Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Pia nimpongeze waziri kwa hotuba nzuri ambayo ame-present hapa na timu yake kwa ujumla. Sitakuwa mbali na wachangiaji wenzangu waliotangulia, ningependa nijikite katika suala la TARURA pia, ila sitajikita zaidi katika kulalamikia mazingira nataka kutoa ushauri. Nitoe ushauri hasa kwenye mgawanyo wa fedha kama Waziri ama Serikali ipo hapa itatusikia, itakuwa vizuri zaidi maana nimekuwa najaribu kupitia.

Mheshimiwa Spika, ukijaribu kuangalia network ya barabara ambayo ipo chini ya TANROADS naambiwa ipo chini ya TARURA, TARURA wanahudumia barabara nyingi zaidi. Hata hivyo, kuhudumia barabara nyingi zaidi si sababu tu, ni kwamba pesa kubwa inayoelekezwa TANROADS ku- maintain barabara ambazo zimejengwa kwa gharama kubwa zaidi ambazo tunajua ziko durable zaidi, naona haina uwiano halisi na fedha zinazoelekezwa TARURA ku-maintain barabara za vumbi, barabara za changarawe na barabara za udongo kwa sababu nadhani wana kilokita 78,000 za barabara za undogo. Sasa barabara ya udongo always mvua inaponyesha, barabara ile sio barabara tena inakuwa tope na uharibifu unaanzia hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili, TARURA wanahudumia sehemu ambayo wengi wa wapiga kura na watu ambao wametuchagua kutuleta hapa wanaishi huko kwenye hayo mazingira. Kwa sababu ni barabara ambazo ziko kwenye Serikali za Mitaa, ahadi tulizozunguka tukaliliwa barabara na wananchi, hawakuwa wanatulilia barabara za lami zile kubwa hapana, sehemu kubwa ya nchi imeshaunganishwa. Walikuwa wanalia na barabara za vijijini, barabara zile ambazo wakulima wapo kule wanalima lakini wanashindwa kutoa mazao na watu wanaumwa wanashindwa kufika kwenye hospitali. Hizo ndizo barabara ambazo hata sisi wakati wa kampeni walio wengi humu, tumeletwa hapa na wananchi walituuliza tukasema tutazishughulikia. Sasa niiombe Serikali, kama hawataweza kutusaidia kwenye suala hili, wakajaribu kuangalia mgawanyo mpya, aidha kama wanaona ule mgawanyo uendelee kubaki TANROAD, basi waje na alternative ya kupata fedha ili tuweze kupata fungu kubwa kwenye upande wa TARURA ili iweze kutusaidia sisi kama Wabunge na hasa wananchi ambao wako kule vijijini.

Mheshimiwa Spika, lipo jambo kwa upande wangu nilikuwa najaribu kuliangalia kwenye wilaya yangu. Nilivyozunguka kwenye kampeni na sehemu kubwa kitu ambacho nilikiona, wananchi hasa wa upande wa vijijini, naomba Serikali wajikite kwenye kujenga madaraja. Huko vijijini wananchi wanachokwama zaidi ni madaraja, maana utakuta mvua imenyesha, mtu anaumwa, kuna bodaboda ndio usafiri, vijijini hawatumii magari kwa sehemu kubwa, labda nyie kwenye wilaya zenu, lakini kwangu sehemu kubwa za vijijini wanatumia bodaboda, wanatumia miguu na baiskeli. Kwa hiyo, mvua zinaponyesha kwenye msimu huu, kuna sehemu madaraja hayapitiki kabisa, unakuta daraja limefunga kata mbili, limefunga vijiji sita, limefunga vitu vingapi, kwa hiyo wajaribu kutusaidia. Fedha nyingi ya TARURA ielekezwe kwenye ku-maintain madaraja.

Mheshimiwa Spika, kujenga madaraja sio kitu kigumu, kuna makampuni hapa yanatengeneza mabomba yale makubwa, bomba linaenda mpaka three meters, hata kama ni kina kikubwa sana, wapo Pipe industries, wapo PLASCO tunajua. Ukienda hata Ngorongoro Craters kule chini, mabomba yanayotumika sasa hivi kutengeneza madaraja kule mbugani ni mabomba ya plastiki. Kwa hiyo wangeweza kwenda kununua, lile halihitaji mkandarasi, mtu tu wa kawaida, a normal technician anaweza kufanya ile kazi kule kijijini. Kwa sababu atachimba na wananchi, wataingiza lile bomba pale na watafukia, watajengea cement huku na huku basi kitu kinaenda. Ile Force Account wanayoitumia huko TARURA kwenye madaraja vijijini inaweza ikatusaidia zaidi tukaweza kupunguza gharama lakini tukasaidia watu wengi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, nataka niongelee suala la shule. Niipongeze Serikali kwa kazi kubwa ambayo wanazidi kuifanya. Nadhani kwa record kubwa tuna kikosi kukubwa sana ambacho tunategemea tutaanza kukipokea kwenye shule za sekondari, nadhani miaka miwili au mitatu, maana mazao ya elimu bure ile sasa ambayo Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliianzisha, tunaanza kuipata nadhani miaka miwili au mitatu ijayo. Wale ambao waliingia darasa la kwanza bure, nadhani sasa hivi wako darasa la sita, either wengine wanaelekea la tano, kwa hiyo ule wingi mkubwa tunaanza kuuona huko. Sasa naomba Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, tunaomba waje na mpango mkakati wa miaka hii miwili au mitatu inayokuja, ili waweze kutusaidia, maana Watoto kule vijijini ni wengi na wale watoto wana akili watafaulu, kwa hiyo tunachotegemea, wasifaulu wakaishia kubaki vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivi kwa sababu sisi kama wawakilishi tutakuja na kazi nyingine ya kurudi kwa mzazi anayekwambia mimi bwana mtoto wangu amefanya vizuri lakini amekosa shule. Mimi Mbunge siwezi kujenga shule, lakini Serikali inaweza kujenga shule, kwa hiyo watusaidie. Nataka nitoe mfano hapa, kwenye jimbo langu kuna shule moja ya msingi kwenye Kata ya Nemba, shule nzima ina wanafunzi 4,819, ila ina vyumba tisa vya madarasa. Kuna maboma matatu sasa hivi wananchi wanahangaika ndio wanayanyanyua matatu mengine, Wizara ingeweze kutusaidia kuyaezeka sasa angalau wawe navyo 12.

