Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, kwanza nashukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia huu mpango wa maendeleo kwa miaka mitano ijayo. Kwanza nashukuru wachangiaji wenzangu wengi wamezungumza katika maeneo mengi, lakini kipekee nataka kumshukuru pia Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Prof. Mkenda na Msaidizi wake kwa kazi nzuri wanaoifanya.

Mheshimiwa Spika, katika michango yangu iliyopita nilikuwa nimezungumzia mambo ya kilimo. Kwa upande wa ugani nilizungumzia habari ya mbegu, habari ya utafiti wa udongo na pia habari ya soko. Nilipopata nafasi ya kuzungumza naye wiki iliyopita tukiwa tunakunywa chai, alinieleza kwa shauku kubwa sana ni namna gani ambapo ameweka bajeti kwanza kuhakikisha kwamba tunapata mbegu bora. Hiyo inatokana na kuwekeza kwenye maeneo ya umwagiliaji, kwamba katika maeneo yanayozalisha mbegu wanasema sasa watazalisha mwaka mzima, kwa sababu tunakwenda kuweka umwangiliaji. Kwenye soko akawa ananieleza kwamba mwaka huu tutafanya maonyesho ya bidhaa zetu China na Oman na mambo mengi alizungumza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa udongo, alinieleza kwamba wanakwenda kununua vifaa kwa ajili ya Halmashauri 45 ili tuwe tunapima udongo. Kwa hiyo, kwa kweli kwa kazi hiyo nzuri nawapongeza, lakini baada ya hapo acha niendelee na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nchi hii nimemsikia hata Mheshimiwa Rais akizungumza siku ile kwamba tunaweza tukapata pesa nyingi kwenye madini. Alizungumzia suala la Serengeti, lakini nchi hii ina maeneo mengi sana yenye madini ambayo Watanzania hatujafanya utafiti. Wazo langu nilikuwa nafikiri kwamba Serikali ingeweka bajeti ili tutengeneze kama kitabu ambacho kinaonyesha maeneo yote Tanzania. Tufanye utafiti ili tuandike na mwekezaji anapokuja aambiwe ukienda Kalenga utapata madini haya. Kule Kalenga wazee wameniambia kama maeneo matatu muhimu, kwamba zamani tulikuwa tunachimba madini hapa; na kuna madini mengi.

Mheshimiwa Spika, sasa nilikuwa naishauri Serikali, katika mipango yake tuweke alama (marks) kwamba eneo hili na hili unaweza ukapata madini haya, ili hata wawekezaji wanapokuja, ni rahisi sasa tukimpa kile kitabu, achague kwamba mimi nikawekeze Kalenga kwa sababu naweza kupata Shaba au Dhahabu. Kwa hiyo, hilo tulifikirie katika mipango ya baadaye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna eneo la pili ambapo nimejihusisha kidogo katika utafutaji wa hizo wanazoita tunu na malikale. Nimewekeza fedha nyingi, lakini nimefanya katika kipindi cha miaka miwili nikakimbia. Hili eneo inaonekana ni muhimu sana na watu wapo wenye ushuhuda kwamba wamekuwa wakipata fedha na hizi tunu zipo. Sasa ushauri wangu, kuna mambo mawili kwamba ukienda Maliasili, wanataka ulipie ile leseni miezi mitatu mitatu. Sasa miezi mitatu mitatu hii, watafiti wengi wamekuwa wakifanya huko zaidi ya mwaka mmoja mpaka inaendelea hata miaka mitano au sita. Sasa inakuwa ni gharama kulipa laki tano tano kwa miezi mitatu.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa nafikiri kwa sababu eneo hili lina watu wengi na wengi sasa hivi wanafanya na hawalipi hata leseni, kwa sababu wako huko porini, wanaona hii miezi mitatu mitatu ni gharama. Nilikuwa naishauri Serikali, wenzetu hawa wa Maliasili angalau wangeweza ku-charge hata kwa miezi sita sita ili kuwapa nafasi hawa watu wanaofanya utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo linguine, nimegundua kwenye huu utafiti wa tunu, kuna utamaduni wa Kijerumani katika mambo haya. Nikawa nawaza, kama hawa Wajerumani wanahusika, kwa nini Serikali isifikirie sasa kutafuta hawa wazee wa Kijerumani ambao wanaonekana wana ramani za haya mambo ya malikale, tukafanya partnership kama tunaweza kutoa hizi tunu, basi wao wabakie na asilimia 40, sisi tubakie na asilimia 60. Ili sasa hili jambo liwe wazi, kwa sababu watu wanajitafutia tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nina Ushahidi, kuna mzee mmoja ambaye nilikuwa nafanya naye utafiti, hata sasa nimemwacha site, mimi nimemkimbia baada ya kuona gharama zinakuwa nyingi. Anasema yeye alifanya kazi na Wajerumani na hiyo scanner anayoitumia katika kuangalia maeneo ambayo madini yapo, ni ya Kijerumani na alipewa na Mjerumani. Kwa hiyo, maana yake haya mambo yapo, lakini hayajawa wazi sana. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri katika eneo hilo nalo, tuone; kwanza, kupunguza hizo gharama za kulipia hivyo vibali na pili tuone kama tunaweza tukawatafuta hao Wajerumani ili tushirikiane nao.

Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa najaribu kuliangalia kwamba kwenye mashirika yetu ya Serikali performance yake imekuwa kidogo, lakini nikaja nikawa nafanya utafiti kujua kuna tatizo gani? Kwa nini kuna performance ndogo? Nikaliangalia kama shirika la TTCL ambapo mimi nimefanya kazi kwenye mitandao kwa miaka 20. Yaani hatujalipa nafasi, kama unamteua Mkurugenzi, basi mpe mamlaka ya kufanya maamuzi na kuweza kufanya maamuzi fulani hata kufanya promotions. Kwa mfano, kwenye mitandao tulikuwa tunasema, we copy with pride, kwamba ukionga mwenzako…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)