Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. George Natany Malima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. GEORGE N. MALIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami nichangie hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu.

Kwanza kabisa, kabla sijachangia naomba kutoa pole kwa Watanzania wote kwa ajili ya msiba mkubwa ambao ulitupata tarehe 17 wa Mheshimiwa wetu Rais, Marehemu Dkt. John Pombe Magufuli. Pia nitoe pole kwa Rais wetu wa sasa, Mheshimiwa Mama Samia Hassan Suluhu kwa ajili ya msiba huo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichangie na nitaanza na kuzungumzia ukurasa wa 67 wa Hotuba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Katika ukurasa huo wa 67,

Mheshimiwa Waziri Mkuu ameeleza nia ya Serikali ya kuanza Awamu ya Pili ya ujenzi wa Mji wa Kiserikali wa Mtumba. Jambo hilo limenipa faraja sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Dodoma ndiyo Makao Makuu ya nchi yetu na wafanyakazi wengi wamehama kutoka Dar es Salaam kuja hapa Dodoma. Kwa hiyo, ni muhimu sana kuwe na makazi ya kutosha ili wafanyakazi hawa wafanye kazi bila kuwa na shida ya upangaji wa nyumba na usumbufu wa aina yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, ipo miradi ambayo Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakisaidiana na mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu ambaye ni Rais wetu wa sasa, walikuwa wameipanga. Naiomba sana Serikali izingatie sana jambo hilo. Kwanza, kuna Mradi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato. Uwanja huu ni muhimu sana kwa Serikali yetu; kwa uchumi wetu na kwa sababu Dodoma ni Makao Makuu tutakuwa na wageni wengi ambao watatoka nje ya nchi watakuja na ndege kubwa ambazo zitahitaji kutua katika Mji wetu wa Dodoma. Vile vile kutakuwa na mwingiliano wa watu wengi, kwa hiyo, tutaweza kufanya biashara kupitia kiwanja hiki cha ndege.

