Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Francis Isack Mtinga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Iramba Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. FRANCIS I. MTINGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kupata nafasi nami kuweza kuchangia Mpango huu wa Tatu. Kwa sababu nafasi yenyewe ni ya dakika tano, niende moja kwa moja kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, mchango wangu unajielekeza katika kutafuta fedha ambazo zitatusaidia kwenda kwenye TARURA ili Jimbo langu la Mkalama, Iramba Mashariki liweze kupata fedha za kutengeneza barabara. Yako mambo ambayo mara nyingi Serikali imekuwa ikiyatumia kupata fedha na mara nyingi sana wamekuwa wakienda kwenye vinywaji, lakini safari hii fedha ya uhakika ipo kwenye mafuta.

Mheshimiwa Spika, viko vifungu vingi sana ambavyo kwa ujumla wake vinatengeneza bei ya mafuta ya lita ambayo tunanunua kwa sasa. Katika vifungu hivyo, kimojawapo ni kifungu ambacho kinahusu marking, yaani kuweka alama ya mafuta ambayo yako on transit na yale ambayo yanatumika ndani ili kuepuka wanaokwepa kodi na kuepuka uchakachuaji.

Mheshimiwa Spika, kifungu hiki, kinafanywa na Kampuni ambayo imepata tender na gharama yake inayolipwa, ni shilingi 14 na senti 22 kwa lita moja. TBS pia wanapata pesa kutoka kwenye hivi vifungu vya mafuta, wenyewe wanapata kama shilingi moja na senti kadhaa hivi.

Mheshimiwa Spika, naona kazi hii ya kuweka marking, TBS wanaweza kuifanya kwa uhakika tu, kwa sababu ndiyo Shirika letu la Viwango. Kazi hii ikifanywa na TBS hata kama wataongezewa fedha kidogo kutoka kila shilingi moja tutaokoa fedha nyingi sana ambazo zinafanywa na kampuni; na kwa bahati nzuri kampuni hii muda wake umeisha lakini wamekuwa wakiongezewa ongezewa muda tu kwa miezi mitatu mitatu na EWURA sijui kwa utaratibu gani? Kama kazi hii itafanywa na TBS, hii shilingi 14 tukaamua kui-save, tutaipeleka TARURA.

Mheshimiwa Spika, naomba tu niseme jinsi fedha hii itakavyopatikana. Takribani kwa mwezi mmoja, mafuta yanayoingia nchini ni kati ya lita 390,000 mpaka 400,000 metric ton ambapo Metric ton moja ni sawa na lita 1,000. Kwa hiyo, ukibadili hizi metric ton 390,000 kuwa lita ni kama lita 390,000,000 kwa mwezi. Uki-compute hizi shilingi 14 kwa kila lita kwa mwezi mmoja, unapata takribani shilingi 5,545,800,000/=. Ukifanya mara 12 kwa mwaka unapata shilingi 66,549,000,000/=. Fedha hii ikienda TARURA, Majimbo yetu yatakuwa yamepoma na bado kazi ya marking inaweza ikafanywa na TBS.

Mheshimiwa Spika, namwomba Waziri wa Fedha, hii ni shilingi bilioni tano kwa mwezi, ni hela ambayo anaweza kuipata mwezi ujao tu akiamua, kwa sababu hata hiyo Kampuni inayofanya kazi hiyo, muda wake umeisha. Kwa hiyo, ni kauli tu na maamuzi kwamba kazi hii sasa ifanywe na TBS na ile shilingi 14 kwa lita ambayo ilikuwa inachukuliwa na hii Kampuni ziende kwa ajili ya TARURA. Kila mwezi tuna uhakika wa kutengeneza shilingi bilioni tano ambapo wananchi wetu na barabara zetu zitapata fedha ya uhakika kiasi cha shilingi bilioni 66,549,000,000 kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba hebu Waziri afanye maamuzi haya, kwa sababu ni maamuzi ambayo yana maslahi ya Watanzania hata Mungu ataona. Baada ya kutafuta pesa, naomba tu niseme, huu ni Mpango wa Tatu kuchangia, kuusikiliza tangu niingie Bunge hili kwa sisi ambao tunaitwa Form One. Mchango wa kwanza kwa Wabunge, ulikuwa unahusu Hotuba ya Rais; mchango wa pili, ulikuwa unahusu Rasimu ya Mpango huu; na sasa Mpango huu.

Mheshimiwa Spika, ambacho nakiona, Waheshimiwa Wabunge wanatoa michango mizuri sana yenye mashiko ya kuongoza nchi hii, lakini yanapokuja majibu ya Mawaziri, zile dakika tano tano, yanakuwa majibu mepesi ambayo hayaendani na uzito wa michango ambayo Waheshimiwa Wabunge wamekuwa wakiitoa.

Mheshimiwa Spika, nakuomba, ikikupendeza utengeneze Kamati Maalum ya Kudumu ambayo itakuwa inaangalia majibu, ili vitu ambavyo viko kwenye Hansard ambavyo Waheshimiwa Wabunge wameshauri Mawaziri, kila linapokuja Bunge linguine, wametekeleza kiasi gani? Ili tupate Hadidu za Rejea. Vinginevyo, tutakuwa tunasema vitu vizuri, watu wanavisikia, wanatupia simu wanatupongeza, lakini implementation yake haipo. Hata vikao vya kawaida huko nje, kuna yatokanayo na maazimio, lakini hapa tukisema, vinaenda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba ukitengeneza Kamati hii, Mawaziri watakuwa wanajua kabisa Bunge lijalo wataenda kuulizwa; hili lilichangiwa, hili lilichangiwa, limefanya kazi gani? Limefika wapi? Yako mambo mazito sana yamechangiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakumbuka nilisikia mchango mmoja wa Mheshimiwa Mbunge mmoja aliongelea suala la kiwanda kikubwa cha pamba kitakachomeza pamba yote ya nchi hii ambayo itatoa tija kwa wakulima, itatoa ajira kwa vijana, tutauza majora nje, lakini ilipofika kwenye majibu, sikusikia, imeishia vivyo hivyo hewani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilisikia Mheshimiwa Mbunge alisema kuhusu mambo ya task force ambayo inasumbua wafanyabiashara, alisema Mheshimiwa Nape pale, lakini ilipokuja kwenye majibu, kimya. Mpaka niliposikia Mheshimiwa Rais wangu analiongelea juzi, wakati anasema watu wasisumbuliwe kuhusu kodi.

Mheshimiwa Spika, hebu tutengeneze Kamati ambayo itakuwa inafuatilia mambo haya kwa Mawaziri ili vitu vinavyosemwa humu, tuvione vinafanya kazi kwa sababu ni vitu vyenye mashiko, ni nondo zinashuka humu lakini zinaishia hewani hewani tu. Matokeo yake mpaka watu wengine huko nje wanaanza kusema viongozi sio asilimia 60, hatuna uwezo. Uwezo tunao. Kama watu hawawezi kutoa mrerejesho, wapishe wengine waweze kufanya hizi kazi.

Mheshimiwa Spika, fedha zinazopatikana TARURA, naamini kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Mwigulu atalijibu hili, kwa sababu ni kauli yake tu inatupatia mabilioni ambayo yanakwenda kwenye mambo ya barabara.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)