Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nami naomba kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo. Ni dhahiri kwamba kitu na jambo la muhimu sana ambalo Serikali ingeanza nalo ni kushughulika na suala zima la mikopo ya Elimu ya Juu. Nimekuwa nikisema hili na nitarudia kusema tena kwa sababu tumeshuhudia wanufaika wa mikopo hii wanapata adha kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, tunajua kwamba Serikali inatakiwa kuwekeza kwenye elimu ambapo inatakiwa hata itoe elimu bure kwa watu wetu wa Vyuo Vikuu ili waweze kupata ujuzi ambao utaweza kutumika kwenye Sekta ya Umma, Sekta Binafsi na hata wengine waende nje kama ma-expert, kama vile ambavyo tunaleta watu kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, kwa jinsi ilivyo, Sheria ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Mwaka 2004 ambayo tuliifanyia marekebisho mwaka 2016 ni kandamizi. Hata kwenye ripoti ya CAG ametaja upungufu wa kisheria na kimfumo kwenye ukusanyaji wa haya madeni kwamba yanazidi uwezo ya walipaji. Tumependekeza na Waheshimiwa Wabunge wengi wameonyesha hii adha.

Mheshimiwa Spika, napenda kujielekeza na kuiomba Serikali ifanye marejeo; kufanya makato ya asilimia 15 ya mshahara ghafi wa huyu mfanyakazi ni kubwa sana. Tumesema mara nyingi hapa kwamba huyo mfanyakazi anakatwa asilimia 15 ya mshahara ghafi, anakatwa asilimia 10 ya mifuko ya jamii, anakatwa Pay As You Earn, anakatwa Bima, kuna wengine wana michango mingine, mwisho wa siku unakuta huyu mfanyakazi habaki na chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia ile penalty ya asilimia 10 ambayo ameiweka baada ya maturity ya miezi 24 ni kandamizi. Ambapo amesema mnufaika baada ya miaka miwili kama hana kazi anatakiwa atoe shilingi 100,000/=, short of that anakuwa na penalty ya asilimia 10. Hii mikopo tunaipitisha humu ndani inaenda, is a Revolving Fund; kwa nini muweke hizi tozo kama vile ni riba za mabenki? Isitoshe wameweka na six percent ya kutuza thamani ya fedha (retention). Huku kote ni kumkandamiza mnufaika ambaye ni huyu mtoto wa masikini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni rai yangu Serikali iangalie, hapa hatufanyi biashara, after all hii mikopo tunayotoa ni kodi zetu; hizi za Watanzania sisi masikini ambao tunatoa. Tuhakikishe: mosi, tunawapa Watanzania wote wenye hadhi ya kupata mikopo na wengi wao mayatima na bado wanafurahia masikini, wanapata hii mikopo. Hii mikopo iwe reduced kutoka 15 Percent ije kwenye single digit 5 mpaka 8 ili tuweze kuwasaidia hawa Watanzania masikini. Kwa hiyo, ije sheria hapa, tumesema na tumeomba, wasipoleta natangaza rasmi, ninaandaa Muswada Binafsi wa Sheria wa Mikopo ya Elimu ya Juu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni kwenye Utawala Bora. Mmetaja hapa kwamba moja ya kiashiria cha utekelezaji wa mpango huu ni Utawala Bora. Hata hivyo ukiangalia kwenye Sheria ya Utakatishaji Fedha, kifungu namba 12, 13 na 14 vinatumika vibaya na vinakandamiza sana Watanzania hawa. Hasa tukichukulia mfano kifungu 12 (a) ambacho kinasema mtu yeyote ambaye atajihusisha na muamala ambao una viashiria vya utakatishaji wa fedha ama kwa kujua au kwa kutokujua anakuwa amekosa na anaenda jela.

Mheshimiwa Spika, ameeleza hapa Mheshimiwa Judith kwamba unakuta wengi wanakumbwa wanaenda bila dhamana. Inabidi tutambue kwamba uchumi wetu kwa Tanzania kwa asilimia kubwa unatumia fedha taslimu siyo cash less. Is not a cash less economy. Kwa hiyo, kama ni fedha taslimu, kwa mfano mtu anakuja kwangu, anataka kununua nyumba, ana hela zake, nitajuaje kama hizi hela anataka kutakatisha fedha haramu ambazo amepata somewhere else?