Mheshimiwa Naibu Spika, uwanja huu wa ndege utakuza uchumi wa Jiji la Dodoma kwa sababu watu watafanya biashara mbalimbali. Walioko pembezoni mwa uwanja watafanya biashara kwa sababu kutakuwa na wageni wengi ambao watakuwa wanatua katika uwanja ule na kuondoka. Kwa hiyo, ni muhimu sana tukazingatia kwamba Mji Mkuu wa nchi yetu uwe na uwanja mkubwa wa ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo linguine ni kwamba kuna mpango ule wa kujenga barabara ya kuzunguka Mji wa Dodoma (ring road). Barabara hii ni muhimu sana. Bado ina umuhimu mkubwa, nami nafarijika kwa sababu Serikali yetu imejipanga kutekeleza. Faida kubwa ambayo tutaipata kwenye barabara hii, itasaidia kupunguza msongamano wa magari katika Jiji letu la Dodoma. Magari yale makubwa yenye mzigo, yakitoka Dar es Salaam na maeneo mengine, yakiona hayana haja ya kuingia mjini, yatazunguka kupitia hiyo barabara kuelekea Mwanza, Iringa au Arusha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, barabara hiyo itatusaidia magari kama malori na wale wa usafiri wa kawaida ambao hawana nia ya kuingia mjini, waweze kwenda haraka na kuzunguka. Hiyo italeta mandhari nzuri sana ya Mji Mkuu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji Mkuu hauwezi kukamilika kama hakuna maji ya kutosha. Mji huu watu wameongezeka sana, kwa hiyo, kile kiasi cha maji kilichokuwa kinatosheleza miaka ya nyuma sasa hivi hakitoshi. Tunahitaji kuwa na mkakati wa kuwa na maji ya kutosha katika Jiji la Dodoma. Mpango wa kuvuta maji kutoka Ziwa Victoria, naomba sana Serikali izingatie; pia kuna Mpango wa kujenga Bwawa la Farkwa ambalo ni jirani sana hapa Chemba, hilo pia litasaidia kuongeza kiwango cha maji katika Jiji letu la Dodoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana Serikali izingatie sana hayo. Ili Mji wetu uweze kuonekana kwamba ni Mji Mkuu unahitaji kuwa na mambo hayo muhimu sana. Lazima wageni wetu wakifika wasikutane na shida ya maji. Kwa kweli maji ndiyo sura ya Jiji lolote katika Dunia. Kama hakuna maji, hata wageni wetu watatushangaa, tumeletaje Mji Mkuu Dodoma hakuna maji? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima tuhakikishe kwamba tunatoa kipaumbele maji yaletwe Dodoma na yawe ya kutosha, yaendane na idadi ya watu wanaohamia katika Mji wa Dodoma. Baada ya miaka mitano kutakuwa na watu wengi zaidi. Kwa hiyo, suala la maji ni muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuzungumzia Mji Mkuu wa nchi yetu, naomba kidogo sasa nizungumze katika eneo la kilimo hususan katika eneo la mbegu. Wakulima wetu wengi bado wanalima kilimo cha zamani, cha mazoea. Wanatumia mbegu za zamani ambazo hazina tija. Hii inatokana na ukweli kwamba, pamoja na nia njema na bidii ya Serikali kuendelea kufanya utafiti juu ya mbegu bora zenye tija lakini bado kiwango cha mbegu hakitoshelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu kiwango hakitoshelezi, shida imekuwepo kwamba mbegu inayopatikana ni kidogo, kwa hiyo, bei inakuwa kubwa. Tuki- apply ile law of demand; supply ikiwa ndogo, demand kubwa automatically bei itakwenda juu. Mwaka huu wakulima wetu wamenunua mbegu ya mahindi, nami nimenunua pia. Nilikuwa nanunua kilo mbili kwa shilingi 15,000/= just imagine, kijijini nani anaweza kununua mbegu kilo mbili kwa shilingi 15,000/=? Kwa hiyo, unaweza kuona ni kwa kiasi gani bado tunahitaji mbegu bora za kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwezi Januari kule kwetu Mpwapwa tulitembelea kiwanda kimoja kimoja kiko kule Morogoro, kinaitwa Mahashree Agro-Processing Tanzania Limited. Kiwanda hiki ni cha watu kutoka India, wanakamua mafuta ya mbegu mbalimbali na tulikwenda baada ya wao kuja Mpwapwa kutafuta Soko la Karanga. Sasa kabla hatujawaunganisha na wakulima wetu tuliona ni vizuri sana tujiridhishe tuone kiwanda hiki kina-capacity ya kiasi gani kununua karanga kwetu. Kwa hiyo, tulienda mimi, Mkuu wa Wilaya na Watendaji wa Halmashauri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulipofika kwenye kile kiwanda tulikuta kweli wana capacity kubwa sana ya kununua mbegu mbalimbali pamoja na karanga. Alichotuambia yule mwenye kiwanda ni kwamba, shida iliyoko katika maeneo yetu ya Mpwapwa na Kongwa, zile mbegu siyo bora, hazitoi mafuta ya kutosha. Kwa hiyo, alikuwa ana-suggest kwamba ni vizuri sana tukapata mbegu ambazo zitakuwa bora, zitakuwa na tija kwa wakulima wetu na zitatoa mafuta ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, suala la mbegu ni muhimu sana na tunaiomba sana Serikali yetu izingatie, pamoja na mambo mengine, ili kilimo hiki kiweze kuwasaidia wakulima, lazima tuwe na mbegu bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mwisho ni kwamba katika maeneo yote yenye kilimo kama ya kwetu huko kwenye karanga na kadhalika, haitasaidia hata tukipata mbegu bora kama barabara zile zinazotoka kwenye maeneo ya kilimo hazitatengenezwa. Hilo ni jukumu ambalo nataka niwa-assign TARURA. Ni muhimu sana watu wetu wakipata karanga au mazao ya kutosha kama alizeti na kadhalika, ni muhimu sana kukawa na njia za kuyaleta kwenye masoko. Wakati mwingine yameharibikia shambani kwa sababu hakuna namna ya kuyaleta kwenye masoko. Kwa hiyo, suala la barabara Serikali naomba iendelee kulitilia mkazo na hasa barabara za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)