Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nitoe mchango wangu. Kwanza nikushukuru wewe binafsi mama wa kazi, mama mzito, software and hardware, ambaye unafanya kazi kwa akili kubwa sana, mtu anaweza kukuona simple lakini uwezo wako ni mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nimshukuru Waziri Mkuu, huyu ni mtu mwema, Waziri Mkuu wetu niliwahi kumfananisha humu Bungeni kama Rashid Kawawa (Simba wa Nyika), ukimtuma kazi anafanya. Kufanya kazi na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli miaka yote hiyo, Mungu akubariki Mzee. Maana yake lile lilikuwa burudoza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Mawaziri wote, maana nimeona hapa Mawaziri wengine wameanza kuyumba, wana hofu mara baraza litakufa au litafanyaje. Fanya kazi kwa uwezo wako mambo ya Uwaziri ni dhamana, ikitoka unakuwa Mbunge kama sisi kuna kosa gani? Kwa hiyo fanya kazi kwa uwezo wako. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nizungumzie jambo moja muhimu, tutofautishe kati ya utendaji au utekelezaji wa Ilani wa Chama cha Mapinduzi au ilani anayoitekeleza Rais aliyeko madarakani na nidhamu ya diplomasia ya utendaji wa kazi, hivi ni vitu viwili tofauti. Leo Rais wetu Mheshimiwa Samia, akisema anakwenda Marekani hatuwezi kumzuia tukasema Rais Magufuli hakwenda, hiyo ni diplomasia ya utendaji, lakini leo Rais aliyeko madarakani akishindwa kutekeleza reli, akishindwa kujenga Bwawa la Nyerere, akishindwa kujenga shule zilizoko kwenye ilani, wananchi watatuhukumu kwenye Chama cha Mapinduzi, lazima atafanya tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Rais, Mheshimiwa Samia akisema Tundu Lissu njoo, usiwe kibaraka wa Nchi za Ulaya, njoo tukupe cheo hapa. Atakuja na atafanya, hatuwezi kuuliza. Kwa sababu kuna watu wa namna hiyo, wamefanya hivi na wakapewa na wakaishi. Hiyo ni diplomasia ya utendaji, lakini utekelezaji wa ilani upo pale pale, kwa hiyo, tutofautishe hayo mambo ndugu zangu ili twende vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, linalofuata sasa hivi ni la Waziri Mkuu, naomba anisikilize. Mheshimiwa Lukuvi amwache Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize. (Kicheko/ Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere hata kama yeye anazungumza wewe unaongea na mimi huongei na Waziri Mkuu.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo linamhusu.

NAIBU SPIKA: Unaongea na mimi siyo na yeye. Hata hivyo Mawaziri wake wako hapa wanakusikiliza usiwe na wasiwasi, Mheshimiwa Waziri Mkuu ana mikono mingi, masikio mengi na macho mengi, usiwe na wasiwasi.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo linaitwa kodi ya majengo. Kodi ya majengo haina tofauti na kodi ya kichwa, leo vijijini mama bibi kizee anaenda kuorodhesha nyumba yake ya vyumba viwili na sebule anaambiwa kwa sababu ana bati alipe kodi ya majengo, hii hapana. Hatuwezi kwenda kuwalipisha watu kodi ya majengo watu wa vijijini, tunawa-encourage watu wasijenge majengo ya mabati, tunataka watu wabaki kwenye nyasi, haiwezekani. Hili naomba Mheshimiwa Waziri Mkuu alichukuwe na alitendee kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ripoti ya CAG tumeonyesha kwamba kuna trilioni 360 ambazo zinakaa pale kila mwaka kwa sababu mauzo hayapo. Ukichukua trilioni 360 ukazigawa kwa bajeti ya trilioni 32, ni miaka 11 ya bajeti ya Bunge hili, ziko pale! Naomba tuunde Tume...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa ngoja tuweke takwimu vizuri, trilioni 360?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Ndiyo, trilioni 360.

NAIBU SPIKA: Ukurasa gani huo uliosoma wa trilioni 360?

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, madeni yaliyo pending ya TRA ni trilioni 360…

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwita Getere kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Jerry Slaa.

MHE. JERRY W. SILAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ukisoma ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Serikali ni kweli kwamba TRA ina mashauri ya kesi yaliyoko kwenye Mamlaka, Bodi na Mahakama mbalimbali yenye thamani ya shilingi trilioni 360. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana. Mheshimiwa Mwita Getere endelea na mchango wako.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana mtaalam, huyu ni mtaalam namjua, ni mtaalam mwenzangu huyu. Namshukuru sana. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo ndiyo kosa la watu kutochungulia mambo. Kuna bilioni 52.5 ambazo ziko kwa DPP. Sasa hizo fedha naomba tuunde tume ya kwenda kuchunguza trilioni 360 na bilioni 52.5. Hizo bilioni 52.5 ziko kwa DPP tuzichukue ziende kutengeneza madawati ya watoto, hizo fedha zipo wazi pale, kwa hiyo tuzichukue zikatengeneze madawati ya watoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi niende pole pole. Bandari ya Bagamoyo. Tunaambiwa kwamba itakuwa bandari kubwa kuliko zote Afrika, sawa na vema; tunaambiwa kwamba meli kubwa zitatia nanga hapo kwenye hiyo bandari, sawa na vema; tunaambiwa kodi kubwa itakusanywa, sawa na vema; tunaambiwa viwanda karibu 3,000 sijui na 100 vingine, sawa vema. Swali la msingi, nini Serikali yetu inapata kutokana na hiyo bandari? Nani atafuta maelezo ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwamba bandari hiyo ni mgogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza TRA ikishakuwa pale haikanyagi pale; pili ardhi yote hiyo ya bandari inachukuliwa, hatupati chochote; tatu maili 250 magharibi, maili 250 mashariki itakwenda kwao na jamani tukisema maili wale ambao mnajuwa hesabu ni kwamba, maili 250 ni kilomita 400, kilomita 400 inaenda. Nani atafanya maelezo hayo kwa wananchi, umma kwa Tanzania ujue kwamba faida ya bandari hiyo au maelezo hayo siyo halali. Naomba hiyo mikataba ya Bandari ya Bagamoyo iletwe Bungeni ili tuthibitishe kwamba haya wanayosema ni ya kweli au siyo ya kweli…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, kengele imegonga.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)