Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

hon Hassan Seleman Mtenga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtwara Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuweza kuchangia Mpango wa Tatu wa Miaka Mitano. Pili, nimpongeze Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha kwa kutuletea Mpango ambao umekaa vizuri sana. Nina mambo ambayo nitayachangia kwenye maeneo zaidi ya matatu hasa tukianza kwenye miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama tunahitaji tuvuke na tupambane kuondoka kwenye umaskini kuingia kwenye suala zima la kimaendeleo hasa kwenye uchumi mkubwa tunapozungumza miundombinu hasa kwenye maunganisho ya nchi yetu Kusini mwa Tanzania, kule Mtwara, naishukuru sana Serikali kwa kutujengea daraja la Mtambaswala. Nataka nitoe angalizo, daraja hili limetengenezwa kwa gharama kubwa sana, lakini kwenye utengenezaji wake na matumizi ni tofauti.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nieleze uhalisia kutoka Mtwara kuelekea Masasi kuna kilometa zaidi ya 230, lakini kutoka Masasi kuelekea kwenye daraja la Mtambaswala kuna kilometa 130 lakini kutoka Mtambaswala kwenda border kuna kilometa 75. Ukitoka border kuelekea Beira Nampura pana kilometa zaidi ya 788. Hoja ni vipi? Ukitoka Mtwara kuelekea Ruvuma pana kilometa 70, kutoka Ruvuma Mpakani unaelekea Msimbwa Naplaya mpaka Nampura unatumia kilometa 445. Kama tungejenga daraja hili kupitia pale Mto Ruvuma tungeweza kufungua mawasiliano kati ya Msumbiji na Tanzania na Afrika Kusini kupitia Msumbiji kuja Tanzania. Sasa hivi wenzetu Afrika Kusini wakitaka kwenda kuuza magari wanapitia Zambia ambapo wanatumia zaidi ya kilometa 2,800 kuja Tanzania. Kwa hiyo nataka niseme hapa hapahitaji watu wenye degree wala maprofesa, ni suala la uamuzi sasa kwa Waziri mwenye dhamana alishughulikie hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka nimpongeze mdogo wangu Mheshimiwa Bashe. Mimi nasema Bashe ana akili kubwa sana. Pia nataka nishauri, kule kwetu Mtwara liko eneo moja linaitwa Kitele. Toka nazaliwa napata umri mpaka leo naingia uzeeni, liko eneo linamwaga maji chemchem, maji ya kutosha sana na eneo lile wakazi wa pale wanalima mpunga. Kwa kuwa mpunga ule unalimwa tofauti na viwango, hatuna scheme za umwagiliaji mpunga ule ni mzuri sana, lakini haukidhi mahitaji ya kibiashara. Sasa naiomba Wizara yenye dhamana, twende pale wakaangalie wajiwekeze ili tuweze sasa kuleta kilimo cha kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mpango nimeangalia kwenye suala la elimu. Kwanza niipongeze Serikali, imeweza kuwekeza kwenye mfumo wa elimu bila malipo tukisema elimu bure, hongera sana kwa Serikali yetu. Hata hivyo, bado kuna tatizo, shule za msingi katika kila pato la kichwa cha mwanafunzi tunapeleka shilingi 6,000, lakini kwenye shule za sekondari kila kichwa cha mwanafunzi tunapeleka shilingi 10,000, lakini fedha hizo tayari Wizara zinapeleka kukiwa na mgawanyiko wa matumizi. Utawala wana asilimia 10 kwenye fedha hiyo, michezo kuna asilimia 20 inagawanyika kwenye fedha hiyo, mitihani kuna asilimia 20 kwenye fedha hiyo, ukarabati kuna asilimia 20 kwenye fedha hiyo, vifaa kuna asilimia 30 kwenye fedha hiyo. Niombe fedha hii ni ndogo mno na fedha hii inasababisha sasa hivi Walimu wetu kufanya njia mbadala ya kuwafaulisha watoto ilimradi tu wasionekane kwamba wao hawana mafunzo kwenye zile shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, shule nyingi zimekuwa