Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Jesca Jonathani Msambatavangu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Iringa Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mimi nitaongelea jambo moja tu kuhusiana na urasimu katika utekelezaji wa Mpango huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba nitoe mfano mmoja ambao uliwahi kutokea hapa kwetu, inaweza kuwa siyo hadithi nzuri sana, lakini itatusaidia kukumbuka. Kuna wakati fulani ilitokea hadithi ya mafuta ya upako; yalimwagwa kwenye carpet na watu wakapita wakiwa na malengo ya kupona pale, huzuni zitabaki pale, wakiwa na malengo kwamba kama waliingia na mawazo, yataisha pale na kwamba wataondoka hawana stress. Sasa basi, Mpango huu naufananisha kama mafuta ya upako, kumbe ndani ya yale mafuta ya upako kulikuwa kuna utelezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya watu kutoka wamepona pale, wakawa wanakatana mitama mle, wanalaliana, wanakanyagana, wengine wakatoka wamekufa, tukapata majeruhi na wengine ambao walikuwa mahututi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mpango ni mzuri na mambo yamekaa vizuri. Wasiwasi mkubwa ni urasimu ambao hauna maana katika utekelezaji wa Mpango. Lazima tukubaliane sasa kama tunakwenda kama nchi, tushirikiane mihimili yetu yote mitatu, Wizara zetu zote, pamoja na Idara zetu zote, tushirikiane na vyombo. Kwa sababu kuna wakati fulani tunaweka mipango mizuri lakini unaweza kukuta kuna mahali tunaweka vitu ambavyo vinasababisha tusiende mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tumeongea kwenye Mpango kwamba tuna miradi ya kimkakati. Miradi hii mingine imeanza siku nyingi, bado inahitaji gharama ndogo sana. Sasa kwa sababu ya urasimu usiokuwa na maana, utakuta kuna vikwazo vinatokea tu ama kutoka katika Idara moja ama kutoka katika Idara nyingine au kutoka katika Wizara fulani au kutoka katika chombo fulani tunakuwa hatuendi mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna miradi kwa mfano ya utalii, tayari tuna capital kule kwa sababu tayari tuna Wanyama, tuna Mbuga za Wanyama, tuna kila kitu. Kuna miundombinu tu kuielekeza kufika kule kwenye utalii ili sisi tuanze kukamua dola, kunaanza kutokea urasimu usiokuwa na maana. Halafu wakati mwingine ku-connect sasa; tumeboresha viwanja vya ndege, tumenunua ndege, zinafika kwenye viwanja vya ndege. Kutoka pale kwenye kiwanja cha ndege kufika kwenye Mbuga ya Wanyama hapaingiliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa huu ndiyo tunasema utelezi kwenye upako. Utelezi ndani ya Mpango, kwa nini sasa? Hii miradi ya kimkakati kama ya utalii ambayo inaweza ikatengenezewa tu miundombinu na tukaanza kupata fedha, isitolewe hiyo fedha tukafanya mambo haya na tukatekeleza ili tuanze kukamua hela huku wakati huo huo tukiboresha huduma zetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna Wizara ya Viwanda na Biashara, tuna Wizara ya Vijana na Ajira, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha kwamba wanatengeneza ajira kwa vijana wetu. Tuna Wizara zinafanya juhudi kubwa au Idara zinafanya juhudi kubwa kuua vyanzo hivyo vya ajira. Ndiyo maana hapa unakuta Waheshimiwa Wabunge tunakuja kulalamika, ni kwa nini bodaboda zijae kwenye Vituo vya Polisi na vijana wetu wakati wamejiajiri na tumeruhusu kama sehemu ya ajira? Huo ndiyo unakuwa utelezi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, tumekubaliana kwamba tunavutia wawekezaji kwenye Taifa hili. Tuna Wizara ya Uwekezaji kwenye nchi yetu, tulikuwa na TIC wakati ule inavutia wawekezaji kwa kuweka mazingira mazuri. Kuna Idara nyingine wanapofika ndani ya hii nchi, wanazuiliwa vibali, wanaanza kuwekewa urasimu wa vibali kibao, sijui kodi, vitu kama hivyo. Huo ndiyo utelezi sasa kwenye Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka uchumi shindanishi kikanda na Kimataifa. Leo hii tunataka Watanzania wakauze bidhaa kwenye Soko la Afrika Mashariki, Soko la SADC na Soko la AGOA. Rudi sasa kwenye utelezi; namna ya kupata Passport, namna ya kupata Hati tu ya Uraia, namna ya kupata cheti cha TBS, utelezi! Kina Mama wanatengeneza products zao, kuwekewa tu alama ya TBS kuna milolongo mirefu, akina mama wanashindwa kwenda mbele, tunashindwa kufanya biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mwingine tunadanganyana humu. Unapofuatilia kibali kwa ajili ya wawekezaji au kuleta wawekezaji, utasikia kuna vyombo, kuna vyombo, kuna vyombo; sasa sijui ni bakuli, sijui ni thermos, sijui ni chupa! Vinazuia! Hapa vyombo vinafanya utafiti, uongo mtupu! Tunadanganyana, tunaweka utelezi kwenye Mpango. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii tuna miradi mikubwa ya umeme hapa imeanzishwa, kama Julius Nyerere Stiegler’s Gorge. Ule ni mradi ambao utatusaidia. Wapo Watanzania wanaubeza, zipo Idara nyingine ni utelezi. Wapo Watanzania wengine hawaoni umuhimu. Mradi ule utatuongezea nguvu ya umeme, utatupunguzia production costs, utasababisha bidhaa zetu kushuka bei. Hivyo utasababisha nasi tuweze ku- compete kwenye soko la East Africa na Kikanda. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi ule ukiwekwa maji pale, umeshatengewa tena hekta zaidi ya 150,000 kwa ajili ya irrigation scheme unakwenda kwenye ile irrigation, utakutana na watu wa bonde. Utelezi hutuzuia sasa tushindwe kufanya irrigation schemes. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuna vitu ambavyo nasema kama hatutashughulika na utelezi kwenye mafuta ya upako, tutaondoka tumekufa, tutaondoka majeruhi. Lazima Serikali yenyewe ijipange. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nilikuwa nasoma taarifa ya CAG, anaongelea kuhusu kukusanya mapato na TRA jinsi ilivyokusanya, lakini moja ya mapendekezo ya CAG, aliwapa mapendekezo kama 338; ni asilimia 19 tu wameyafanyia kazi, mapendekezo 266 wameshindwa kuyafanyia kazi. Asilimia 38 ya mapendekezo 266 ni kwa sababu yako Idara nyingine, kwa hiyo, yameshindwa kutatuliwa, Idara nyingine imeleta utelezi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ndugu zangu kama hatutaangalia haya na kuangalia urasimu tuliouweka ambao unatukata mtama wenyewe kwenye upako, hatuwezi kufika mbali. Lazima sasa Serikali iamue kwa nia ya dhati kuondoa urasimu usiokuwa na maana. Kama tumeamua tunajenga ajira kwa vijana wetu, walindwe; machinga walindwe; bodaboda walindwe; na mama ntilie walindwe. Wale hawajaenda shule lakini tuna wasomi, Maafisa Biashara wetu, siyo kazi yao kuingia kuwasumbua wale, ni kwenda kuwaelimisha wafuate taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo kazi ya Jeshi la Polisi tu kukamata bodaboda peke yake, ni kutoa na elimu. TRA leo ni chombo kinachokusanya mapato, siyo kazi yao kuwa innovator wa kesi kwenye nchi hii. Zipo kesi za biashara kwenye Mahakama ya Rufani 1,097 ambazo ziko created na TRA, wamehama kwenye lengo lao la msingi, wamehamia kwenye ku-create kesi. TRA wana kitengo cha kutoa elimu kwa wafanyabiashara, watoe elimu kwa wafanyabiashara na sio kuwavizia wafanyabiashara wamekosea ili wao wapate mazingira ya kuwashtaki. Kwa hiyo lazima tuondoe utelezi na urasimu usiokuwa na maana, twende tukatekeleze hii miradi ya kimkakati. Tujenge barabara kwenda kwenye National Parks zetu. Kwa mfano sisi tuna barabara ya kutoka Iringa - Ruaha National Park, ni park ambayo ni ya pili kwa ukubwa duniani. Ina tembo wakubwa kuliko National Park yoyote lakini miaka yote barabara iko kwenye Ilani lakini haitekelezeki mahali ambako tungekwenda kuchukua dollar bure. Unaona watu wanaingia Serengeti wanakwama kule ndani, wakati vitu tayari viko pale. Tuache, twende tukaamue sasa kufanya kazi kwa ajili ya ku-implement Mpango huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo tutakwenda vizuri. Tukiangalia hawa watu wa chini, ameongea Mheshimiwa Mbunge mmoja kama tukiangalia hii micro enterprise ya wafanyabiashara wadogo tukaielimisha, leo tunaongelea ujuzi, kutoa elimu ya ujasiriamali. Tuna mkakati gani wa kuwapa hiyo elimu? Tunawapa mafunzo ya ujasiriamali kwa mtindo gani? Au tumeweka tu tunatengeneza mifuko ya wajasiriamali, sijui ya wafanyabiashara wadogo wadogo, hiyo mifuko inaishia juu. Kuna mmoja amesema hapa kuna Benki ya Kilimo ina majengo mazuri Dar es Salaam, Dar es Salaam kuna kilimo gani? Haya ndiyo mambo ya utelezi, yaani vitu ambavyo watu wanatengeneza dili ambazo hazieleweki! Twende kwenye grassroot tukatatue matatizo ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunaongelea akinamama wajengewe vituo vya afya, zahanati na hospitali, huduma za uzazi ziwe bure, wewe unakaa unazuia fedha ya matibabu kwa akinamama wasitibiwe, una hila gani? Utelezi huu. Sisi tunataka kuongeza wapigakura kwenye nchi hii, tunataka kuongeza raia bora kwenye nchi hii, wazaliwe watoto bora kwenye nchi hii, unazuia fedha bila sababu, huo ni utelezi. Tunataka sasa urasimu na Wizara zijione kama kila Wizara ina heshima, maana ipo ile kuona kwamba labda Wizara hii kwa sababu sisi ni Fedha, basi ni wa muhimu sana, samahani kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu, wewe ni rafiki yangu sana. Labda wewe ndiyo wa maana zaidi kuliko yule Waziri wa Wizara ya Kilimo au Waziri yeyote, hapana! Kwa sababu ili Waziri wa Fedha awe na fedha, ni lazima kilimo kichangie mapato, ili awe na fedha, lazima bodaboda wachangie, ili awe na fedha, lazima mama ntilie wachangie. Leo hii tuna vitu vya ajabu, tunatakiwa kuangalia mambo ya utelezi, urasimu wa kijinga. Kwa nini tusifikirie Watanzania wetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele ya pili imegonga Mheshimiwa…

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: … wanaofanya vizuri tukawatumia sisi wanaanza kuonekana kutumika kwanza Afrika Kusini.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. JESCA J. MSAMBATAVANGU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja lakini utelezi uondolewe. (Makofi)