Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Daniel Awack Tlemai

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karatu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia bajeti ya ofisi ya Waziri Mkuu. Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye ametupigania uhai sote tukiwa salama ndani ya ukumbi huu. Awali ya yote nishukuru sana Chama changu lakini vile vile nishukuru sana Serikali ya awamu ya tano, kwa kazi kubwa sana waliyofanya kazi hiyo kubwa waliyofanya imeweza kuleta Wabunge asilimia kubwa ndani ya ukumbi huu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Spika, kwa wale wana CCM waliopitia Chama Cha Mapinduzi wanajua kwamba, chama chetu mwaka wa 2010 ilikuwa na hali gani? Lakini vile vile, unajua changamoto tuliyokuwa nayo mwaka 2015. Lakini baada ya jemedari Hayati Dkt. Magufuli kuingia madarakani mwaka wa 2015 na ndio matunda sasa yameonekana kwa watanzania, kuamini Chama Cha Mapinduzi mwaka wa 2020 kwa kazi kubwa iliyofanyika chini ya jemedari na Serikali ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia nishukuru sana Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt. Bashiru Ally kwa kusimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni Mbunge wa Jimbo la Karatu ni takribani miaka 25 Jimbo hili halijaweza kuleta Mbunge wa Chama Cha Mapinduzi. Kwa hiyo, usimamizi mzuri wa Serikali ya awamu ya tano watanzania wengi walikiamini Chama Cha Mapinduzi kwasababu, kuna muda ulifikia kwamba, watanzania walifikiri kwenda kutafuta chama mbadala nje ya Chama Cha Mapinduzi. Lakini mwaka wa 2015 Serikali ya Awamu ya Tano ilivyoingia madarakani sasa watanzania walio wengi wakaamini kwamba, Chama Cha Mapinduzi kwamba ni chama cha kimbilio ya walio wanyonge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme eneo la fidia, katika Jimbo langu la Karatu pale kuna uwanja wa ndege wa Lake Manyara, pale Serikali iliwaambia itawapa fidia takribani sasa miaka sita wananchi wale hawajaweza kupata fidia. Nilikuwa naomba Serikali katika bajeti hii ya ofisi ya Waziri Mkuu, waangalie maeneo haya. Serikali yetu wanaweza kusema tunatoa fidia lakini baadae inaweza kuchukua miaka sita wananchi wale hawaruhusiwi kufanya jambo lolote katika eneo hili la Lake Manyara.

Mheshimiwa Spika, sasa nafikiri ifikie muda kwamba, Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na nafikiri ni sikivu, waweze kuangalia maeneo haya ya fidia. Wananchi wetu wanateseka na wakati huo ukifika kwenye haya kama Mbunge, unakutana na maswali magumu kweli na unashindwa kutoa majibu kwa wakati huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikihama kutoka eneo hili la fidia niende kwenye eneo la maji pale Jimboni kwangu Karatu. Pale Jimboni kwangu Karatu Waziri Mkuu ni shahidi alitembelea lile Jimbo la Karatu, pale kuna bodi mbili za maji, kuna bodi ya KARUWASA, na kuna bodi ya KAFIWASA, wana wachaji wananchi wale wa jimbo lile kwa bei tofauti. Hawa KAFIWASA wanachaji bei ya shilingi 3,500/= kwa unit KARUWASA, wanachaji shilingi 1,700/= kwa unit. Na wakati Waziri Mkuu alitembelea jimbo lile wakati akijinadi yeye ni mgombea wa Chama Cha Mapinduzi kwa wakati huo, lakini vile vile na Rais wa Jamhuri ya Muungano tarehe 24 mwezi wa 10 alikuja jimboni Karatu na akasema hili halimshindi kurudisha bei moja ya shilingi 1,700/=.

Mheshimiwa Spika, kwasababu hawa watu wa KAFIWASA hata hawakaguliwi na Serikali wanajiendesha wenyewe, wanakusanya hela wenyewe, lakini wakati huo wakichaji/wakiwaonea wananchi kwa shilingi 3,500/=. Na hili tumelilalamikia kwa muda mrefu sana zaidi ya miaka 15 imekuwa ngumu kutekelezwa kwa Serikali, sijajua ni kwa nini? Kwamba, hawa watu wanaweza kunyonya wananchi wa Jimbo la Karatu kwa shilingi 3,500/= kwa unit halafu hakuna jambo lolote na hatua yoyote inayochukuliwa kupitia Wizara husika katika eneo hili la bei kubadilishwa, kuwa na bei moja katika Jimbo lile la Karatu kwasababu, kuna bei ya shilingi 3,500/= kwa unit na kuna bei ya shilingi 1,700/= kwa unit na inashindikana kuja bei ya shilingi 1,700/= kwa unit sijajua shida ni nini katika Wizara hii ya Maji? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wengi wameongelea suala la tembo, kwa Jimbo langu nimezungukwa na hifadhi mbili, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Lake Manyara lakini watu wanasema kwenye Wizara ng’ombe akiingia ni shilingi 100,000/= lakini…

SPIKA: Tayari Mheshimiwa

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Tupange kwenye Bunge hili tembo wakiingia kwenye eneo la wananchi ni shilingi ngapi?

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Awack.

MHE. DANIEL A. TLEMAI: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)