Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

Hon. Njalu Daudi Silanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Itilima

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala Za Mikoa Na Serikali Za Mitaa

MHE. NJALU D. SILANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Kwanza nianze kumshukuru Waziri pamoja na Manaibu wake wawili pamoja na Makatibu Wakuu kwa kazi nzuri ambayo wanayoifanya katika Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nitoe ushauri katika maeneo ambayo katika hotuba yao wameelezea. Wamezungumza suala la elimu, tuko na maboma mengi sana kwenye halmshauri zetu nchini, ambayo wananchi wamejenga kwenye kwa nguvu zao, lakini Serikali imeendelea ikileta fedha kidogo kidogo na kuanzisha miradi mipya. Ningetoa ushauri kwa sababu ile miradi inasimamiwa na halmashauri, fedha zinazopatikana angalau zingekuwa zinakwenda kumalizia zile nguvu za wananchi ambazo tayari majengo yalishajengwa kwa maana ya zahanati, vyumba vya madarasa, pamoja na maabara ambavyo itatusaidia. Jambo hili litawatia moyo wananchi kwenye maeneo yetu kwamba Serikali sasa inakuja kuunga nguvu ya madarasa, zahanati kwa yale ambayo yamejengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yake Mheshimiwa Waziri amezungumza ataanzisha sekondari, kwenye wilaya yangu nina kata 22, lakini nina kata mbili ambazo hazina sekondari, lakini kata zile mbili, tayari wananchi wameshajenga, Kata moja ya Nkuyu imejengwa kupitia kusaidiwa na TANAPA, tumejenga madarasa manne na yamekamilika bado hatujapata utawala pamoja na nyumba za Walimu. Ningeomba tu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa sasa kwenye mpango huu watuletee hizo fedha kumalizia haya maeneo mawili ikiwepo Ndobola pamoja na Nkuyu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, TARURA; kwenye eneo lao la hotuba yao wameelezea vizuri sana kufungua fursa za kiuchumi. Uchumi hauwezi ukaufungua kama wananchi hawafikiwi na huduma ya barabara pamoja na zingine. Ningeiomba Serikali pamoja na kile kidogo kinachopatikana, muundo huu wa TARURA wajaribu kuungalia vizuri. Sasa hivi mamlaka yote yapo mkoani, Afisa aliyeko kwenye halmashauri hiyo, yuko peke yake na wasaidizi wake. Kwa hiyo chochote kinachotolewa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kinafika tu taarifa, mamlaka yote yatafanyika mkoani na baadaye ndio yatashushwa huko kwenye halmashauri. Hatuwezi kwenda na speed tunayoitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo hili ni muhimu sana, ukizungumza Diwani au Mbunge hawezi kuwa kila wakati anakwenda mkoani kwenda kuuliza, barabara yangu imefikia hatua gani, tender imetangazwa lini, yaani ni changamoto na ukiangalia kwenye hotuba yao wameelezea vizuri kwamba barabara zinazopitika ni asilimia 15. Sasa angalia nchi nzima ina halmashauri 180, ina ukubwa wa eneo gani na mahitaji ni katika maeneo yapi, lakini bado kunakuwa na changamoto hapa. Huwa najiuliza mtu wa TARURA yupo chini ya Ofisi ya Rais na Mkurugenzi yupo chini ya Ofisi ya Rais, kuna nini hapa katikati, haya mahusiano ya watu wawili kati ya Mkurugenzi na Msimamizi wa TARURA wakawa kitu kimoja na wakafanya kazi kwa pamoja. Likifanyika hili litatusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo changamoto kubwa ya madaraja yanaunganisha kati ya wilaya nyingine na Wilaya ya kwangu Itilima. Watu wa Itilima hawawezi kutoka Itilima kwenda Bariadi mvua zikinyesha, kuna daraja linaitwa Bulolambesi. Wangetusaidia TARURA, watutengee bajeti kwa sababu bajeti inayokuja haitoshi kabisa kukidhi mahitaji katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna jambo tumelizungumza sana. Mimi napakana na watu wa Kwimba na Mheshimiwa Marehemu Ndasa tulizungumza Bunge lililopita tukielezea daraja la Sawida na hilo linaunganisha Mkoa wa Mwanza na Wilaya ya Itilima na Wilaya ya Maswa. Ningeomba watutengee kwenye bajeti hii, daraja lile lijengwe. Vile vile tunayo madaraja madogo madogo ambayo yanaunganisha kata na vijiji kwenye maeneo yetu, tunayo changamoto kubwa kwenye Daraja na Nhomango, nadhani wataalam kwenye kumbukumbu zao zipo, Walimu wanaofundisha wanatoka toka kata nyingine kwenda kijiji kile husika. Mvua ikinyesha Walimu hawawezi kwenda kutoa huduma katika Kata ya Nhomango. Nalo ningeomba Serikali iweze kututengea hicho kilichopo, ili maeneo hayo yaweze kupata huduma safi na salama,wananchi wetu waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais, hayati Dkt. John Pombe Magufuli, lakini kuna ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye kampeni alipokuja kuzindua pale makao makuu. Tulimwomba lami, Mheshimiwa Waziri Ummy Mwalimu, Makamu Makuu ya Lagangabuli ameshafika, tunamwomba sana angalau Wasukuma pale Lagangabuli wapate lami, wamkumbuke mtani wangu kwa kazi kubwa ambayo atakuwa anaifanya kama alivyosema mwenzangu, ameingia na yeye ni jembe kama jembe lililokuwepo kwenye eneo hilo husika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika vijiji vyetu, Serikali hii ya Awamu ya Sita naamini kwenye hotuba hii waliyoizungumza, watafanya mambo mengi na makubwa na matarajio ya Watanzania tunahitaji yale ambayo wameweka kwenye hotuba yao yaweze kujibu na yaweze kuleta mabadiliko makubwa sana, hasa kwenye sekta ya afya. Wametutajia fedha nyingi ambazo wamezitenga, naamini kabisa kwa usimamizi mahiri fedha hizi zitafika na zitafanya kazi vizuri sana na sisi kule kama Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani tuko tayari kutoa msaada na ushirikiano wa hali ya juu ili kusudi azma ya Serikali ya Awamu ya Sita iweze kufikiwa kwa kutimiza malengo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunacho Kituo cha Afya Kabale, kuna daraja na bahati nzuri Naibu Waziri wa Afya ni mwenyeji kwenye maeneo yale. Kile kituo mvua ikinyesha hakifikiki, naomba kutoka Nzanzui kwenda Kabale watuwekee angalau fungu kidogo ili eneo hilo liweze kupitika; Kabale pamoja na Lalang’ombe.

Mheshimiwa Spika, baada ya haya machache, naunga mkono bajeti ya Rais kwa asilimia mia moja. Ahsante sana. (Makofi)