Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Flatei Gregory Massay

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mbulu Vijijini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kupata nafasi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nipongeze Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano kuanzia mwaka 2020/2025 ambao umeletwa hapa. Mpango huu nimeusoma vizuri sana, ni mpango mzuri sana, lakini ninayo machache ambayo napenda kuyaelezea katika mpango huo. Ukiangalia mpango uliopita wa pili utaona jinsi ambavyo uchumi ulikuwa unasogea kidogo kidogo, lakini pia uwekezaji katika mpango huu katika eneo letu la kilimo haujawa vizuri sana. Sasa naomba na kushauri kwamba; Dkt. Mwigulu Nchemba umesoma vizuri sana. Ukiangalia sasa wakulima wetu ndio walio wengi, na zaidi ya asilimia 70 ni wakulima. Sasa ni vyema tukaangalia namna gani mpango utawa-favor watu wengi hawa ambao kimsingi uchumi wao unategemea kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia saa hizi kilimo kimekuwa kwa asilimia tatu peke yake. Kwa nini iko hivyo? Ni wazi kwamba mpango uliopita haukwenda vizuri sana katika eneo hili ili ku-favor Watanzania katika suala la kilimo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini? Wizara zote hizi ambazo zipo katika Serikali zinatakiwa ziende zikipangilia kuendana na mpango unaowekwa kwa kila mwaka.

Mheshimwia Naibu Spika, na sasa ukienda kuangalia Tanzania kama nchi hatuko pembeni ya dunia. Ukiangalia sisi bahati nzuri tunapata mvua za misimu na hatuwezi kabisa kulima kupitia mvua hizi kwa sababu kuna wakati unafika mvua zinaisha.

Kwa hiyo nishauri, kwenye Wizara ya Kilimo mkija na bajeti muweke bajeti ambayo itasaidia kujenga mabwawa katika maeneo yote ya nchi hii ambako utaweza kuzuia maji kwa wingi ili basi tukawa na kilimo cha uhakika, na kilimo hiki kikishakuwa cha uhakika maana yake uvunaji wa uhakika unaonekana; pale ambapo mwananchi anaweza kunyeshea mazao yake na akavuna kwa uhakika.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia leo tuna mikopo ya wakulima, unamkopesha mkulima huyu kutoka benki aende akalime, lakini anakwenda kulima kwa kutegemea mvua za masika, mvua zikiisha au zisipofika wakati wake mvua ikawa kidogo maana yake ni kwamba yule mkulima sasa anakutana na kitu kinachoitwa deni, na hilo deni lazima alipe. Lakini kumbe Serikali ikijiandaa vizuri ikaenda kuweka mabwawa katika maeneo yetu kule vijijini wakulima wale wakaweza kunyeshea yale mazao kwa hiyo utakuwa umemsaidia yule mkulima kwanza, atakuwa na uwezo yeye mwenye wa kulima na ataweza kuvuna na kulipa Serikali. Kwa hiyo utakuwa umemuinua mwananchi moja kwa moja kutoka chini katika mazingira ya kujenga mabwawa ya kunyeshea.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo mengi yana maeneo hayo ya kunyeshea lakini si kila mahali. Ukiangalia nchi nyingi za nje zimekopa mambo mengi toka Tanzania. Ukiangalia kilimo cha korosho ukienda Cuba utakuta walichukua mbegu kwetu. Pia ukienda katika suala la mbegu na pembejeo hizi za kilimo imekuwa tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii ukienda kununua mbegu ni ghali; na mbegu zote zinatoka nje ya nchi, mbegu zinazotoka nje ya nchi zinakuwa ghali zikifika kwa wakulima wetu; kwa mfano sasa hivi mbegu zinatoka Kenya. Lakini ebu tujiangalie sisi kama Watanzania, tumeshindwa kweli kuzalisha mbegu nchini? Na kwa nini tusizalishe mbegu nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna Watanzania wengi vijana wameenda shule hawana kazi, tunalia namna ya kuwatafutia ajira, lakini kumbe tunayo ajira. Ajira tuliyonayo ni ipi, ukienda ukawapatia eneo kubwa tu vijana hawa ukawawezesha wakalima mbegu, mbegu hiyo itashuka thamani, na ikishuka thamani ni wazi kwamba wakulima wetu watanunua mbegu katika hali ambayo iko chini. Leo hii mbegu ni ghali, inapotokea mbegu zinakuwa ghali vijana wetu hawawezi kuendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi ya China imeendelea kwa sababu ya wingi wa watu wake, imewapa kazi ya kufanya na kazi hiyo wanayofanya inawaletea kipato katika nchi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niombe kabisa, Mheshimiwa Mwigulu nakumbuka maneno yako ulipokuja kusoma kwa mara fulani bajeti hii hapa ya kwako ulisema hivi; ‘ukitaka mali utaipata shambani’, mwisho wa kunukuu hotuba yako, wakati huo ukiwa Waziri wa Kilimo na Mifugo enzi hizo. Sasa ndugu yangu leo umepewa Wizara hiyo angalia namna gani ya kusaidia kilimo moja kwa moja. Ukifanya hili utakuwa umeisaidia sana Serikali kunyanyua watu wote na kuwa katika kipimo kile cha uchumi wa kati ambao sasa tunakwenda kuinua watu wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wowote ukitaka upande, eneo lolote, katika nchi zozote; na katika nchi zilizoendelea waliangalia swala la miundo mbinu. Miundo mbinu ikishakuwa salama na mizuri maeneo yoyote yale inasaidia uchumi wetu kupanda. Kwa mfano ukienda moja kwa moja katika maeneo ambako uchumi umekwenda juu ni kwa sababu ya miundo mbinu. Tunapogawa rasilimali kupitia mpango huu, tuna hakika tunatakiwa kuangalia. Nimshukuru sana Hayati John Pombe Joseph Magufuli, ameangalia sana miundo mbinu na katika maeneo haya ameunganisha mikoa mingi sana kwa barabara za lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, maeneo yale mambo yameenda vizuri sana. Sasa na kwasababu unajua Mheshimiwa Mwigulu kuna barabara yetu ambayo ingesaidia kuinua uchumi wa Tanzania. Barabara ya Karatu, Mbulu, Hydom, Singida, Sibiti kule mpaka Simiyu na Meatu wamekaa huko. Barabara hiyo ni barabara ya kimaendeleo. Najua resources au rasilimali zetu si kubwa sana, lakini barabara hii ikifunguliwa na mpango huu ukajielekeza hapo, ni wazi kwamba utakuwa umeinua sehemu hii ya uchumi wa nchi yetu kama Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Fedha nikuombe sana mpango huu unaonekana namna hii, na jimboni kwako kumbuka ni kule. Kuna mtu mmoja alisema hapa hutarudi, mimi nikuombee 2025 urudi, lakini kwa masharti haya. Mpango huu uelekeze moja kwa moja kwenye barabara hii ninayoisema ambayo inapita jimboni mwako. Na bahati nzuri Mungu alivyokubariki…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Flatey Masey, kwani anakuja kugombea…

