Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Mohamed Lujuo Monni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chemba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nichangie hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuanza kuchangia naomba niseme maneno machache. Kwanza kabisa nichukue fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema, ambaye amekuwa akitupa uhai na afya njema ya kuendelea kuwatumikia Watanzania. Pili, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais ameanza vizuri na tuna uhakika wa asilimia zote yale ambayo tumeahidi kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi yatatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda naomba mimi nianze kuchangia. Kwanza kabisa nataka nimpongeze sana Waziri Mkuu kwa hotuba yake nzuri. Hotuba hii imegusa kila eneo, lakini kwangu imekuwa nzuri zaidi kwasababu ameeleza namna gani tunaenda kujenga lile Bwawa la Farkwa. Mradi huu wa Bwawa la Farkwa ndio mradi peke yake ambao unaenda kumaliza matatizo yote ya maji kwenye Jiji letu la Dodoma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na bahati nzuri mradi huu ukitekelezwa hautamaliza tu changamoto za maji kwenye Jiji la Dodoma, utamaliza pia kwenye wilaya zetu zote za Mkoa wa Dodoma. Bahati nzuri sana Waziri Mkuu mwenyewe ametembelea kwenye huu mradi na yapo maelekezo ambayo aliyatoa, lakini bahati mbaya sana kuna changamoto kwenye maelekezo mengi ambayo ameyatoa hayajatekelezwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja ya changamoto hizo ni kwamba, tayari Serikali ilitoa 1.8 billion kwa ajili ya kulipa fidia ya watu wote waliokuwa kwenye maeneo yale na fidia hiyo tayari imelipwa. Wametengewa maeneo ambayo wanatakiwa waende kuishi, lakini bahati mbaya sana tumechukua shule zao, lakini kule hatujaenda kujenga shule. Wamelipwa fidia tunawaondoa, lakini wanaenda sehemu ambapo hakuna shule ya msingi, hakuna zahanati, wametengewa eneo waende, lakini miundombinu ile ya kuwafanya waishi haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Waziri Mkuu alipofika aliwaambia msiwaondoe hawa, jengeni kwanza shule, jengeni zahanati na akaelekeza fedha zitolewe, lakini mpaka leo hii bado ni changamoto kubwa sana. tunaendelea kuwaondoa watu wahame, lakini tunawapeleka sehemu ambako watoto wao watakaa bila kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, ushauri wangu kwa Serikali, tuna mipango mizuri na sisi watu wa Chemba pamoja na Dodoma kwa ujumla tuna uhitaji kweli huo mradi. Na huo mradi ndio peke yake ambao unaenda kuondoa changamoto yote ya maji kwenye maeneo yote yanayozunguka. Lakini bahati nzuri ukisoma andiko la mradi ule limeeleza namna gani kwenye maeneo yale watatengeneza skimu za umwagiliaji kwa hiyo, kwa namna yoyote ile mradi ule una faida kwetu zaidi. Changamoto ni moja tu ni hiyo ambayo nimeieleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Wizara ya Maji itoe fedha kama tulivyokubaliana kwa ajili ya ujenzi wa shule na zahanati, ili watu wale wahamie kule. Tukiendelea kwasababu, sasa hivi kuna kama kigugumizi cha watu kuondoka, watu wengine wamehamia, lakini watu wengine bado wapo. Na nikifika kule naulizwa Mheshimiwa Mbunge wanatuambia tuje hapa, watoto wetu watasoma wapi?

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kuhusu maji ni huu, lakini pia naishukuru Serikali, tuna mradi pia katika ile miradi ya miji 28 Halmashauri yetu ya Chemba ni moja ambayo inanufaika na bilioni 11 zile. Na bahati nzuri watu wale wanaotekeleza ule mradi tumefika tukafanyanao vikao tukawaomba watu wale waliokuwa wanadai fidia za watu kupisha mabomba ya maji wamekubali wanaondoka na hawahitaji fidia. Niiombe sasa Serikali ifanye haraka kwa ajili ya kutekeleza ule mradi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia niongee kidogo kuhusu kilimo. Sisi sote tuliopo hapa tunafahamu asilimia 77 ya ajira za Watanzania zinapatikana kwenye kilimo, lakini si hivyo tu, tunafahamu asilimia 90 ya ardhi iliyopo Tanzania hii inalimwa na wakulima wadogowadogo. Sasa ni mawazo ya kawaida tungefikiria kwamba, huku ambako watu waliko wengi ndiko tuingize fedha nyingi kwa ajili ya matokeo makubwa, lakini ukweli ni kwamba, bajeti ya Wizara ya kilimo ni ndogo sana na hii ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe sana kuwa tuangalie namna sehemu ambako tunatakiwa kuwekeza ni sehemu ambako idadi ya wanaochangia uchumi ni kubwa. Idadi ambayo ya waliojiajiri ni kubwa, ili tuweze kutatua changamoto na kwasababu hiyo, tunaweza tukaongeza pato la Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hivyo kuna changamoto kubwa sana kwa wakulima wangu. Moja ya changamoto kubwa ni kile kitu kinachoitwa stakabadhi ghalani. Serikali ina dhamira njema kwelikweli, lakini changamoto iliyopo unawalazimisha watu mpaka kwa bunduki ili wakauze huko kwenye stakabadhi ghalani, sijui ni nini? Unalima mwenyewe, unavuna mwenywe, unapalilia mwenyewe, Serikali hujapeleka hata mbegu, unashika bunduki ili mtu akauze kwenye stakabadhi ghalani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linaleta kero kubwa sana, kule kwangu sasahivi wameanza kuvuna. Nilikuwa na mkutano weekend hii wameanza kuniuliza tumeambiwa tena tuanze kupeleka mazao kule; hivi kweli kama hiyo stakabadhi ghalani ina faida kwa wananchi kwa nini wao wasihamasike kwenda kuuza huko? Unamlazimisha mtu mwenye debe moja aende akasubiri mwezi mzima ndio aje alipwe fedha yake? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nafikiri hili haliwezi kuwa sawa, nashauri Serikali kwa baadhi ya maeneo au kwa baadhi ya mazao waachane na huu utaratibu kwa sababu kwa namna yoyote ile ungekuwa na faida wakulima wenyewe wasingeukataa.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongee kidogo kuhusu barabara, kuna barabara yetu ambayo na Mheshimiwa Rais, Hayati, alivyofika kwenye Jimbo langu la Chemba aliahidi. Barabara inatoka Kibarashi inaunganisha mikoa minne, Kibarashi – Kiteto – Chemba hadi Singida. Barabara hii kwenye Ilani imekuwa ikiandikwa mara zote, lakini hakuna hata mwaka mmoja ambao imetengewa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwasababu ya hayo naomba kuwakilisha. Naunga mkono hoja. (Makofi)