Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Mpango huu wa Maendeleo katika bajeti yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya kuchangia yapo mengi katika hotuba iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri lakini nitachangia zaidi tutakapoingia kwenye maeneo ya kisekta, leo nitachangia katika maeneo machache.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisije nikachelewa, nianze kwa kuunga mkono hoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa leo nitazungumzia sana maslahi ya watumishi. Nchi hii ina watumishi katika maeneo mbalimbali; wapo wakulima, walimu, madaktari na kadhalika. Hawa wanastahili zao; wanastahili kupandishwa madaraja kwa wakati, wanastahili kwenda likizo, wanastahili kwenda masomoni lakini wapo wengine ambao wanastahili kupata malipo kutokana na kazi wanazofanya kwa muda wa ziada. Kwa bahati mbaya stahili hizi hazipatikani kwa wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuwezi tukasema kwamba bajeti yetu ipo salama bila kuzingatia hilo. Tunapokwenda kukamilisha Mpango huu, wapo watumishi ambao wananung’unika, wapo ambao hawapandishwi madaraja lakini wapo ambao hawalipwi, niombe sana zitengwe fedha maalum kwa ajili ya wale ambao wanastahili kupandishwa madaraja hii ikiwa ni sambamba na kuwapandisha madaraja kwa wakati na walipwe stahili zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nitazungumzia ni miundombinu. Ipo miundombinu ya barabara, reli na kadhalika. Katika hili nitazungumzia miundombinu ya barabara.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi natoka Mkoa wa Kigoma, lakini katika taarifa iliyotolewa ndiyo mkoa pekee ukiunganishwa na Mkoa wa Katavi haujaunganishwa katika mpango wa barabara kwa maana kwamba kufika kila mkoa. Niombe sana katika bajeti inayokwenda kukamilishwa sasa, mkoa wetu uweze kuunganishwa kwa barabara ambazo zinatosholeza kuweza kufikia kwenye ngazi ya mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo barabara mfano inayotoka Mpanda – Mishamo - Uvinza – Kigoma; Tabora – Kaliua - Uvinza – Kigoma; na Mpanda – Inyonga – Koga - Ipole - Tabora. Niombe sana, barabara hizi zikamilishwe ili wananchi wa maeneo hayo kwa Mikoa ya Tabora, Katavi, Kigoma nao waweze kufurahia uhuru wa nchi yao kwa kupata barabara na kuweza kusafiri bila shida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Mkoa wa Kigoma ipo barabara ambayo inatoka Kabingo – Kakonko – Kibondo - - Kasulu - Manyovu – Buhigwe anakotoka Makamu wa Rais. Barabara hii imetengewa fedha sasa huu ni mwaka wa tatu, hawa ambao wanasema ni wajenzi wa barabara kasi yao ni ndogo. Niombe Wizara husika ifanye ufuatiliaji wa jumla ili barabara hii iweze kukamilishwa na wananchi waweze kupata huduma muhimu hasa hiyo ambayo nimeitaja ambayo ni barabara. Niombe sana barabara hiyo ikamilike kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika Wilaya ya Kakonko, tunayo barabara ya Kakonko – Ruhuru - Nyakiyobe - Gwarama - Mpaka wa Mhange. Mpaka huu kuna soko ambalo linaunganisha Mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Kakonko na nchi jirani ya Burundi. Pale limejengwa soko kubwa, soko la Kimataifa lakini halina barabara. Niombe barabara hiyo ijengwe kwa maana ya kutuunganisha na wenzetu wa Burundi ili biashara ambayo inastahili kufanyika katika eneo lile ambalo tayari kuna soko iweze kufanyika na iweze kukamilika kwa wakati na kuweza kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii inakwenda sambamba na barabara ya kutokea Gwarama - Nabibuye inakwenda kuunga kwa jirani yangu Mheshimiwa Ndaisaba Wilaya ya Ngara.

Niombe sana barabara hii nayo iweze kukamilishwa. Barabara hizi zikikamilika wananchi wetu watakuwa na uwezo wa kusafirisha bidhaa kutoka vijijini kwenda mjini na kwenda kule ambako soko linapatikana. Hii ni pamoja na barabara ya kutoka Kibondo kwenda mpaka Mabamba.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kilimo, wananchi wetu wengi ni wakulima, hili halina ubishi. Shida inayojitokeza katika eneo hilo ni upatikanaji wa pembejeo, mbolea na matrekta tena kwa wakati. Niombe, kwa kuzingatia kwamba kilimo ni uti wa mgongo, wananchi wetu wengi wanategemea kilimo, pembejeo kwa maana ya mbolea, zipelekwe kwa wananchi wetu mapema ili ziwasaidie katika kuandaa kilimo na kulima vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mazao ya kimkakati, mwenzangu kaka yangu Mheshimiwa Vuma asubuhi alizungumzia masuala ya kilimo cha chikichi kwa upande wa Mkoa wa Kigoma. Nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Mkuu ametumia muda mwingi sana kuja Kigoma kuhamasisha zao la chikichi. Ametumia muda mwingi na amejaribu kwa nguvu zake zote kuhamasisha jamii ile na wananchi wameamka. Niombe sana katika bajeti hii, nguvu kubwa ipelekekwe katika zao hili na hasa ikizingatiwa kwamba zao hili litaleta jibu sahihi katika tatizo ambalo linalotukabili la upatikanaji wa mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naamini kwamba ipo mikoa mbalimbali ambayo inaweza ikalima zao hili. Mkoa wa Kigoma ukiwa mkoa wa kwanza, lakini zao hili linaweza likalimwa vizuri sana katika Mkoa wa Rukwa, Katavi na Tabora. Niwaombe sana Mawaziri hasa Waziri wa Kilimo, tafiti zifanyike, ufuatiliaji ufanyike, pembejeo zipelekwe, wataalam wapelekwe ili kuhakikisha kwamba zao hili linalimwa kwa wingi katika mikoa yetu na ikiwa katika mazingira hayo nina uhakika itatusaidia kumaliza tatizo linalotukabili la upatikanaji wa mafuta katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la chikichi kama ambavyo nimesema, ndilo jibu la tatizo la mafuta katika nchi yetu. Maeneo mengi katika nchi hii, chikichi inaweza ikalimwa. Ipo Wilaya ya Kyela katika Mkoa wa Mbeya zao hili linaweza likakubali, lakini maeneo mengine hata katika Mkoa wa Kagera, niombe tafiti zifanyike kwa ku-support Mkoa wa Kigoma kilimo hiki cha zao la chikichi kifanyike kwa nguvu zote kuhakikisha kwamba kinajibu na kinatuletea matunda katika kuhakikisha kwamba shida kubwa ya mafuta inayotukabili inakwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nahitaji kuchngia ni upande wa madini. Yapo maeneo mbalimbali ambayo yamebainishwa kwamba yana madini ikiwemo Mkoa wa Kigoma, maeneo ya Mkoa wa Njombe kama ambavyo umezungumza maeneo ya Mchuchuma. Hata hivyo, yale maeneo mengine ambayo yamebainishwa bado hakuna tafiti za kutosheleza ambazo zimefanywa. Niombe maeneo yale ambayo yamebainishwa kwamba yana dhahabu, almasi na kadhalika tafiti zifanyike kwa kupeleka wataalam wa kutosha na mwisho kabisa uchimbaji uweze kufanyika kwa ajili ya manufaa ya nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)