Mheshimiwa Spika, au tukichukulia mfano wa kule kwetu Kijijini Nyanchabakenyi, huyu mtu amepeleka ng’ombe zake kwenye miradi ya Kenya, Mabera kule kwenda kuuza ng’ombe zake 80, anarudi na mfuko wa milioni 100, ikitokea amekamatwa anaambiwa anatakatisha fedha. Kule tunajua kwenye minada hatuna mabenki wala mawakala, hatuwezi kufanya transaction huko, lazima azibebe na akiwa na knowledge aje sasa aziweke kwenye benki; asipokuwa na hiyo knowledge, ataenda kuweka ndani kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwamba watu watoe fedha ndani wazipeleke kwenye mabenki. Ila akikamatwa anakuwa liable kwa that.

Mheshimiwa Spika, kuna mfano mwingine ambayo ni hai. Nilivyokuwa Segerea, kuna wadada walikuwa kule, wamekuja kwa kosa la kutakatisha fedha miaka saba. Wawili; kulikuwa kuna mtu aliyekuwa ni mfanyakazi wa umma, sitamtaja, kumbe amechukua fedha ya mishahara hewa huko, ana girl friends amewaingizia kwenye account as normal transaction. Hao nao wakakamatwa, wamekaa Segerea seven good years, pamoja na mke wake kwamba wametakatisha fedha. Wameachiwa muda siyo mrefu kama miezi mitatu nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hii sheria ni kandamizi sana, lazima ifanyiwe review ili tusiweze kuwanyanyasa hawa Watanzania, tuwe na utawala bora tuweze kutekeleza huu mpango. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ni kwenye Sera ya Fedha na mifumo ya kibenki. Tunajua kabisa kwamba utekelezaji wa mpango huu na ushiriki wa sekta binafsi kwa kiasi kikubwa katika Taifa letu hutegemea Sera ya Fedha na mipango na mifumo yetu ya kibenki. Sote tunajua riba za mikopo kwenye mabenki yetu ziko juu sana; sixteen percent, nyingine seventeen; hizi zimekuwa kandamizi ukilinganisha na nchi nyingine, unakuta ni less than ten; single digit; 3,4,5,6. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kikubwa kupitia Sera ya Fedha, Benki Kuu ilishusha kiwango cha dhamana kutoka 12% mpaka 6%. Cha ajabu mabenki yetu ya ndani yameshusha kutoka 17% mpaka 16.3% tu. Mbaya zaidi, hata kwenye mikopo ambayo ni risk free; kwa mfano, mikopo ya wafanyakazi ambayo marejesho yao yanatokana na mishahara, bado na wenyewe wanakatwa 16.5 percent to 17 percent. Huu ni ukandamizaji.

Mheshimiwa Spika, tunaomba sana, kama kweli tunataka utekelezaji wa mpango uende vizuri na kuweza kuhakikisha kwamba sekta binafsi inashiriki katika utekelezaji wa mpango huu, Serikali ihakikishe inaingilia kati na kuhakikisha kwamba viashiria vyote ambavyo vinapelekea kuwepo na hizi riba kubwa pamoja na kushushwa kiwango cha amani cha Benki Kuu kinapungua au mojawapo unakuta haya mabenki yanajiendesha, kuna gharama kubwa nyingine zinaweza kuepukika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunashuhudia pia utolewaji wa mikopo ambayo haifuati utaratibu, inayoongeza kiwango kikubwa cha mikopo chechefu ambayo wanashindwa kui- control, kwa sababu mzigo unakuja kwa Watanzania hawa wengine wa chini. Kwa hiyo, ili tuweze kuwa na sekta binafsi nyingi na shiriki, napenda Serikali iingilie kati kuhakikisha kwamba riba za mikopo ya mabenki zinaenda chini.

Mheshimiwa Spika, kingine ni usimamizi wa kodi. Tunajua kabisa kwamba haki ni wajibu. TRA wana wajibu wa kukusanya kodi, nasi wananchi tuna wajibu wa kulipa kodi, lakini kumekuwa na tatizo kubwa la muda mrefu. Malalamiko ya marejesho ya kodi ya ongezeko la dhamani, nina maana VAT. Kwa mfano, mwaka 2020 nilivyokuwa kwenye PAC, Kamati yangu ilitembea mashirika mbalimbali, madhalani ALAF; walikuwa wanalalamika wanaidai Serikali zaidi ya shilingi bilioni 17.