Mheshimiwa Spika, lakini nilipokuwa napitia hii shule, ni shule ya kata. Darasa la saba sasa hivi wako 276, la sita wale wako 703 kwenye shule moja tu. Hii shule inahudumiwa na shule moja ya sekondari ambapo shule moja ya sekondari ukiangalia watoto walioko darasa la sita maana yake walioko form three leo wanavyoondoka kumaliza form four wao ndiyo watapisha room kwa ajili ya watoto walioko darasa la sita. Sasa form three wako 999 hawafiki hata 100 lakini shule hii ita-release watoto zaidi ya 700 wanaingia sekondari. Of course, hata wakifeli labda haiwezi kuwa chini ya asilimia 90 maana kwa Kagera Biharamulo sisi hatujapungua chini ya asilimia 95 kwneye ufaulu wa primary.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nina uhakika watoto si chini ya 600 kutoka kwenye shule moja tu wanatakiwa waende sekondari. Sasa wanaendaje sekondari kwenye shule ambayo leo inatoa wanafunzi 99 inapokea zaidi ya 600. Na hawa 600 ni kwenye shule moja ya msingi na hii shule ya sekondari inahudumia shule za msingi takriban nne. Kwa hiyo, ninategemea hawa watoto zaidi ya 1,000 watakuwa wanafaulu kwenda form one. Sasa shule hii mjaribu kutusaidia. Kwa hiyo ningeomba sasa Mheshimiwa Waziri mje na kikosi maalum cha kuzunguka kwenye kata. Shule hizi za kata tulizozianzisha za haraka haraka hizi zinaenda kuzaa matunda. Zisizae matunda watoto hawa wakabaki mtaani maana wengine ni darasa la saba akimaliza kabaki mtaani anafanya nini? Hatuna vyuo vya ufundi sehemu hizo maana ziko kwenye kata bado. Kwa hiyo, mtusaidie kwenye hilo ili watoto hawa tuwatoe hapa walipo tuweze kuwasogeza mbele zaidi na wao wayafikie malengo ya kuwa madaktari, wahandisi, walimu, maaskari, wanasheria na kada nyingine ambazo wanategemea wazifanye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pili wakati wa kampeni mwaka jana kuna jambo lilijitokeza. Huenda lilikuwa nchi nzima au lilikuwa kwenye wilaya yangu ya Biharamulo lakini naongelea kwa experience yangu. Suala la vitambulisho vya wajasiriamali. Suala la vitambulisho vya wajasiriamali mwaka jana lilileta saga sana Biharamulo. Watu wakawa wanaona sasa wanalazimishwa kuwa na vitambulisho vile, vurugu zikawa kubwa sana lakini baadaye kwa busara yale mambo yakaja yakatulia. Sasa juzi wiki iliyopita wenzetu waislamu wameanza mfungo siku ya Jumatano. Biharamulo tuna gulio siku mbili, tuna gulio siku ya Alhamisi na tuna gulio siku ya Jumapili sehemu ile ambayo sasa hata wakulima na yeyote yule anayejisikia kuuza anakuja sokoni kuuza.

Mheshimiwa Spika, ningeomba sasa maelekezo mahsusi yatolewe. Tutofautishe wakulima wa kawaida na wafanyabiashara wadogo wadogo. Kuna mama yangu kule kijijini anabeba ndizi, shilingi 5,000 ukipeleka ndizi sokoni na basically unachoenda kukifanya sokoni ni barter trade. Mtu analeta mkungu wa ndizi shilingi 5,000… (Makofi)

SPIKA: Engineer muda sasa.

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Spika, nimalizie dakika moja. Mtu analeta mkungu wan dizi shilingi 5,000. Anavyofikisha mkungu wa ndizi shilingi 5,000 akimaliza kuuza anaondoka na chumvi, sukari, habaki hata na shilingi ya hela. Lakini mtu anataka yule mtu awe na kitambulisho cha 20,000. Ndugu zangu tuliozaliwa vijijini tunajua, kuna watu huko unamuuliza leo ni mzee, hajawahi kuwa hata na shilingi 5,000 mfukoni. Ukimuambia atafute shilingi 20,000 na kukata kitambulisho ili alete ndizi sokoni tunamuumiza. Kwa hiyo ningeomba hilo jambo tuliangalie tuweze ku-harmonize hao watu ili situation irudi kawaida na hakika Serikali hii ni Sikivu mtaweza kutusaidia ili wananchi wetu huko waweze kufanya kazi anayeuza auze, anayelima alime lakini wafanye kazi kwenye mazingira mazuri. (Makofi)