Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Dennis Lazaro Londo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mikumi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Mikumi nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nianze mchango wangu kwa kumnukuu mwanafalsafa Frantz Fanon ambaye anasema kwamba kila kizazi kina jukumu la kihistoria. Ni jukumu la kizazi hicho kutafuta na kulifahamu jukumu lake. Aidha, ni jukumu la kizazi hicho kubeba hilo jukumu na kulitekeleza ama kulisaliti. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, Hayati Dkt. John Joseph Pombe Magufuli akisaidiana na Makamu wake ambaye sasa ni Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, wanaingia kwenye historia ya nchi yetu kama wazalendo na viongozi ambao walitambua jukumu lao la kihistoria, walilibeba na walilitekeleza. Maamuzi ambayo walichukua kuongoza Taifa letu katika vita dhidi ya wahujumu uchumi, vita za kiuchumi duniani, kurejesha imani ya wananchi kwa Serikali yao, kurudisha nidhamu ya utumishi Serikalini, ujenzi wa miundombinu ya barabara ya reli, ununuzi wa ndege, ujenzi wa vituo afya na miundombinu ya elimu, ni mambo ambayo yatawafanya waendelee kukumbukwa kwa vizazi vingi vijavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni dhahiri Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ameshaonyesha dira yake, ameonyesha azma ya Serikali yake katika kutekeleza miradi yote ya kimkakati na miradi ya kimaendeleo. Azma yake ni njema na azma hii sisi kama Bunge tunapaswa kuiunga mkono kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni jukumu la Bunge lako kuhakikisha kwamba kila mmoja ndani ya Bunge hili anatimiza jukumu lake la kihistoria katika kuhakikisha kwamba tunaenda kuisaidia Serikali chini ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kutekeleza majukumu yake, lakini pia kuhakikisha kwamba anafanya kila linalowezekana ili Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi itekelezwe. Ni jukumu la Bunge lako kuhakikisha kwamba tunaenda kutoa kila support ambayo Rais wetu anastahili ili nchi yetu itekeleze yale yote ambayo tumewaahidi wananchi katika ilani ya chama chetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu siyo kisiwa, ni sehemu ya ulimwengu mkubwa ambao unaingia sasa kwenye mapinduzi ya nne ya viwanda. Mapinduzi haya si lele mama, mapinduzi haya yanaenda kuwa katili kuliko mapinduzi yoyote ya viwanda. Tumejiandaaje kuingia katika uchumi shindani na shirikishi katika mazingira ambayo bado vijiji vyetu vingi havijafikiwa na umeme lakini pia tuna tatizo kubwa la mawasiliano? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, katika Jimbo la Mikumi katika vijiji 57 vya Jimbo langu, ni vijiji 23 tu ambavyo unaweza kupata mawasiliano ya simu ya uhakika. Maeneo makubwa ya Kata za Uleli Ng’ombe, Vidunda, Masanze, Kivungu, Kisanga na Tindiga hayana mawasiliano ya uhakika. Hata kwa upande wa umeme, ni vijiji 17 tu katika vijiji 57 ambavyo unaweza kupata umeme katika Jimbo la Mikumi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hii, tunapoenda katika uchumi shindani na shirikishi, hatuwezi tukahakikisha watu hawa wanashiriki kikamilifu katika uchumi huu wa mapinduzi ya nne ya viwanda bila kuhakikisha kwamba tunawaunganisha wananchi hawa kupitia mawasiliano na pia kuhakikisha kwamba tunawapa umeme. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, mengine ambayo…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele imegonga.

MHE. DENNIS L. LONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)