Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amour Khamis Mbarouk

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, Bismillah Rahman Rahimu, nakushukuru sana kwa fursa hii na kwasababu leo ni siku ya kwanza kabisa kusimama katika Bunge lako hili na Mwenyezi Mungu amejaalia kwamba ni siku ya mwanzo katika siku za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, basi nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu Sub-hanallah wa taala kwa kutuwezesha sisi wote huku kuwa Wabunge na kuhudhuria kwenye nyumba hii. Pili Chama changu Chama Cha Mapinduzi CCM lakini hasa hasa viongozi wake Mahsusi Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli kwakuwa yeye alikiongoza Chama Cha Mapinduzi hadi leo nipo hapa kwenye Bunge hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Mheshimiwa Mama Samia kama msaidizi wake naamini walishauriana sana katika kupitisha majina yetu, kwa hiyo, nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia Mwenyezi Mungu ampe maisha marefu yenye manufaa ya duniani na akhera.

WABUNGE FULANI: Amin!

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nisiwasahau Katibu Mkuu na Katibu wa Itikadi na Uenezi hawa ndio walitumwa kabisa kabla ya kampeni za uchaguzi walitumwa na Hayati Dkt. Magufuli kuja kupeleka ujumbe na ku-test mitambo pale Pemba kwa hiyo, tuwashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia niwashukuru Spika na Naibu Spika kwa namna mnavyotuongoza kiasi ambacho leo najisikia kusimama hapa na kusema chochote yote hii ni kwasababu ya uongozi wenu. Katika hotuba hii ya Waziri Mkuu ambayo ni ya bajeti ya Wizara yake, naomba nichangie mambo machache sana..

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie jambo la kwanza ni Kilimo, kwa fikra yangu ili kilimo kiendelee ndani ya Tanzania, lazima tuwekeze fedha nyingi sana, na ili fedha hizi zipatikane lazima benki waondoshe riba kwa wakulima. Kwa sababu mkulima anapolima kule shambani alafu ukaja ukamkata riba, na shambani mazao yake akiyaondoa au akiyapeleka sokoni lazima pia kodi atoe kwa hiyo, tunakuwa tunamkata juu na chini kiasi ambacho tunamfanya mkulima akate tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana hii riba kutoka kwenye Benki iondolewe, na hili pia Mheshimiwa Hayati Dkt. Magufuli alilisema katika hotuba yake hii ni kuonesha kwamba riba kidogo inarudisha nyuma maendeleo. Katika kilimo hiki hiki kuna tafiti, watu wengi wamezungumzia kuhusu tafiti. Nilikuwa naomba kama kuna tafiti zozote basi zipelekwe kule vyuo vikuu wanafunzi waliopo pale watusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Halafu fedha ambazo zimepangwa kwenye Mawizara kwa ajili ya tafiti wapewe wanafunzi wetu wa vyuo vikuu kule ziwasaidie, sasa itakuwa sisi vyuo vikuu vinamanufaa gani kwetu ikiwa hadi sasa hatujaweza kusimamia tafiti zetu wenyewe kwa kupunguza gharama. Naomba sana hizi tafiti zipelekwe vyuo vikuu tunavyo vingi na fani tofauti kozi tofauti zinasomwa, naamini vijana wanaweza kufanya kazi hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili katika hotuba ya Waziri Mkuu nilikuwa naombi sana na ombi hili ni kuhusiana na sina hakika nitakachosema nipo kwenye sheria au vinginevyo. Lakini sisi tuna mifuko ile ya Jimbo na ile mifuko kwa upande wetu kule Pemba au Zanzibar inapatikana kidogo sana, na hapa kuna ahadi ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ya kumsaidia Rais wa Zanzibar.

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonaje Serikali kwamba itaongezea katika kusaidia hili kumsaidia Rais wa Zanzibar kama hii mifuko itaongezwa kiwango pengine kutoka Milioni 20 zilizopo sasa hivi au pengine Milioni 50 kwa majimbo mengine bila kujali formula kwamba Jimbo lina watu wengi wapewe kiwango kikubwa basi sisi tuongezewe zile fedha angalau ifike Milioni 100 kwa Jimbo pale Zanzibar na iwe specially kwa Zanzibar. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, hizo hupati mzee.

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine katika hili angalau bajeti tunazozizungumza hapa katika kumsaidia Rais wa Zanzibar pale angalau asilimia 10 kila Wizara ingekuwa inafikiriwa kupelekwa pale Zanzibar, Zanzibar leo ingekuwa Ulaya na watu wengi wangeipenda sana.

MBUNGE FULANI: Hamjashauriana kwa kweli!

MHE. AMOUR KHAMIS MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuchangia mambo haya naunga mkono hoja.