Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba moja kwa moja nijielekeze eneo la madini, niliwahi kuzungumza kwenye Bunge hili hapa eneo la madini pekee yake kwa maana ya nchi yetu ya Tanzania lina uwezo wa kuzibeba sekta nyingine. Nikilisema hili, niendelee kusema mbele ya Bunge lako mimi ni mchimbaji mdogo wa madini, kwa hiyo naomba nielezee kile kitu ninachokifahamu.

Mheshimiwa Spika, acha madini mengine, acha Tanzanite, acha madini ya vito zungumzia dhahabu peke yake. Kupitia dhahabu kwa kupitia wachimbaji wadogo nishukuru kwamba Serikali imeboresha maeneo hayo tozo mbalimbali zimepunguzwa, sheria zimerekebishwa, tunaweza kwenda mbali Zaidi. Nashukuru mara mwisho nimemsikia Rais wetu mpendwa akiongelea suala moja, leo unaweza ukawepo kwenye hifadhi, sikatai uhifadhi, lakini kwenye hifadhi kuna dhahabu, kuna almasi, kwa kupitia almasi hiyo, kwa kupitia dhahabu hiyo, tuna uwezo wa kufanya mambo mengine. Tembo hali dhahabu, kwa hiyo unaweza kwa kuitoa dhahabu tukajenga mahospitali, kwa kutoa dhahabu tukawaendeleza akinamama.

Mheshimiwa Spika, katika eneo hili pia naomba ulifahamu vizuri ninachokiomba sasa hivi, tafiti mbalimbali ambazo sekta imekuwa ikizifanya, tafiti hizo ziendee kwenda huko mbali. Kuna watu hapa wanatuangalia wachimbaji kama labda watu wa kupiga ramli hivi na mambo mengine ya namna hiyo, hapana. Tukiwa na tafiti kwa kupitia GST hakuna uchawi, ni suala tu la kujua kiwango cha mashapo, kujua dhahabu iko wapi, unachimbaje, kwa hiyo niombe na katika hili nafahamu kuna maeneo ambapo Wizara kwa kupitia Wizara ya Fedha, wameendelea kutoa ujenzi wa vituo mahiri. Niombe sana ili tuendelee kupata zao hasa kwa maana ya zao la dhahabu, bila tafiti, unaweza kushangaa leo umekaa hapa Dodoma dhahabu mtu anachimba choo kapata dhahabu, mtu amekwenda shamba analima kapata dhahabu maana yake kama ni kwa kupitia tafiti hatufanya kwa kubahatisha kwa kiwango hicho.

Mheshimiwa Spika, niseme, katika eneo hili leo sehemu ambayo inaisadia nchi katika eneo la ajira ni pamoja na uchimbaji. Nikilisema hili namaanisha, unaweza ukakuta sehemu ya mgodi mmoja idadi ya watu kama wale wangekuwa barabarani ni tatizo kwa nchi. Kwa hiyo ninapozungumzia habari ya kwenda kuimarisha huko namaahisha.

Mheshimiwa Spika, kubwa tuende kwenye jambo lingine. Leo kwa mfano, maeneo mengine kwa mfano kama Mkoa wa Katavi unaweza ukachimba ukapata dhahabu, ile dhahabu ni asilimia themanini tu, ukienda kuuza wanakuambia madini yako ni asilimia themanini, Serikali iende mbali Zaidi, tukisema themanini ina maana hii ishirini ni kitu gani, unakuta ni madini mengine yanaweza yakawa madini ya fedha, yanaweza yakawa madini ya shaba. Kwa hiyo Serikali itusaidie, watu wanajenga viwanda vikubwa, leo teknolojia iko wazi, maana yake huyu mtu mmoja anapoteza hayo madini mengine, lakini kama Serikali itakuja na utaratibu kwamba bwana nyie wachimbaji kadhaa mji-organize najua mipango hiyo ipo, lakini twende mbali zaidi kwa maana huyu mtu ukimsaidia hapahapa nchini katika kuchimba madini yake, hiyo dhahabu yake, baada ya kuiuza nje kama madini ghafi, tukilifanya hapa nchini mbali ya kuuza dhahabu tu anaweza akauza na madini mengine, yawe madini ya shaba au yawe madini ya fedha. Naomba sana Serikali yangu sikivu iweze kuliangalia hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikizungumzia eneo hilo hilo la uchimbaji kwa maana ya teknolojia, leo niliseme hapa, zamani tulikuwa tukiwaona akinamama kama ni watu ambao hawawezi wakajikita katika eneo hilo la uchimbaji, wakifikiri kwamba ni kazi ilikuwa inahitaji nguvu zaidi na watu wenye misuli Zaidi. Serikali ina nafasi ya kufanya jambo moja, niwaombe turudi kwenye kuwapa ruzuku wachimbaji, nikisema hilo namaanisha kwa kupitia ruzuku, fedha iliyojificha huko itatoka na itaendeleza maeneo yetu.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Nakushukuru sana na Mungu akubariki. (Makofi)