Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Eng. Dr. Leonard Madaraka Chamuriho

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa fursa hii ya kuchangia Mpango huu katika Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Spika, kwa vile ni mara yangu ya kwanza kusimama rasmi kuchangia, napenda kushukuru Mwenyezi Mungu kwanza kwa kutuweka hai na kukutana hapa. Pia kumshukuru aliyeniteua Hayati Rais wetu Mtukufu lakini vilevile kumshukuru Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kunibakiza katika nafasi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa hii kuchangia hoja ambazo zimetolewa katika mjadala huu nikianza na Shirika letu la Ndege la Tanzania. Shirika la Ndege la Tanzania mpango wa kulifufua ulipoanza 2016 haukuanza kwa kukurupuka, kwani tulianza na mpango wa mwaka mmoja wa Oktoba 2016 hadi Oktoba 2017 na mpango mkakati uliofuata ambao ulikuwa ni wa miaka mitano ulianza Julai 2017 na utaendelea hadi Juni 2022. Kwa hiyo, tunaendelea vizuri na tija inaanza kuonekana kwani tulipoanza tulikuwa tuna miruko 576 kwa mwaka, lakini sasa tumefika miruko 4,752 kwa mwaka ambapo lengo letu ni kufika miruko 6,500 kwa mwaka lengo ambalo tumekwama kidogo kulifikia kwa sababu ya changamoto ya COVID ambayo imezuia ndege zetu kuruka kwenda katika destinations mpya za China, Afrika Kusini, Nigeria na London.
(Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile kulikuwa na hoja ya ufanisi wa ndege zetu, lakini ndege hizi japokuwa tulianza na ndege moja mwaka 2016 na sasa hivi tuna ndege nane hazikuja kwa siku moja, kwa hiyo, kuchukua wastani wa pamoja siyo sawa. Ndege mbili za kwanza tulizipokea Septemba 2016, ndege iliyofuata ilikuwa Aprili 2018, Boeing ya kwanza tuliipokea Julai 2018 na zile Air Bus ya kwanza tulipokea Desemba 2018 na ya pili Januari 2019. Dreamliner ya pili tulipokea Oktoba 2019 na Bombardier ya mwisho tulipokea Desemba 2019. Kwa hiyo, utaona hizi ndege zinakuja kulingana na mpango na tatu zilizobaki zilikuwa zije mwaka jana lakini zimekwamishwa na COVID. Hivyo mipango yetu inakwenda vizuri na miruko hiyo inadhibitiwa kisheria hivyo hatuwezi kuruka kukiuka Sheria za Udhibiti wa Marubani pamoja na Wahudumu wa Ndege. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukiangalia kwa wastani miruko ya Bombardier ya kwetu sasa hivi inaruka saa kumi na nusu kwa siku lakini saa ambayo inapendekezwa huwa ni saa nane, kwa hiyo, tumezidisha tunafanya vizuri sana. Kwa Boeing 787 ambayo ni Dreamliner tunaruka sasa hivi saa tatu na nusu inapendekezwa saa 12 na Air bus tunaruka saa sita lakini inapendekezwa saa 10. Sasa hizi ndege mbili kubwa tumekwamba tufikisha hiyo miruko kwa sababu safari ya China ambayo ndiyo ilikuwa imepangiwa na ya Uingereza na Afrika Kusini ndio imesababisha changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunaendelea vizuri na ufanisi unajidhihirisha wazi kwani ukiangalia umiliki wa soko tulivyoanza mwaka 2016 ulikuwa ni asilimia 4.5 lakini leo tunaongelea umiliki wa soko wa asilimia 75. Hakuna Shirika la Ndege ambalo limeweza kufikia ufanisi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile tukiangalia jinsi ilivyochangia watalii wetu, tulikuwa na watalii milioni 1.2 lakini sasa hivi tuna watalii wanaokaribia milioni mbili. Hawa wote wamesababishwa na hizo ndege zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile ndege zetu zimeweza kutoa huduma kwa Watanzania waliokwama nje ya nchi wakati wa janga la COVID. Vilevile zimechangia vizuri katika soko la mazao ya mifugo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na hoja za uendelezaji wa bandari. Uendelezaji wa bandari zetu unaendana pamoja na Mpango wa Taifa wa Uendelezaji wa Bandari yaani National Port Master Plan ya mwaka 2020-2040. Ukiangalia kwa sasa hivi bandari yetu ya Dar es Salaam ilikuwa na uwezo wa kubeba tani milioni 11 kwa mwaka lakini baada ya maboresho yatakayokamilika mwaka 2024 itaweza kuwa na uwezo wa kuhudumia tani milioni 28 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile tukiangalia bandari zetu za Mtwara na Tanga; ya Mtwara ilikuwa inaweza kuhudumia tani laki nne kwa mwaka lakini sasa hivi itahudumia tani milioni moja kwa mwaka. Bandari ya Tanga ilikuwa inahudumia tani laki tano kwa mwaka lakini nayo baada ya maboresha tunayofanya sasa hivi itaweza kuhudumia tani milioni moja kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa Bandari ya Bagamoyo na ujenzi na uendelezaji wa bandari zote utazingatia mahitaji na ukuaji wa maboresho tunayoendelea kuyafanya sasa katika Bandari zetu za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara. Endapo atatokea mwekezaji yeyote ambaye ataweza kutusaidia katika kuboresha bandari yoyote kulingana na mahitaji mapya milango ipo wazi na tuko tayari kukabiliana na changamoto hiyo. Katika hoja hii ya bandari, tayari kama Serikali tumeshakutana na hoja hii tunayo kwa Waziri Mkuu ambapo tumeangalia mapendekezo yote na mmetoa mapendekezo mazuri ambayo tutayatumia katika ushirikishaji wa maboresho wa bandari zetu hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hoja nyingine ambayo imetolewa ni kuhusu Reli ya TAZARA, ni kweli kwamba reli hii ilikuwa inasuasua hapo mwanzo. Tayari tuna mkakati mzuri wa kuihuisha reli hiyo. Tumeshaanza mchakato wa sheria, sheria hii imechukua muda kidogo kuihuisha lakini imebidi iwe hivyo kwa sababu sheria hii inabidi iwe moja ambayo itapitishwa na Bunge lako pamoja na Bunge la Zambia kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Spika, sheria hii tutakapoirekebisha itaruhusu wawekezaji kwani sasa hairuhusu, vilevile itaruhusu upatikanaji wa watumishi kutoka mahali popote kwani sasa hivi tuna hii changamoto ambayo sheria inasema lazima Mtendaji Mkuu atoke Zambia. Kwa hilo, lipo katika mkakati wetu wa kuendeleza hiyo reli mpya ya TAZARA. Vilevile tunaendelea na majadiliano na wenzetu wa China pamoja na wawekezaji wengine ili tuweze kuirekebisha hiyo reli yetu ili iweze kuwa na ufanisi zaidi kuliko ambavyo ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo katika mikakati hiyo, tunaungana na aliyetoa kwamba tuongeze matawi ya Tunduma hadi Kasanga Port, kwani upembuzi huo tunaangalia haya yote ili tuiboreshe reli yetu. Vile vile katika TAZARA tunafanya tafiti za bei ili kuwa na bei shindani ili iweze kushindana pamoja na taratibu nyingine za usafiri.

Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kuchangia kuhusu reli. Tuna reli za aina tatu hapa kwetu. Kwanza nianze na hii reli ya kisasa, standard gauge ambayo awamu ya kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na ina vipande vitano. Kipande cha kwanza ni kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro, sasa hivi tumefikia asilimia 92; kipande cha pili ni kutoka Morogoro hadi Makutupora, tumefikia hatua ya asilimia 58; kipande cha tano ambacho ni Mwanza hadi Isaka, tumefikia hatua ya mobilization na tayari mkandarasi ameshalipwa malipo ya awali tarehe 1 Aprili, mwaka huu 2021. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ilizuka hoja ya ujenzi wa reli kwa muda mrefu lakini kwa ujenzi wa awamu ya kwanza imepangwa kukamilika 2025. Hivyo, tunaendelea na kutafuta wawekezaji ambao watatusaidia katika kumalizia kipande cha tatu na kipande cha nne kutoka Makutupora hadi Tabora na kutoka Tabora hadi Isaka. Awamu ya pili itakuwa ni kutoka Tabora hadi Kigoma pamoja na Mpanda hadi Kaliuwa. Kwa hiyo, sasa hivi tunaendelea na upembuzi yakinifu pamoja na usanifu wa kina ili itakapokamilika tuweze kupata wawekezaji wa sehemu hizo. Hivyo mtandao wa reli nzima utajengwa kulingana na uwekezaji lakini mradi huo utakuwa ni mchanganyiko pamoja na fedha za ndani, kwenye mikopo, PPP, pamoja na fedha za ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, kulikuwa na hoja ya wafanyakazi wa kigeni kuwa wengi kule lakini hili linadhibitiwa kwa mkataba na tunahakikisha kwamba wafanyakazi wa kigeni ni asilimia 20 tu katika ujenzi huu na wazawa wanakuwa asilimia 80. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vile vile, tuna mpango wa reli yetu ya Mtwara hadi Mbambabay na Matai kuelekea Mchuchuma hadi Liganga. Hii imepangwa kujengwa kwa ubia kwa sekta binafsi na Umma. Tayari tulikuwa tuna Mshauri Mwelekezi KPMG JV ambaye alitufanyia kazi ambayo hatukuridhika nayo, tayari tumeshamwondoa na sasa hivi tunatafuta Mshauri Mwelekezi mwingine ambaye atatupatia mwekezaji mahiri ili tuweze kuendelea na mradi huo kama ambavyo tumekuwa tumepanga.

Mheshimiwa Spika, vile vile napenda kuongelea masuala ya barabara ambayo tumeendelea na vipaumbele…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri.

WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru na ninaunga mkono hoja. (Makofi)