Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nami kwa kunipatia leo nafasi hii ya kuchangia. Kwa niaba ya wanananchi wa Jimbo la Msalala naomba niipongeze Serikali kwa mambo makubwa na mazito kabisa ambayo yamefanyika ndani ya miaka mitano iliyopita na ambayo kwa sasa yanaendelea kufanyika kwa Awamu hii ya Sita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tumesomewa mpango hapa na hotuba ya Waziri Mkuu kwa ajili ya bajeti ya Waziri Mkuu. Hotuba hii ya bajeti ya Waziri Mkuu ni hotuba iliyoshiba kweli kweli; imeeleza wapi tumetoka na inatuelekeza wapi tunaenda. Niseme kwamba katika hotuba hii ya bajeti Waziri Mkuu ameelezea mambo mengi na nijikite kuelezea mambo machache.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuelezea mradi wa Julius Nyerere. Mradi huu wa Julius Nyerere ni mradi muhimu sana na niseme tu kwa niaba ya wananchi wa Msalala, tunaunga mkono Serikali ili mradi huu uende ukatekelezwe na ukamilike. Kwa hiyo, tunafahamu the cheapest source of energy kwenye nchi hii ni umeme unaotokana na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia gharama ya sasa ya umeme, wananchi wetu wanalia huko; unit moja kwa sasa ni shilingi 100/=, lakini ukiangalia manufaa ya mradi huu utakapokamilika, uzalishaji wa unit moja katika mradi huu wanaenda kutumia kiasi cha shilingi 36 kuzalisha unit moja. Maana yake nini? Ni kwamba itaenda kushusha gharama ya uzalishaji kwenye viwanda na pia itashusha gharama ya unit kwa wanananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niseme, japo mradi huu utaenda kukamilika, niipongeze Wizara ya Nishati, inafanya kazi kubwa. Katika Jimbo langu la Msalala ni ukweli usiopingika kwamba watu wa Nishati wanafanya kazi kubwa, lakini kuna baadhi ya maeneo umeme huu haujafika. Wananchi wa Msalala tunapoona mtu anasimama na kuupinga mradi huu, tunashikwa na hasira kwa sababu Jimbo la Msalala lina Kata 18 na Kata zaidi ya 12 hazina umeme. Kwa hiyo, matarajio yetu ni kwamba mradi huu wa REA III ambao kimsingi utaenda kukamilika, ni kwamba baada ya mradi huu wa Mwalimu Nyerere kukamilika tutakuwa na umeme wa uhakika lakini pia nasi wananchi wa Jimbo la Msalala tutanufaika na nishati hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie suala la kilimo. Katika Kata 10 katika Jimbo langu la Msalala ni wakulima wa mpunga. Kuwepo na ukamilishaji wa mradi huu na uwekwaji wa umeme katika Kata zetu hizi utachochea uchumi kwa wakulima. Maana yake nini? Wakulima wataweza sasa kuchakata na kuongeza dhamani ya mazao hayo katika maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kwenye suala la madini. Nimeona hapa imeelezewa na ninaipongeza Wizara imefanya kazi nzuri sana kwenye Sekta ya Madini. Namwomba Mheshimiwa Waziri Dotto hapa, sisi tunaotoka katika maeneo ya migodi, Mheshimiwa Bonnah Kaluwa amezungumza hapa, kuna masuala ya fidia ambayo kimsingi imekuwa ni tatizo katika maeneo yetu haya.

SPIKA: Mheshimiwa, anaitwa Bonnah Kamoli.

MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Bonnah Kamoli.

SPIKA: Eeeh! (Makofi/Kicheko)

MHE. IDDI KASSIM IDDI: Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la fidia kwenye eneo langu. Tunatambua ya kwamba kuna mgodi umeanzishwa pale katika eneo letu Kata ya Bulyanhulu ambao ni mgodi wa Bulyanhulu. Baada ya hao watu kuanzisha mradi pale kuna watu mpaka leo toka mwaka 1966 hawajalipwa fidia ya ardhi yao. Naiomba Wizara na Serikali kuhakikisha ya kwamba tunamaliza tatizo hili, kwani ni la muda mrefu sana. Tatizo hili limedumu toka Mheshimiwa Rais Mwinyi akiwa bado ni Rais.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naiomba Wizara kwamba sasa tuhakikishe tunatatua tatizo hili la mgogoro na fidia kwa wananchi hao wa Kata ya Bulyanhulu.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, maslahi ya wafanyakazi. Bado kuna wafanyakazi wanadai. Naomba sasa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wameshaanza kulifanyia kazi, waharakishe kuhakikisha kwamba wafanyakazi wale wanapata stahiki zao mapema ili waweze kujikita kwenye shughuli za uchumi na kutumia fedha hizo katika mambo mengine.

Mheshimiwa Spika, naomba nizungumzie suala la maji. Tuna miradi ya maji katika Jimbo langu la Msalala. Ni kazi nzuri inafanywa na kaka yangu Aweso, lakini namwomba Mheshimiwa Aweso aweze kuharakisha mradi wa maji unaotoka Mangu mpaka Ilogi uweze kukamilika. Baada kukamilika sasa waanze usambazaji wa maji mara moja katika Kata ya Ikinda, Kata ya Runguya na Kata ya Segese ili wananchi wale nao waweze kufaidika na huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la barabara limekuwa ni mtihani. Wabunge wengi wanalia hapa kuhusu suala la TARURA, lakini mimi naweza nikasema ni jimbo langu la Msalala ni jimbo ambalo lina miundombinu mibovu sana katika. Leo hii tunapozungumza hapa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Hayati Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kampeni, tuliahidiwa kupata barabara mbili zenye kiwango cha lami. Kuna barabara inayotoka Geita - Bukori -Kata ya Bulyanhulu – Kahama. Barabara hii tuliahidiwa kujengwa kiwango cha lami. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naomba niikumbushe Wizara kwamba wakati Serikali inaingia makubaliano na mgodi huu wa Twiga, moja ya makubaliono ambayo walikaa wakakubaliana ni kuhakikisha kwamba wanatenga kiasi cha dola milioni 40 ili waweze kukamilisha barabara hii kwa kiwango cha lami. Fedha hizi zipo, naiomba Wizara husika iweze kuona ni namna gani sasa wanaenda kukaa na kuzungumza fedha hizi zipelekwe ujenzi ili barabara hii ianze kujengwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, hivyo hivyo, tuna barabara nyingine ambayo inatoka Solwa inakuja Bulige inaenda Ngaya na Kahama. Barabara hii pia imeahidiwa kwa kiwango cha lami. Naendelea kuomba Wizara ione namna gani basi inaweza kuanza ujenzi wa barabara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna barabara moja ambayo ni ndefu sana ina zaidi ya kilometa 85. Barabara hii inaunganisha Makao Makuu na Jimbo la Solwa. Naomba Wizara ya Ujenzi waone namna gani basi wanaweza kuanza mchakato wa kuihamisha barabara hii kutoka TARURA iende TANROADS ili ingie kwenye matengenezo ya kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kuishia hapo, niseme kwamba naunga mkono hoja. (Makofi)