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ina…

NAIBU SPIKA:… Maana umesema barabara hii ikitengenezwa ndio atarudi atakuja kugombea kwako kwa hiyo wewe hutarudi?

MHE. FLATE G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Barabara hii inapita jimboni kwangu, halafu inakwenda jimboni kwake. Kwa maana hiyo basi barabara hii asipoiangalia isipopita wananchi watajua Flatey Massey Mbunge wa Mbulu Mjini kaisema barabara hii na Mwigulu Lameck Nchemba yeye ni Waziri katika Wizara hii na katika mpango uliopita barabara ilikuwepo haijatengewa fedha, sasa hivi amekuwa Waziri wa Fedha ataiwekea fedha; na kwa bahati nzuri wamewekwa pamoja. Waziri naibu wake anaitwa Masauni hawa wote ni vijana mwingine yuko yanga mwingine yuko simba unaona hiyo! Mwingine yuko bara mwingine yuko visiwani unaona hiyo! Hawa wote ni vijana. Sasa itakuwa hatari kama mpango huu hautakuja kwenye bajeti ikiwa na fedha katika barabara hii ambayo nimetaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hiyo inapita kwenye majimbo tisa. Jimbo la Karatu, Mbulu Mjini, Mbulu Vijijini, Iramba kwake mwenyewe, inaenda Meatu, inakuja Sibiti inakutana mpaka Lalago kule, mpaka Maswa, Bariadi wananisikia kwa hapa. Kwa hiyo nimesema hii tu ili tukitoka hapa tuwe na knowledge; baadaye pasije pakawa na kwamba aah! Unajua katika mipango hii inayopangwa hapa, resources nyingine imeenda upande fulani na upande mwingine umesahaulika. Sina maana ya kujitenga katika nchi hii, napanga tu na kusema ili ninapokuja katika bajeti aje na hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na akishakuja na hiyo ni wazi kabisa mipango hii itakuwa inakwenda vizuri, kwasababu hamna uchumi wowote mahali popote unaweza kuendelea kama huna miundombinu. Mazao kutoka shambani kwenda viwandani unapelekaje? Ni lazima tuwe na miundombinu ya kutosha. Na kwasababu hiyo ukiangalia maeneo yote yale hakuna barabara ya kutosha. Hakuna barabara ambayo unaweza kusema utapeleka mazao kwenye viwanda, na ukiangalia viwanda vyetu viko mijini na kwa maana hiyo basi niombe sana sana sana sana Mheshimiwa Lameck Mwigulu Nchemba na ndugu yangu Masauni, sisi wote ni vijana na vijana wengi tumeingia humu; tuwasaidie vijana wetu kwa kupeleka mazao yao kwenye viwanda kwa kuwawekea barabara hizi ambazo nimezisema.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho naona kabisa muda umeondoka lakini niombe kama nchi ni vizuri kujiwekea sheria ili sheria hizi zitusaidie. Nimshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan kwa kusema kabisa tunakwenda kupigilia maendeleo katika miradi mikakati iliyowekwa. Mungu ambariki sana na ninaendelea kumuombea ili tuendelee vizuri katika mipango ambayo imewekwa wote wawili wakiomba kura katika ilani ya CCM kwasababu barabara iko kwenye ilani ya CCM…

NAIBU SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa…

MHE. FLATEI G. MASSAY: …na nafikiri itakwenda vizuri Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii Mungu akubariki sana, naunga mkono hoja.