Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Simon Songe Lusengekile

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Busega

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. SIMON S. LUSENGEKILE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kutuwezesha kuwa hapa. Lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii nami kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa nchi yetu. Nimpongeze pia Mheshimiwa Vuma kwa kuitambua na kukubali mafanikio ya Timu ya Simba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijikite katika mambo machache sana kuchangia mpango huu ili kuendelea kuimarisha uchumi wetu. Lakini ijulikane ya kwamba ni lazima sisi kama Wabunge tuendelee kuisimamia Serikali ili tufikie ule mpango ambao unasemwa sasa wa per capita income dola 1,400 katika hii miaka mitano ijayo. Kwasababu sasa ni 1,080 na cut off ni 1,036. Kwa hiyo, bado tuko katika eneo ambalo si salama kwa sababu tofauti yake ni dola 44. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano Nchi ya Algeria mwaka 2019 per capita income ilikuwa 4,060 lakini 2020 ilishuka ikawa 3,970. Kwa hiyo, kushuka pia inawezekana. Kwa hiyo, sisi kama Wabunge lazima tuisimamie Serikali ili uchumi wetu uendelee kupanda kama ambavyo Mheshimiwa Waziri wa Fedha ameeleza katika mambo matano ambayo ameyazungumza yatakayokwenda ku-reflect uchumi wetu. Na ninaomba uchumi huu sasa uende uka-reflect kwa wananchi hawa waliopo huko kwenye majimbo yetu na wananchi kwa ujumla wa nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi watu wa Simiyu ukitafuta identity yetu ni zao la pamba. Lakini wananchi wetu wameshapoteza hope na zao la pamba. Kwa nini; kwasababu ya bei ya zao la pamba. Leo ninataka kuzungumza kidogo kuiomba Serikali kutafuta namna ya kuwezesha Mkoa wa Simiyu kuupelekea kiwanda, hasa cha kuzalisha vifaa tiba vitokanavyo na zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukipata kiwanda hiki maana yake zao la pamba sasa bei yake itaenda kuimarika. Na zao la pamba likiimarika maana yake sasa tutarudisha morali ya wananchi wetu kulipenda na kulima tena zao la pamba ambalo litaongeza uchumi wa wananchi wetu walioko huko kwenye Mkoa wa Simiyu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kiwanda hiki kitasaidia nchi yetu kwa namna ya pekee sana kwasababu kitazalisha zaidi ya ajira ambazo ni rasmi 600 na ajira ambazo si za moja kwa moja zaidi ya 1,000. Wananchi watapata ajira, watalipa kodi, watapata kipato, na hii sasa itakwenda kuimarisha uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe Wizara ya Uwekezaji iendelee kuhakikisha kwamba inawekeza kiwanda hiki katika Mkoa wa Simiyu ili zao la pamba, kama nilivyosema pale awali, liweze kuimarika.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitengeneza vifaa tiba vitokanavyo na pamba maana yake tunakwenda sasa kuimarisha kutokuagiza vifaa hivi nje zaidi ya asilimia 38.3. Asubuhi tumesikia hapa, tunaagiza zaidi ya asilimia 80. Sasa tukiwekeza kwenye kiwanda hiki tunakwenda kupunguza uagizaji kwa asilimia zaidi ya 38.3 ambapo tunatumia zaidi ya bilioni 147 kila mwaka kuagiza vifaa tiba nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ni imani yangu kwamba Waziri wa Fedha, Mawaziri wanaohusika, mtatusaidia kuhakikisha kwamba tunapata kiwanda kule Mkoa wetu wa Simiyu ili tuweze kuzalisha vifaa tiba vikiwemo cotton gauze, cotton swab na nguo za madaktari na manesi pamoja na mashuka ambayo yanaweza kutumika katika hospitali zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe Wizara ipunguze tozo mbalimbali kwa ajili ya wawekezaji. Lakini pia mamlaka husika ziwe na lugha moja, hasa mamlaka zinazotoa vibali kwa hawa wanaokwenda kuwekeza kwenye miji yetu. Nilitaka nizungumzie sana hapo kwenye eneo la kilimo ili wananchi wetu sasa wakanufaike. (Makofi)