Mheshimiwa Spika, nilivyokuwa nashiriki kwenye Kamati ya UKIMWI, taasisi mbalimbali zilikuwa zinalalamika kuhusiana na hii VAT kurejeshwa; na wakienda kuomba, TRA wana-order kwenda kukagua ili kuona kama kuna kosa lolote waweze kufidia zile fedha zinazodaiwa za Kodi ya Ongezeko la Thamani. Wakikosa kupata kosa lolote, wanaendelea ku- delay. Ukienda kukumbushia, wanakuja tena kukagua. Kwa hiyo, inaenda kwenye cycle hiyo, wanakutafutia kosa ili kuweza kufidia hiyo tozo la Ongezeko la Thamani. Hiyo siyo haki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ni hili sharti la moja ya tatu ya kodi ambayo umekadiriwa. Ikitokea Mtanzania amekadiriwa; na kuna cases umekadiriwa shilingi bilioni tisa, umeweka pingamizi kwamba mlivyokadiria sivyo, wanakwambia, toa moja ya tatu. Moja ya tatu ya bilioni tisa is almost bilioni tatu. Unazitoa wapi wakati unajua labda hukuwa liable kulipa tu; kulipa labda shilingi bilioni moja au shilingi milioni 500 umeandikiwa shilingi bilioni tisa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hizi zote lazima ziweze kufanywa review ili tuweze kuwa na harmonization ya wawekezaji, kuvutia wawekezaji wengi waje Tanzania. Kwa hali hii hatuwezi kuvutia wawekezaji kuja Tanzania. Pia wale ambao wako kwenye sekta isiyo rasmi, hawatapata mvuto na mwamko wa kutaka kwenda kwenye sekta rasmi kama kuna bureaucracy hizi zinazoendelea katika mfumo wote wa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine na cha mwisho ni hili la Bandari ya Bagamoyo, limeshika kasi sana kwenye mijadala na ambalo lina tija kwa Taifa letu. Nadhani kama Taifa tujiuleze na tutafakari. Tuangalie kama project ya Bagamoyo is it viable? Ina tija? Kama ina tija, ni nini cha kufanyika? Tusikae na kuji-bide; naangalia mijadala mingi inaenda, ooh masharti yalikuwa makubwa na vile.

Mheshimiwa Spika, kama Taifa lazima tuangalie, kama project ina tija, hatujabanwa kwamba twende na huyo mwekezaji. Tukiona project ina tija, tunaweza tukatangaza tenda tena, kama kuna mwekezaji ambaye anaweza kuja kutaka kuchukua ile bandari kwa manufaa mapana; au Serikali tukaenda through PPP kuweza kujenga ile bandari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine nimejaribu tu kuangalia, narudia tena kusema, bado sijafanya tafiti ya kutosha. Ukiangalia Bandari ya Dar es Salaam, kwa mwaka ina uwezo wa only seventeen million metric tons, tunajenga SGR. Bandari ya Dar es Salaam pale ilivyo haina uwezo wa kupanuka zaidi, lakini kule Bagamoyo already zimeshatumika twenty-seven billions za Watanzania kulipa fidia. Kupitia Special Economic Zone almost over thousand viwanda vinatakiwa vijengwe kule.

Mheshimiwa Spika, sasa tuangalie tija, tufanye cross benefit analysis; tukiona kama Taifa kuwekeza Bagamoyo kuna tija, twende, hatujafungwa na huyo mnayemwita the so called Mchina. Tuna wataalam wa kutosha, waende wafanye tafiti za kina kule Bagamoyo, tukijenga bandari kama Taifa, tunaenda kupata faida ipi? Je, masharti yaliyowekwa kwa huyo mwekezaji wa mwanzo ambayo mmesema ni magumu, tuyachambue tuone masharti ambayo ni rahisi, tunapotangaza tenda sisi ndio tunashikilia ni yupi mwekezaji ambaye anakuja na tija akiwekeza hapa kama Taifa tutanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinyume cha hapo, una mamlaka na Bunge lako hili. Kama mikataba ipo, kuna Kamati Maalum ya Miundombinu, unaweza ukai-task ikaenda kufanya kwa niaba ya Taifa letu kuona kama huo mradi ni viable kwa Taifa au la.

Mheshimiwa Spika, kwa hayo machache, naomba kuwasilisha. (Makofi)