Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Mpango huu wa Tatu wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichangie maeneo machache; eneo la kwanza ni sekta binafsi kwa ujumla. Ni ukweli usiopingika kwamba kwa kweli kama tunataka kufanya uchumi ukue sekta binafsi haikwepeki. Sekta binafsi ni muhimu, kwa hiyo, tuiwezeshe ili iweze kusaidia kwenye kukuza uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachojitokeza kwa kiasi kikubwa sana kwa miaka hii ya karibuni, nachelea kusema kwamba sekta binafsi imeingia katika challenge kubwa sana na kwa kiasi kikubwa tumesikia kwamba baadhi ya wawekezaji katika sekta binafsi na hapa tunaongelea ngazi mbalimbali hatuongelei wakubwa peke yao, tunaongelea wakubwa wa kati na wadogo wamefika mahali wamekatishwa tamaa na baadhi yao wamefunga biashara au wamekaa pembeni wakiangalia kitachoendelea kama watazamaji. Hii haina afya kwa uchumi wetu na haina afya kwa mpango wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri jambo hili limeshapewa mwelekeo na Serikali. Nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kutoa kauli ambayo imetoa mwanga mpya kwa nchi yetu. Mkubwa akishasema watendaji tunatakiwa tuwe tumeshaelewa, this is the tone from the top. Kwa hiyo, tunatakiwa sasa watendaji wajipange wakijua mwelekeo wa nchi yetu inavyoiangalia sekta binafsi ni tofauti na ilivyokuwa miaka ya jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhusishwaji wa sekta binafsi uko katika maeneo mengi, uko katika ngazi ya sera lakini uko katika ngazi ya mambo ya kikodi. Sekta binafsi ina vyombo ambavyo ndivyo maalum kwa ajili ya kufanya dialog na Serikali. Vyombo hivyo vipo, kazi imekuwa ikifanyika lakini wote tunafahamu mwisho wa siku challenges ambazo sekta binafsi inazipata wengi tunaambiwa hapa zimefikia mahali ambapo wote tunangoja kitu kinaitwa blue print mkakati ambao ndiyo unaenda kujaribu kushughulikia masuala mengi ambayo dada yangu pale Jesca amezungumzia, ametamka neno pale nisingependa kulirudia lakini urasimu ambao ndiyo upo umeonyesha kwa kiasi kikubwa unaua sekta binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nitoe tu angalizo hii blue print inayoongelewa ni karatasi tu tunahitaji kuwa na mindset change kwa viongozi wa Serikali. Tunahitaji kuwa na mindset change katika taasisi mbalimbali zinazosimamia mambo yote ya kiuchumi kuanzia Benki Kuu, TRA na vyombo vyote vya udhibiti kwa maana ya regulators. Hawa watu wasipobadilisha mindset ya kuiona sekta binafsi kama engine ya kusaidia kukuza uchumi tutakuwa tunatwanga maji kwenye kinu, hatutapata matokeo tunayoyakusudia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushirikishwaji wa sekta binafsi ni pamoja na kuifanya sekta binafsi ishiriki kwenye uchumi. Serikali ndiyo mtumiaji mkubwa wa rasilimali fedha ambazo mwisho wa siku zinaishia kwenye mikono ya Watanzania kwa kupitia shughuli zao mbalimbali. Tulichokiona ambacho mimi naamini kinadumisha uchumi wetu ni Serikali kuona kwamba inaweza ikafanya mambo mengine mengi yenyewe ya kibiashara. Tumeona Serikali wakati mwingine inajenga yenyewe, tumeona maeneo ambayo hata kazi za kawaida ndogo ndogo taasisi za kibiashara za umma ndiyo zinapewa zifanye kazi hizo, hii haisaidii kuinua uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumetunga sheria hapa za local content ambazo zinatakiwa zisaidie Watanzania ili waweze kushiriki kwenye uchumi. Napenda kusema sheria hizi zitabakia kuwa makaratasi tu kama Serikali yenyewe haitakuwa na initiative ya kuhakikisha mambo haya yanatokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee eneo lingine la kilimo. Ndugu yangu pale ameshaongelea eneo la kilimo na maeneo ambayo ameyaongea mimi sitaongelea lakini ni ukweli usiopingika kwamba bado sekta ya kilimo itabakia kuwa ndiyo sekta kiongozi ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa kupeleka mbele uchumi wa nchi yetu. Sekta hii tunafahamu ina matatizo mengi na makubwa, inahitaji vichocheo vya kila aina na kikubwa kuliko vyote ni miundombinu wezeshi. Tumeshaongea kwa kiasi kikubwa hapa sitapenda kulirudia lakini kwa kweli tukubaliane kwa wakulima hasa wa mazao fulani fulani mkakati kama tutaendelea kutokuwa na utaratibu wa kuwa na umwagiliaji wa mazao yetu, nina uhakika sekta ya kilimo bado itaendelea kubakia nyuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuangalia Mpango ulivyoandikwa unaona bado umwagiliaji ni chini ya 20%. Mazao kama chai ambalo ni zao kubwa sana maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, ili uweze kupata mavuno hasa unahitaji kuwa na miundombinu ya umwagiliaji. Kuna makampuni makubwa yanafanya uzalishaji wa chai lakini makampuni hayo sisi tunasema yana mchango wake tunahitaji kwenda sasa kuwa na wakulima wadogo wadogo wa chai walio wengi ambao watatoa mchango wa moja kwa moja katika sekta ya chai.