Kwenye eneo la kilimo bado hatujawekeza mahususi katika kilimo cha umwagiliaji. Bado hatujatumia Ziwa letu Victoria, hasa kwenye Mwambao wa Ziwa Victoria, bado hatujalitumia vizuri katika suala zima la kilimo cha umwagiliaji. Ukianzia kule Rorya, ukija Musoma, ukija Bunda, ukija pale Busega, ukienda Magu, Mwanza, Sengerema, Buschosa na huko mpaka Bukoba, bado hatujatumia ziwa letu katika kilimo cha umwagiliaji. Kwa hiyo, niombe Wizara ya Maji ijikite kuhakikisha kwamba tunaimarisha miundombinu ili tuwe na kilimo cha umwagiliaji katika sehemu zetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninapongeza mradi ulioko mkubwa wa kuleta maji hapa; mzuri sana. Lakini pia niseme sisi ambao tunazungukwa na Ziwa Victoria bado tuna shida kubwa ya maji. Mfano kwenye Wilaya ya Busega wanaotumia maji safi na salama ni asilimia 42.9; bado tatizo ni kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapokuwa tunaangalia suala hili la maji pia tuone kabisa kwamba linaenda ku-reflect kilimo cha umwagiliaji kwa wananchi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili ambalo nataka kuchangia hapa ni eneo la asilimia10 ambazo zimepangwa kisera kwenye halmashauri zetu, ambapo asilimia nne ni kwaajili ya vijana, asilimia nne kwaajili ya akina mama na asilimia mbili kwaajili ya walemavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ipo kisheria na imepangwa lakini cha kusikitisha ni kwamba haifuatwi na hakuna anayefuatilia. Unakuta Halmashauri imepata mapato ya ndani safi lakini asilimia ambazo zinaenda kwenye group hili hazifiki hata 10, na hamna anayehoji wala anayesimamia. Wakurugenzi hawaojiwi, business as usual.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili lazima tulisimamie. Kama ni asilimia 10 itengwe kweli, kama makusanyo ya ndani ni bilioni moja asilimia 10 ni milioni 100, no discussion kwenye hili, ipelekwe milioni 100 sehemu husika. Lakini sasa hivi inaweza ikawa milioni 100 zikaenda milioni tano, milioni saba, hamna anayehoji, hamna anayechukua hatua, ni lazima eneo hili twende tukachukue hatua ili sasa vijana wetu tuwaimarishe na waweze kupata fedha hizi ili sasa waweze kuzitumia katika kuinua kipato chao pamoja na hawa akina mama na watu wenye ulemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie kidogo kwenye eneo la maliasili na utalii. Nimesikia kengele ya kwanza. Ukitoka Lamadi kuelekea Bunda pale katikati ya Lamadi na Bunda kuna wanyama wa Mbuga ya Serengeti. Ningeishauri Serikali, ili kuinua pia uchumi wa maeneo yale tufungue namna ya wanyama wetu waweze kwenda hadi ziwani, ukienda pale Nyatwali wanyama waende mpaka ziwani. Nasema hivi kwasababu itafungua uwekezaji katika Miji yetu ya Lamadi na Bunda na wananchi wa pale watazidi kunafaika na hali halisi ya uwekezaji ambao utapatikana maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya Maliasili iliangalie hili, ni eneo mojawapo ambalo tunaweza kuwekeza na ni eneo mojawapo ambalo linaweza kuipatia fedha Serikali, na hasa hasa katika hizi sehemu ambazo nimezitaja ikiwemo na mji wa Lamadi ambao sasa ni mji mkubwa, pamoja na mji mwingine wa Bunda. Eneo hili lazima tulitazame ili liweze kuingiza kipato katika eneo letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie kidogo habari ya TARURA, TARURA lazima tuitafutie fedha; kama TANROADS wanapata asilimia 70 na TARURA asilimia 30 kuna haja ya kuzungumza hapa tena. Kuna haja ya kuendelea kuingalia TARURA kwa jicho la pili, kuna haja ya kuingozea fedha ili maeneo yetu sasa yatengenezwe. Kule vijijini na kwenye majimbo tatizo la TARURA ni kubwa, tatizo la TARURA linalalamikiwa kila mahali. Barabara hazipitikim ukienda pale jimboni kwangu barabara ya kutoka Mwamanyiri kwenda Badugu haipiki, barabara nyingi hazipitiki. Sasa hata kama wazalishaji wa pamba watazalisha hatimaye tutazungumza tena habari ya barabara. Kwamba sasa gari zinaendaje kuchukua pamba huko ambako pamba imezalishwa kuja hapa mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokuwa tunazungumzia kuimarisha uchumi wa watu na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja lazima pia tuziangalie bajeti ya TARURA.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo niombe Wizara ya TAMISEMI, lazima tuje tuzungumze, na hapa lazima tuje tuone hali halisi ya namna ya kuiwezesha TARURA ili iweze kufanya kazi kubwa kwa ajili ya wananchi wetu. Wapo wengine ambao wamekuwa wakisema irudi TANROAD, Wizara ya Ujenzi lakini hapa issue sio kurudi TANROAD issue ni kuiongezea fedha ili iweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuunga mkono hoja na kazi iendelee. (Makofi).