Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Edward Olelekaita Kisau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiteto

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. EDWARD O. KISAU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa fursa hii nichangie mpango huu. Kwanza nimpongeze sana Waziri wa Fedha kwa umahiri wa ku-present mpango huu. Katika kusoma mpango huu ziko baadhi ya taarifa ambazo ndiyo zinaongoza mpango huu. Moja ni Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, nyingine ni Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, nyingine ni hotuba mbili za Mheshimiwa Rais, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, na Mungu amlaze mahali pema peponi; nyingine ni Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki 2020 na nyingine ni Agenda 2063. Lakini muhimu kuliko yote ni Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2020-2025, hii hapa.

Mheshimiwa Spika, kama kuna ilani bora ambayo imewahi kuandikwa kwa utaalam mwingi sana na kwa lugha nyepesi sana ambayo Watanzania wanaifahamu ni Ilani ya Chama Cha Mapinduzi 2025. Na kama kuna zawadi ametuachia Hayati Dkt. John Pombe Magufuli, ni Ilani ya Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Bunge hili mkitaka heshima kwa Watanzania, na legacy ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli ni kuleta mpango unaotekeleza ilani ya miaka mitano ijayo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wakati tunatafuta kura, nimenunua ilani hizi na nimewapa wananchi wangu, nimewaambia wasome; Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji. Kwasababu miradi ya kimaendeleo ipo. Kama Bunge hili linataka heshima kwa Watanzania tuisaidie Serikali kutekeleza ilani hii kwa asilimia 100. Na sisi tutakuwa tumejenga heshima kubwa sana kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa wale ambao walikuwa Chato, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete alisema hivi; mwanasiasa kwa level ya Urais ukichaguliwa miaka mitano ya kwanza unafanya bidii ile miaka mitano ili uchaguliwe tena, lakini miaka mitano ile mingine ya mwisho unaacha legacy.

Mheshimiwa Spika, ilani hii ina tafsiri zote mbili. Ni legacy ya Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kama tutakuwa tumetekeleza kwa asilimia 100. Lakini vilevile kwa lugha ya kisheria, ni fast turn ya Rais mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kama tutawekeza nguvu kutekeleza ilani hii kwa maana ya fast turn ya Mheshimiwa Rais wetu na legacy ya Dkt. John Pombe Magufuli, maana yake mpango huu tunatakiwa tu-double katika kuleta utekelezaji wa namna ya kutekeleza ilani hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukizungumza mambo ya kilimo, mimi nilikuwa naongea na wataalam wangu wa Wilaya ya Kiteto hapo. Kati ya hekta 1,000 walizowekeza kwa ajili ya umwagiliaji, ni hekta 15 tu ndiyo zinatumika. Na nilizungumza na Mheshimiwa Bashe hapa, excellent, alinishauri tulete andiko la mradi ili tuweze kuongeza hekta zile kwa ajili ya umwagiliaji, na tumeshaandika Mheshimiwa Naibu Waziri, the ball is on you.

Mheshimiwa Spika, sisi tunachotaka baada ya miaka mitano wananchi wale, Watanzania wale waliokuwa wanalia siku ile waweze kufuatilia ilani yao na kila kitu kilichosemwa kiwe kimetekelezwa kwa asilimia 100.

Mheshimiwa Spika, ilani hii inazungumzia barabara mbili kuu nzuri sana; Barabara ya kutoka Kongwa – Kiteto – Simanjiro mpaka Arusha, kilometa 430, ni mikoa karibu minne; Dodoma, Manyara, Arusha na Kilimanjaro. Unaunganisha mikoa minne, ni uchumi. Najua barabara hii iko kwenye ilani hii, lakini sasa tuweke vipaumbele.

Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Tanga – Kilindi – Kiteto mpaka Singida, karibu mikoa mingine mitatu. Tulete sasa mkakati wa namna ya kutekeleza ilani hii ili wananchi hawa, Watanzania hawa waweze kusema legacy ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli imetekelezwa kwa imani kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namalizia na kitu kimoja alichosema Mheshimiwa Rais wetu juzi. Kuna concept inaitwa ya Serikali moja, ambayo sasa naomba Mawaziri wasikilize vizuri sana; sisi Halmashauri yetu ya Kiteto kwa mara ya kwanza baada ya mvua za miaka miwili hii tumepata maji mengi sana na tuna Samaki sasa na wafugaji wameanza kula Samaki sasa. Na wilaya yangu imetengeneza kama source ya mapato kwamba ni pato jipya, wameanza kutoa leseni. Anakuja Wizara ya Maliasili na Utalii anasema ninyi mmepewa leseni lakini hamruhusiwi kuvuna; concept ya Serikali moja.

Mheshimiwa Spika, naomba sana Ofisi ya Waziri Mkuu ishughulike na hii concept ya Serikali moja. Kitu ambacho wananchi hawataki kusumbuliwa kabisa ni Wizara moja inakupa leseni moja halafu mwingine anatoka anasema haiwezekani, hiyo confusion tuondoe. Tukiondoa hiyo wananchi wetu watakuwa wamenufaika.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru na ahsante sana. (Makofi)