sasa wazazi wakiwa wanachangia, lakini kwenye uchangiaji wazazi wamefika mahali wanagoma. Wanasema Serikali inaleta fedha nyingi sana kwa sababu mnyumbulisho huu wazazi hawauelewi. Kwa hiyo niiombe Wizara yenye dhamana twende tujiwekeze sasa kwenye Sekta hii ya Elimu, kama tumekubali sasa Serikali kubeba mzigo wa elimu bila malipo basi twendeni sasa tuongeze ruzuku hii ambayo inapatikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nataka niguse kwenye suala la viwanda. Kusini tuna Kiwanda kikubwa sana cha Saruji cha Dangote. Kiwanda hiki kina wafanyakazi zaidi ya 6,000. Kimetoa ajira ya kutosha, lakini kiwanda hiki kinashindwa ku-move kwa sababu ya kodi za TRA. hHpa karibuni mlikuwa mnasikia kwamba Kiwanda cha Dangote kinataka kufungwa, lakini Kiwanda cha Dangote wamefika mahali sasa wamechoka wanataka kuondoka. Kwa mfuko wa saruji mmoja TRA wanachukua shilingi 3,000, mfuko unaouzwa shilingi 11,000 kwa bei ya jumla. Ukienda ndani ya kiwanda kile, maintenance ya kiwanda, mkanda mmoja unavyokatika wa mashine unatumia zaidi ya milioni 180 kuagiza mkanda mmoja wa mashine. Twendeni sasa tuangalie kama tunahitaji kuboresha uchumi huu wa Tanzania lazima tufike mahali sasa viwanda vyetu tuvisaidie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna wawekezaji, kila tunapozungumza, sasa hivi nimeshazungumza na wawekezaji zaidi ya sita kutoka nje (investors) lakini wanasema kwamba Mtenga, hili suala kwenu haliwezekani. Ukitaka kufungua kiwanda, kuwa mwekezaji, shughuli yake ni kubwa mno. Mle kuna watu wapo zaidi ya nane au tisa, ukitaka kiwanda unamkuta NEMC, ukienda hapo NEMC mambo ya NEMC Mwenyezi Mungu mwenyewe anayafahamu. Pia kuna mtu anaitwa TBS, ndani ya kiwanda hicho hicho kimoja. Yuko mtu mmoja anaitwa TRA, lakini kuna janga kubwa la Kitaifa linaitwa NIDA, leo mwekezaji ametoka nje kadi ya NIDA anaipata wapi hapa Tanzania? Hili lazima tuliangalie, lakini kuna mtu anaitwa OSHA, pia mtu mwingine anaitwa Zimamoto. Vile vile Kuna kibali cha kuishi, hili nalo ni shughuli nyingine. Vibali vya kuishi leo kama kuna wawekezaji ambao tayari wana wafanyakazi wao wako wanafanya kazi, kwenda ku-renew kibali tu cha miaka miwili au mwaka mmoja wanachukua takriban zaidi ya miezi nane au tisa. Hebu tufike mahali kama kweli tunahitaji sasa, tufike mahali tubadilike ili tuingie kwenye uchumi mkubwa sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nishauri hawa OSHA, NIDA na kadhalika kwenye Sekta hii ya Uwekezaji hebu wakae sehemu moja ili shughuli ile iwezekane kupatikana. Yuko hapa mtu mmoja anaitwa Mkurugenzi wa NEMC, yaani afadhali leo unaweza kumtafuta Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukampata kuliko Mkurugenzi wa NEMC. Tunakwenda wapi? Leo tunazungumza kwamba nchi yetu tunataka iwe nchi ya uchumi, lakini uchumi wetu tunazungumza viwanda, ni kitu ambacho hakiwezekani. Ukiangalia kwenye viwanda vyetu, wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwenye viwanda hivyo, mishahara yao wanayolipwa ni midogo. Serikali kama Serikali wanasema kuna viwango vya kima cha chini vimepangwa, sasa viwango vinavyopangwa vya kima cha chini tuangalie na kodi tunazowatoza wale watu na service za viwanda vyao wanavyofanya ili tufike mamlaka ya kuwabana wale juu ya mishahara yao ambao inalipwa.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Kengele ya pili imeshagonga.

MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimeshamaliza? Loh, naunga mkono hoja. (Makofi)