Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Vita Rashid Kawawa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Namtumbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. VITA R. KAWAWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru nami kwa kunipa fursa hii ili niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu. Nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kuwasilisha vyema hotuba yake iliyo-cover na kusheheni maeneo yote kwa ujumla na ufasaha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa majukumu ya Kikatiba ya Ofisi ya Waziri Mkuu ni kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali, lakini pia kusimamia shughuli za Serikali Bungeni. Kazi hiyo imefanyika vizuri sana katika kipindi kilichopita; wameisimamia Serikali katika miradi ya kimkakati vizuri na mafanikio ya miradi yote tunayoiona ni kwa sababu ya kazi nzuri iliyofanywa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri iliyokuwa inafanyika Bungeni humu ni kazi ambayo imefanywa chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu chini ya Waziri Mheshimiwa Dada Jenista Mhagama. Kwa hiyo, nawapongeza sana kwa kazi nzuri walioifanya. Kubwa ni ile kazi iliyotukuka na ikatufanya tukakaa kwa amani kabisa wakati wa kipindi cha msiba kwa aliyekuwa Rais wetu. Walifanya kazi ya uratibu mzuri wa maziko ya Rais wetu aliyetutoka na tukafanya kazi ile ya maziko kwa mafanikio makubwa sana na dunia imetupa heshima kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze katika kutoa ushauri wangu. Kazi kubwa ya miradi ya kimkakati imefanyika, sasa naiomba Serikali ijielekeze sana sasa hivi katika kuweka mazingira bora ya uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu inayojengwa au iliyokamilika. Kwa mfano, sekta mtambuka ziangalie ni jinsi gani zitaweza kutumia fursa ya SGR ambayo inajengwa, inaenda kukamilika sasa hivi.

Je, kwa mfano Wizara ya Ardhi na Wizara ya Viwanda na Biashara zimepitia na kutambua ardhi na kuweka mkakati wa viwanda katika maeneo ambayo itapita SGR ili tuweze kuvutia wawekezaji kwenda kuwekeza katika maeneo hayo tuweze kuitumia SGR effectively? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili pia Wizara ya Kilimo inaweka mpango gani kushawishi wawekezaji au wakulima wakubwa wakatambue maeneo inakopita SGR wakaweka kilimo kikubwa pale ili tuweze kutumia reli ile ya kati? Pia Wizara ya Maliasili nayo ina mpango gani wa kushawishi kuweka mashamba makubwa ya miti katika maeneo inapopita SGR? Hapa nina maana fedha nyingi zimewekezwa katika ujenzi wa reli hii, lakini inapopita reli kwa eneo kubwa ni kwenye mapori ambayo yalikuwa hayatumiki. Sasa ni fursa kwa sisi kama Serikali kushawishi sekta binafsi kuwekeza katika maeneo hayo ya kilimo, ya viwanda vitakavyo support kilimo, lakini pia kuwekeza katika mazao ya misitu ya mbao ambayo yana soko kubwa katika nchi zetu zinazotuzunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijielekeze jimboni. Naishukuru sana Serikali Waziri Mkuu ameeleza mafanikio yaliyofanyika katika kipindi hiki cha nyuma. Sisi wa Namtumbo tunawashukuru sana, Serikali imewekeza karibu billioi 27 katika usambazaji wa umeme, katika kuunganisha umeme wa grid katika Wilaya yetu na maeneo makubwa katika vijiji vyetu vimewekwa umeme na vingine vilivyobakia changamoto iliyopo ni katika vitongoji, lakini baadhi ya maeneo katika kuunganishwa umeme. Kwa hiyo tunaomba sana katika eneo hili mafanikio makubwa tumefanikiwa. Katika Sekta ya Afya Serikali ilituingizia bilioni moja na milioni mia nane na imetujengea hospitali ya wilaya. Haya ni mafanikio makubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mafanikio mengine, Serikali imetujengea Chuo cha Elimu cha VETA kilichogharimu bilioni sita na milioni mia tano na chuo sasa kinatumika. Tunachoiomba Serikali sasa iwekeze kwenye rasilimali watu katika maeneo haya ya elimu na afya ili waweze kuja kwa kutosha waweze kutoa huduma iliyokusudiwa kwa sababu tumeweka fedha nyingi katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia katika maeneo ya kilimo sisi ni wakulima wakubwa sana wa mazao ya mahindi na tunategemea sana pembejeo, lakini katika wakati pembejeo za kilimo zinasambazwa bei inabadilika kila siku. Tunaomba Serikali kwa kuwa kwenye mpango Serikali imesema kutakuwa na tathminini ya ufuatiliaji wa miradi, lakini pia ifanyike tathmini ya masoko ya pembejeo. Tuangalie pia masoko ya mazao yetu mchanganyiko, tunaiomba sana Serikali ifungue masoko haya ya mazao mchanganyiko. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia barabara; katika Ilani yetu ya Chama Cha Mapinduzi ambao tulikabidhiwa na sisi ndio tulienda kuinadi katika uchaguzi, tuna barabara mbili kubwa za lami ambazo tunatakiwa tujengewe kutoka Mtwara Pachani kwenda mpaka Tunduru na kutoka Lumecha kwenda Kitanda hadi Malinyi Ifakara. Tunaomba sana Serikali katika mpango wake wa bajeti iziweke barabara hizo mbili katika utekelezaji kama ilani yetu inavyoelekeza. Tumeinadi ilani hiyo, tumeisema kwa wananchi kwa msingi mkubwa kwetu Wilaya ya Namtumbo Wizara ikianza kututekelezea ujenzi wa barabara hizi mbili; kwanza, barabara ya kutoka Lumecha kwenda mpaka Ifakara kupitia Malinyi inapunguza kilomita 350 kwa barabara tunayopita sasa hivi. Kwa hiyo tunaomba sana Serikali itutekelezee ujenzi wa barabara hizi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja. (Makofi)