Mheshimiwa Naibu Spika, tujifunze kwa waliofanikiwa ukienda Bangladesh, sisi tuna viwanda 21 vya chai lakini Bangaladesh wana viwanda vidogo vidogo vya chai 700. Wao Serikali imechukua jukumu kubwa la kuhakikisha hili linatokea kwa sababu chai inaajiri watu wengi sana katika uchumi hivyo una uhakika wa kupata kodi nyingi katika uchumi wako. Siyo hilo tu unasaidia kuinua maisha ya watu na hii inaendana na dhana nzima ya uchumi shindani na viwanda kwa ajili ya maendeleo ya watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme moja ambalo limekuwa ni kikwazo kwa sekta ya chai. Chai ni zao la mkakati na la export lakini ukiangalia kuna tatizo kubwa sana la VAT. Kinachojionyesha ni wazi kabisa kwamba urejeshaji wa VAT katika maeneo mengi ya mazao ambayo yanapelekwa nje ya nchi umekuwa ni hafifu sana. Hii inawaondolea wawekezaji na wafanyabiashara mbalimbali uwezo wa kuweza kuwa na mtaji wa kuendeleza biashara zao na hiyo inaondoa na inapunguza ulipaji wao wa kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee kwa kifupi madini. Eneo la madini tumeona na tumeshuhudia mafanikio makubwa lakini naomba niseme wazi kwamba kama ambavyo Prof. Muhongo alituambia asubuhi na mimi nikazie tusijidanganye, tusipime success ya sekta hii kwa kuangalia mapato ambayo tumeyapata mpaka leo kwani hayatokani na kuongezeka kwa uzalishaji. Inawezekana kuna ongezeko la uzalishaji lakini sehemu kubwa ya ongezeko hilo limetokana na kazi nzuri ya Serikali ya kuzuia utoroshaji hasa uliokuwa unafanyika kwa kutumia njia za panya. Kwa hiyo, inaonekana kama kuna ongezeko lakini kwa kweli uzalishaji haujaongezeka, hakuna migodi mipya mikubwa iliyojitokeza au iliyojengwa katika miaka mitano mpaka sita toka tumebadili sheria zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, inabidi tuwe makini kwa sababu tunapoangalia Mpango tuangalie na threats za wapi tunaweza tukashindwa kuendelea. Mimi naliona hili bei ya dhahabu siku zote huwa inakwenda juu na chini, wakubwa wameshaanza kukaa na tunaweza tukaona hali ya stability katika ulimwengu ambayo itasababisha bei ya dhahabu pengine, hatuombei, ianze kwenda chini na mara moja tutapata impact kubwa negative kwenye Mpango wetu, hili tulielewe na tulitilie maanani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tufanyeje sasa? Tufanye yale ambayo tumeshayasikia, twende kwenye maeneo ya madini mengine ambayo ni muhimu na tusichelee kuona kwamba Liganga na Mchuchuma ni eneo ambalo hatuna sababu kwa nini mpaka leo hatujaweza kuanza kuzalisha pale mawe pamoja na chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kama hiyo ni kengele ya pili. (Makofi)