpaka sasa katika Mkoa mzima wa Manyara zaidi ya Walimu 160 wanadai hayo madeni ya msingi kwa Serikali hii takribani miaka zaidi ya kumi na mbili (12) bila kufikiriwa na hata kupatiwa majibu yanayoleta matumaini kwa Walimu hawa, wamebaki na maumivu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uhaba wa nyumba za Walimu ni kero kubwa kwa Mkoa mzima wa Manyara. Katika shule moja ya msingi Haraa iliyoko katika Mji wa Babati, Walimu wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi. Nyumba yenye vyumba viwili wanakaa Walimu nane (8) wa kiume, nyumba yenyewe haina madirisha wala haijasakafiwa ni nyumba ya udongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nina mapendekezo yafuatayo:-
(i) Serikali itoe rai kwa Wizara ya Elimu kuhusu mambo yote ambayo ni kikwazo kwa sekta nzima ya elimu kushughulikiwa haraka ili kuokoa muda na kuokoa jahazi la elimu;
(ii) Posho za Walimu zilipwe kwa wakati baada ya madai hayo kufanyiwa uhakiki na malipo yafanyike kwa kila Mwalimu anayedai madai yake;
(iii) Nyumba za Walimu zijengwe za kutosha ili kuondoa kero na adha wanayopata Walimu wetu na kuwaondoa Walimu wetu katika mazingira hatari ya ufundishaji; na
(iv) Serikali irudishe utaratibu ule wa mwanzo wa wanafunzi kufundishwa masomo ya elimu ya kujitegemea ili wapate elimu bora ya kukabiliana na mazingira pindi tu wanapomaliza elimu ya msingi na hata elimu ya sekondari na kupunguza mzigo wa kutegemea ajira ya Serikali tu. Ahsante.