Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi. Nami nianze kwanza kwa kuwapongeza Mawaziri na Naibu Waziri wote waliochaguliwa ama walioteuliwa katika awamu hii ya Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo mawili matatu, lakini naomba nianze na hili la viwanda na hapa naomba Waziri wetu wa Fedha anisikilize kwa makini kwa sababu kwanza yeye ni kijana mwenzangu lakini ni mtu ambaye amekabidhiwa jukumu la kwenda kukomboa uchumi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwenye eneo la viwanda ndugu zangu wabobezi katika mausala ya uchumi watanisaidia lakini katika pitapita zangu, uchumi wa viwanda, nchi iliyoendelea kiviwanda inatakiwa iwe na sifa kuu chache. Kwanza, tunatakiwa tu-export manufactured goods. Pili, tunatakiwa tu-import raw materials, tu-import malighafi kutoka nje kuja kulisha viwanda vyetu huku nchini lakini tuingize teknolojia. tukirudi kwenye uhalisia wa uchumi wetu Tanzania hii kitu inaenda kinyume, yaani kichwa chini miguu juu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mazingira haya, kweli tunaweza kufikia ule uchumi tunaosema wa viwanda? Juzi tu hapa, tena sio juzi na hilo tatizo liko hivi sasa, mahindi ya Tanzania yamezuiliwa pale mpakani Kenya. Mimi nilifikiri kama tungekuwa smart Watanzania tungefurahi suala lile, tunatakiwa sisi tupeleke kule nje unga siyo kupeleka malighafi. Tunatakiwa sisi tu-export manufactured goods, sisi tuzalishe, tu-process tuhakikishe tunalisha viwanda vyetu hapa nchini, kule tupeleke bidhaa zilizotengenezwa tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Kanda ya Ziwa wanalalamika hapa kila siku, pamba, pamba, ngozi kwa nini tunatoa malighafi hivi kwenda kuwakuzia wenzetu uchumi wakati sisi wenyewe tunahitaji bidhaa hizi kwa ajili ya viwanda vyetu vya ndani? Ninatarajia katika Mpango huu tunaozungumza hivi sasa, Mawziri wetu, Waziri wa Viwanda, Waziri wa Fedha, Waziri wa Biashara na Uwekezaji mtutoa hapa tulipo twende hatua inayofuata kwa kuhakikisha bidhaa na mazao tunayozalisha humu ndani, tunaya-process wenyewe, tunapeleka nje bidhaa zilizokwishatengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasikia tuna viwanda vya viatu vya ngozi hapa nchini, lakini nashangaa tunafurahia kweli kuvaa viatu vya China. Hatuwatendei haki wakulima wetu na wazalishaji wetu wa ndani kuhakikisha kile tunachowahubiria kila siku zalisheni, kweli wanazalisha lakini kwenye eneo la finishing tunashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mtaalam mbobezi wa uchumi, leo tunasema upele umepata mkunaji, basi kamalize kazi ndugu yangu tunategemea matokeo makubwa sasa. Tuwasaidie vijana wetu basi na wao wapate ajira kupitia sekta zetu za viwanda. Serikali haiwezi kuajiri ikawamaliza Watanzania wote, sasa hivi vijana wako mtaani wanasubiri ajira, utawaajiri wapi? Lazima tuanzishe viwanda vya kimkakati, lazima tuhakikishe raw materials zilizopo nchini zinafaidisha Watanzania hasa kwenda kwenye viwanda vya kwetu humu ndani sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini bado kwenye eneo la kilimo mashaka bado ni makubwa. Nizungumzie tu maeneo machache ambayo nina uzoefu nayo katika Jimbo langu la Singida Kaskazini. Sisi ndiyo wazazlishaji wakubwa sana wa alizeti, haya mafuta mnayokula hapa yametoka Singida Kaskazini mimi ndiyo nazalisha kule pamoja ndugu zangu. Gunia la alizeti iliyozalishwa limefungwa vizuri la kilo 100 ni Sh.40,000 mpaka Sh.50,000 lakini mbegu ni Sh.60,000 au Sh.70,000, tutamkomboa lini huyu mkulima? Tuleteeni pembejeo, mbegu na ziuzwe kwa bei affordable kwa kila Mtanzania. Hata hizi kelele tunazopiga kwenye viwanda watu watazalisha tupapeleka viwandani. Sasa hivi ndugu zangu kule Singida Kaskazini wameiacha alizeti kwa sababu bei ya mbegu ni kubwa, tu- subsidize mbegu, pembejeo ili wakulima waweze ku-afford kwa kiwango tunachofahamu cha hali za wananchi wetu kule vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine la tatu ambalo linaendana sasa na haya masuala viwanda na kilimo ni lazima miundombinu iwe mizuri kwenye eneo la kuzalisha mpaka processing kama ni viwanda. Tulizungumza sana barabara zetu sasa hivi mvua zimenyesha zimeharibu kwelikweli barabara hazipitiki. Sidhani kama kuna Waziri hapa anayetokea Dar es Salaam maeneo ya Magogoni pale, wengi mnatoka vijijini kama ninakotoka mimi, mnafahamu hali halisi ya mazingira ya mwananchi wa Tanzania, tutengenezeeni miundombinu ya barabara za vijijini hata hizi zinazounganisha mkoa na mkoa na wilaya na wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo barabara moja kubwa pale inayotoka Singida Mjini kwenda Haydom, ile ndiyo roho ya uchumi wa Singida Kaskazini. Barabara hii ni ahadi ya viongozi wa kitaifa kuanzia Rais Mstaafu Hayati Mheshimiwa Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Hayati Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Naomba basi, tusiwadhalilishe viongozi hawa, tekelezani hizi ahadi ndugu zangu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ipo barabara inatoka Singida Mjini - Kinyeto – Kinyagigi – Meriya – Maghojo - Sagara nayo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyeko madarakani hivi sasa. Naomba barabara hii nayo itengenezwe kwa kiwango cha lami kwa sababu sisi kwa uzalishaji wetu wa alizeti ninaowaambia hapa ndiyo tunaowalisha kwa mafuta, hatuwezi kuwaletea sokoni kama barabara ni mbovu. Ndiyo tunaozalisha vitunguu kwelikweli lakini hatuwezi kuvikisha sokoni kama barabara ni mbovu. Naomba kwa kupitia Mpango wetu huu wa Maendeleo tuione miundombinu ni kipaumbele na tuhakikishe tunawasaidia wakulima wetu katika eneo lao la uzalishaji.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kwenye utawala bora kidogo…

NAIBU SPIKA: Hiyo ni kengele ya pili Mheshimiwa Ramadhani.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa heshima yako naomba nusu dakika, inanitosha, naomba kuzungumzia suala la maslahi ya Madiwani.

NAIBU SPIKA: Sasa jambo jipya tena hilo Mheshimiwa.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)