Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Amb. Dr. Pindi Hazara Chana

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii. Nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri Mkuu Ofisi yake imefanya kazi kubwa nzuri kwenye utekelezaji wa hii Ilani kipindi kilichopita tumeona na sisi Watanzania tunamatarajio makubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nikimpongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu bila kumpongeza Mheshimiwa Rais, Mama yetu mpendwa Mama Samia nitakuwa sijakamilisha itifaki. Nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Mama Shupavu, Mchapakazi, Hodari na Watanzania tupo nyuma yako Mheshimiwa. Vilevile nitambue maendeleo makubwa ambayo yalifanyika na Baba yetu Mpendwa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kwa kazi kubwa ambayo ilikuwa imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja naomba niende katika suala zima la asilimia kumi za halmashauri. Katika halmashauri zetu tumekubaliana kwamba tutatenga asilimia kumi kwa ajili ya vijana, wanawake na walemavu. Kwa haraka haraka zipo halmashauri ambazo mapato yake kwa mwaka yanafika bilioni tano; kwa lugha nyepesi ina maana kwa mwaka wanatakiwa watenge milioni 500. Na wakitenga ndani ya miaka mitano unapata all most 2.5 bilioni za kukopesha vijana, wanawake na wenye ulemavu. Kuna Halmashauri mapato yake tuchukulie ni bilioni mbili. Maana yake kwa haraka haraka ni kiwango kisichopungua milioni 200 kwa mwaka.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zinarejeshwa bila riba, lakini hatujasema zile pesa zinazorejeshwa kila mwaka utaratibu wake unakuwaje. Je, zinachanganywa na zile ambazo zinabajetiwa mwaka husika? Na kama kila halmashauri inaweza ikatenga milioni 500 kila mwaka ukachanganya na zile zinazorejeshwa kutoka mwaka uliopita maana yake mfuko huu ni mkubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tunapozungumzia uchumi wa kati, uchumi shindani hili ndilo eneo ambalo hata changamoto ya ajira kwa vijana kwa wanawake na walemavu tunaweza tukapata majibu ya kutosha. Kwa hiyo mfuko huu tuungalie vizuri sana; yale marejesho yanapoingia kwenye akaunti what next? Kila Halmashauri baada ya kutoa kwa vikundi wamerudisha, sasa sheria lazima itafsiri, pale ambapo pesa zimerudishwa zinachanganywa na za mwaka huu au utaratibu wake unakuwaje…

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa

SPIKA: Ndiyo taarifa.

T A A R I F A

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba…

SPIKA: Aah sawa, Mheshimiwa ni Viti Maalum Tanga Engineer

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haya.

MHE. ENG. MWANAISHA N. ULENGE: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa mzungumzaji kwamba kwa mujibu wa ile sheria iliyoruhusu kutumika asilimia kumi imeweka wazi kwamba ile pesa ni Revolving Fund and The Rollover Fund. Kwamba hata mwaka ukipituka (ukiisha) ile hela itaendelea kuwepo pale na hata marejesho ni sehemu ya mkopo unaokuja. Imeweka wazi kwamba lazima kila Halmashauri ifungue akaunti ambayo pesa zile zitawekwa zote za kwa pamoja na kila zinavyoji-accumulate inakuwa next amount ya kuweza kuwakopesha wengine. Kwa hiyo wasiokuwa wanafanya hivyo hawana akaunti na wala marejesho si sehemu ya mkopo unaokuja wanafanya makusudi kwa sababu zao, lakini ile sheria ipo wazi imeelezwa vizuri sana. Ahsante.

SPIKA: Ahsante sana. Mheshimiwa Balozi Dkt. Pindi Chana unapokea taarifa hiyo?

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: Mheshimiwa Spika, pamoja na taarifa hiyo naendelea kuchangia kama ifuatavyo; na imani dakika zangu zitalindwa.

Mheshimiwa Spika, kwamba fedha hizi zitakuwa ni mkombozi sana kwa makundi haya na ni muhimu sana tukaziwekea utaratibu mzuri. Kwa tafsiri hiyo basi, maana yake halmashauri zetu zinapaswa kuwa na pesa ya kutosha sana. Hatuhitaji vijana waende benki kutafuta mikopo ya asilimia 16 au 20 kumbe kuna fedha hizi ambazo zinatengwa kila mwaka na zinatumika kukopesha pasipo riba. Hatutakiwi kuwa kilio cha kusema kwamba vijana hawana ajira, ni suala zima la Madiwani kuzisimamia hizi fedha vizuri na kuona ni namna gani tunaweza tukasaidia vijana na makundi mengine. (Makofi).

