Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru sana kuniruhusu kuchangia hotuba hii ya Waziri Mkuu yenye mambo ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumpenda sana Marehemu Rais, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli na kumchukua. Mungu aiweke roho ya Marehemu Magufuli mahali pema peponi.

WABUNGE FULANI: Amen.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, leo ni siku ya 29 tangu ametutoka na kumpoteza mpendwa wetu huyu. Kwa hiyo, msiba huu kwetu sisi bado ni mbichi. Kwa mila zetu za Kitanzania ni mwiko au taboo kumwongelea Marehemu kwa mabaya, bali kumwombea ili Mungu ampokee na aiweke roho yake mahali pema Peponi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nami niendelee kukemea wale watu wenye hulka ya kubadilika kama kinyonga, waache kumsema kwa mabaya Marehemu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, bali waendelee kumwombea na waone aibu na wamwogope Mungu. Kwangu mimi, Marehemu Rais Mheshimiwa Dkt. Magufuli anaishi bado kwa alama kubwa alizotuwekea ambayo ni pamoja na reli, vituo vya afya, bwawa la umeme, hospitali, barabara, ndege, kuhamia Dodoma, madaraja, vituo vya VETA, elimu bure na miradi mengine mingi kama maji na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, alama hizi zote sasa ziko mikononi kwa Mama shupavu, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tunamwomba Mungu ampe nguvu mama huyu, achukue jahazi hili na kulibeba kama ambavyo walilibeba wakiwa na Marehemu Mheshimiwa Dkt. Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hotuba ya Waziri Mkuu, ametaja mambo mengi, lakini mimi nijikite kwenye sekta binafsi ambayo ina sheria za kazi. Sheria hizi zilizopo katika matumizi kwa sasa zimepitwa na wakati. Kwa mfano, Baraza la Usuluhishi la RESCO halijakutana kwa muda mrefu sana na hili ndiyo lingekuwa nafasi ya kujadili matatizo ya waajiri na wafanyakazi. Tungependa Ofisi ya Waziri Mkuu inayohusika na sera na kazi na ajira iziboreshe sheria hizi. Kwa mfano, sasa hivi tulipata tatizo kubwa sana tulipozuiwa mambo ya Covid; waajiri walipata taabu sana kuendelea kulipa mishahara kama tungelifunga hata pale ambapo wafanyakazi hawafanyi kazi. Sheria za sasa zingeweza kuchukua nafasi hiyo na kulisahihisha tatizo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lipo suala la umeme wa REA ambapo vijiji vyote vya Tanzania vitakuwa na umeme ifikapo mwaka 2022/2025 lakini pia umeme huo utakuwa na matumizi makubwa, kwa hiyo, kuna umuhimu wa kulipa nguvu wazo au mradi ule wa Bwawa la Nyerere likamilike ili kuleta umeme katika maeneo ambayo yatapatiwa umeme wa REA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la reli ya SGR ukurasa wa 50, kuna mtu amesema mradi huo utakamilika mwaka 2102, yaani miaka 81 kuanzia leo. Nimemshangaa sana kwa sababu, kanuni za miradi ni kuwa na tarehe ya kuanza na tarehe ya kumalizia. Kwa hiyo, miradi yote ya reli hii ya SGR inajengwa kwa awamu na vipande kutoka Dar es Salaam – Morogoro na Morogoro - Dodoma na baadaye Mwanza - Isaka na miradi hii yote ina tarehe ya kuanza na kwisha…

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, haitafika muda mrefu huo.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Maige, kuna kanuni inavunjwa. Mheshimiwa Halima Mdee.

KUHUSU UTARATIBU

MHE. HALIMA J. MDEE: Mheshimiwa Naibu Spika, Kanuni ya 67(8), Mbunge hatasoma maelezo isipokuwa kwa madhumuni ya kutilia nguvu maelezo yake, anaweza kusoma dondoo kutoka kwenye kumbukumbu zilizoandikwa au kuchapishwa na anaweza pia kujikumbusha kwa kuangalia kwenye kumbukumbu alizoziandika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa mkongwe mwenzangu nimekuwa namvumilia, naona anasoma tu, sasa naomba umshauri mkongwe a-note tu, halafu atiririke. Kwa hiyo, naona hii Kanuni inavunjwa. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Almas Maige nadhani ulikuwa unakumbushwa. Unajua pale hasomi maelezo anayosema, isipokuwa ameamua kuinamia kwenye mic yake. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Maige, hicho kisemeo hata ukitazama pembeni kinashika mawimbi, kwa hiyo, usiwe na wasiwasi. Karibu umalizie mchango wako. (Makofi/Kicheko)

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Mkongwe mwenzangu nakushukuru sana, lakini sikuwa nasoma, maana nilikuwa nimefanya notification, lakini mambo niliyoyaongea kabla ya kuanza kuongea haya, nilifikiri kwamba ningepotea. Nimeongea mambo mazito ndiyo maana ikanilazimu niwe na kumbukumbu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, afya. Jimbo la Tabora Kaskazini lina Kata 19 na Kituo kimoja tu cha Afya. Mimi nafikiri kwamba ipo haja ya Serikali kufikiria Jimbo la Tabora Kaskazini ambalo lina Kituo cha Afya kimoja tu, liweze kupata vituo vingine na hasa kusaidia vituo ambavyo vimejengwa kwa nguvu ya wananchi katika Kata ya Mabama, Kata ya Usagari na Kata ya Shitaghe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)