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala zima la bima ya afya iliyoboreshwa. Bima ya afya iliyoboreshwa kila kaya ni elfu thelathi na wanatibiwa watu sita hii ni mkombozi mkubwa sana. Maana yake ni kwamba kila mtu ni Shilingi elfu tano kwa mwaka, hii haijapata kutokea. Hizi ni pongezi kubwa sana kwa Serikali yetu ambayo inawalinda wananchi. Changamoto iliyopo hapa mara kwa mara tunapokwenda katika hospitali kufuatia bima iliyoboreshwa kuna shida ya dawa. Eneo hili la dawa lazima tuliangalie tunafanyaje?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo mara nyingi wananchi tunapozidi kuhamasisha na nimekuwa nikihamasisha mara kwa mara bima ya afya iliyoboreshwa wanapoenda katika vituo vya afya changamoto imekuwa ni dawa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo wakati umefika sasa wa kulifafanua jambo hili vizuri kwamba bima ya afya iliyoboreshwa ndani yake kuna component gani na zipi hazipo ili mwananchi anapokata bima ajue kwamba matibabu yangu yatakuwa ni haya na haya hayahusiki na bima ya afya; vinginevyo tafsiri yake inakuwa ni tofauti, wakiamini kwamba watapa huduma zote nzuri kwa wakati. Na wanapoenda wananchi wetu, na sasa hivi idadi ya watu ni milioni 60 wakakosa hii huduma hususan dawa katika vijiji vyetu, katika wilaya zetu kwa kweli eneo hili lazima tuwe na majibu. Na tunatakiwa tuwe transparent ni namna gani tunaweza kuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni suala la mahindi, na wananchi wamenituma wa Mkoa wa Njombe na mikoa mingi ya kusini na Iringa. Mahindi wanasema wanalima vizuri sana, wanaweka mbolea, mbegu changamoto ni masoko. Sasa hivi tuna mahindi mengi na tutashukuru sana tukipata delegation ya NFRA hata kesho waende wakanunue mahindi kwa wakulima. Wananchi wetu asilimia sitini wamejikita kwenye kilimo, sasa wanapopata mazao lakini wakakosa masoko kwa kweli inakuwa changamoto kubwa ilhali wamegharamia mbolea. Mahindi hivi sasa mahindi haya yasiponunuliwa maana yake mavuno ya mwaka uliopita yanakutana na mavuno ya sasa kuanzia mwezi ujao mikoa hii ya kusini hadi kufikia mwezi wa sita tunaanza kuvuna mahindi. Kwa hiyo taasisi husika, Wizara husika mahindi yakanunuliwe mapema sana kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na maeneo ya kuuza mahindi yapo mengi wahusika wanajua tunakambi za wakimbizi, mashirika ya kimataifa na tuna nchi jirani wanahitaji sana chakula. Kwa hiyo suala la masoko ya mahindi isiwe changamoto. Wananchi hawa haya mahindi yanasaidia kusomesha Watoto, matibabu na kuendelea kulima.

Mheshimiwa Spika, eneo lingine ni lumbesa, suala hili bado limekuwa ni changamoto. Kwa hiyo tuone namna kama tutaweza kuuza bidhaa zetu kwa vifungashio maalum au kwa kutumia vipimo maalum. Endapo mtu anajaza gunia basi tuseme labda viazi au maharage debe moja ni kiasi kadhaa, kilo mia ni kiasi kadhaa. Lumbesa imekuwa ni changamoto na wakati mwingine katika magunia wakiweka zipu bila lumbesa baadhi ya maeneo wanavyoenda kushusha sasa kama soko la Kariakoo wanasema pasipo lumbesa basi bei inashuka chini. Kwa hiyo eneo hili pia tutafute namna gani.

Mheshimiwa Spika, ukitokea mkoa wa Njombe bila kutaja Mchuchuma na Liganga unakuwa bado hujamaliza hotuba yako vizuri. Mradi wa Mchuchuma na Liganga bado kuna maombi kwa wananchi; tupate majibu mazuri kwamba ni lini mradi huu utaanza ku-take off tumekuwa tunapata majibu mara kwa mara kwamba linashughulikiwa, tunashukuru sana ipo kwenye Ilani lakini sasa tunataka mradi huu uanze kazi, aje Mheshimiwa Mama yetu azindue, Rais wetu, aje Waziri Mkuu na tunashukuru alifika pale Njombe, ahsante sana. Tuje tuzindue rasmi mradi huu wa Mchuchuma na Liganga.

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Madiwani, bado Madiwani Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata wanaomba waendelee kukumbukwa. Madiwani wanafanya kazi nzuri sana kusimamia utekelezaji wa Ilani. Wanasimamia ukamilishaji wa maboma, ukamilishaji wa shule, zahanati. Kwa kweli maboresho tunaomba yaangaliwe. Madiwani wanafanya kazi nzuri hivyo haki zao ziendelee kuangaliwa; ni namna gani tunaboresha haki za Madiwani. Eneo hili ni muhimu sana tuone namna ya kuboresha.

Mheshimiwa Spika, na tunaposema Madiwani timu yao inakwenda pia na Wenyeviti wa Vijiji lakini focus kubwa tuanze kwanza na kwa Madiwani. Hawa ni watu wanaokaa katika kata siku zote, wanashughulika na changomoto aina mbalimbali katika Serikali za Mitaa. Kwa hiyo Madiwani wamekuwa wanachapa kazi sana, wanawajibika sana usiku na mchana, masaa ishirini na nne wako pale na wananchi kwa hiyo Madiwani tuone ni namna gani tunaendelea kuwasaidia... (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. DKT. PINDI H. CHANA: …Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja.