Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Spika, kwa mara ya kwanza humu Bungeni kama kuna hoja ambazo sijawahi kuona hazipingwi na Mheshimiwa Mbunge yeyote ni hii ambayo ipo mbele yetu. Wachangiaji walikuwa Waheshimiwa 10 na wote wameunga mkono hoja ya Kamati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchangiaji wa kwanza alikuwa Mheshimiwa Omari Kigua ambaye yeye alizungumza namna Mheshimiwa Josephat Gwajima, ambavyo hakuweza kutoa ushirikiano kwenye Kamati na hata kwenye Taarifa ni kweli Kamati hii nyinyi Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi hata kwa zile clip chache mlizoziona maana yake zingine zilirushwa.

Mheshimiwa Spika, tulijitahidi kuwa waungwana vitendo vilivyokuwa vinafanyika ndani ya ile Kamati, nimeshangaa kidogo wakati Mheshimiwa Shally Raymond alivyosimama nilitegemea angeweza kusema hata jinsi ilivyokuwa siku moja kwenye Kamati Mheshimiwa Askofu Gwajima alivyoharibu hali ya hewa ya mle ndani mpaka Mheshimiwa Shally Raymond akasema kama kungekuwa na uwezekano wa kumrushia mtu ngumi humu, leo ingekuwa hivyo lakini wacha tumvumilie. Tulifanya uvumilivu mkubwa sana. Kwa hiyo, alichozungumza Mheshimiwa Omari Kigua ni kweli kuhusu Mheshimiwa Gwajima na hakuonyesha kujutia chochote.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu Mheshimiwa Jerry Silaa kama alivyosema Mheshimiwa Kigua ni kweli. Yeye alisema amezua tafrani kwa wananchi kuhusu kusema Wabunge hawakatwi kodi. Lakini akasema naomba radhi kwa hilo lakini hakuna mahali ambapo alisema naomba radhi kwa kusema uongo kuhusu Wabunge kutokatwa kodi. Lakini Mheshimiwa Shally Raymond yeye alipoongea Habari ya Mheshimiwa Gwajima aliunga mkono hoja. Lakini alisema kwa nini Mheshimiwa Gwajima hakugusia nchi zingine amegusia tu Tanzania na wakati yeye anajinasibu anawaumini zaidi ya milioni 2,400,000 dunia nzima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, inaonekana Mheshimiwa Josephat Gwajima yeye aliilenga moja kwa moja Serikali kwa matamshi yake ambavyo yanakwenda. Lakini kwenye hili suala la Mheshimiwa Shally Raymond Waheshimiwa Wabunge si lazima mtu umtaje kwa jina unapomlenga. Wanasheria pia mnafahamu kuna neno linaitwa innuendo ni mahali ambapo unamuelezea mtu lakini humtaji jina lakini yale maelezo unayoyaeleza hata mtoto mdogo mwenye ufahamu atasema huyu unamlenga fulani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Josephat Gwajima yeye alilenga moja kwa moja kwa kutumia neno hilo la kisheria kwa sababu inaonyesha wazi Serikali ndio ilituhamasisha kuchanja na Mheshimiwa Rais, Samia Suluhu Hassan ndio alianza kuchanja na kutuhamasisha. Sasa ukisema wamepewa fedha wanaoshabikia chanjo unasema indirect lakini unailenga Serikali. Kwa hiyo, ni kweli alikuwa anachonganisha na kugonganisha Mihimili.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Tunza Malapo yeye amethibitisha hapa kwamba, Mheshimiwa Gwajima pamoja na kwamba aliuaminisha umma kwamba ninakwenda kwenye hiyo Kamati nitapeleka ushahidi mwingine ambao hata sikuusema hata Kanisani. Lakini Mheshimiwa Tunza Malapo aliposimama hapa ni kweli Mheshimiwa Gwajima hakuwa na ushahidi wowote ambao aliowaaminisha watanzania wote.

Mheshimiwa Spika, na kuhusu suala la Mheshimiwa Jerry Silaa ni kweli hata kwenye kikao alikiri kwamba hata yeye anakatwa kodi kwenye mshahara wake. Sasa tunajiuliza alikuwa na nia gani kuwaambia wananchi jambo ambalo sio la kweli.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Joseph Tadayo aliongelea suala la Mheshimiwa Gwajima kushindwa kuthibitisha suala la Viongozi kupewa fedha ili wachanjwe alishindwa kabisa. Tulipomuuliza unaweza ukatutajia Kiongozi hata mmoja ambaye kapewa fedha? tena alibabaika sana mpaka akafika mahali akasema wanakamati mnakumbuka na Hansard zipo, ile fedha ni misaada. Lakini tukamuambia kwenye kauli zako hakuna mahali uliongelea suala la misaada lakini ulisema Viongozi wanaoshabikia chanjo wamepewa fedha.

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusu Mheshimiwa Jerry Silaa, Mheshimiwa Tadayo alichangia kwamba Mheshimiwa Jerry Silaa alishindwa kuthibitisha kwamba, Wabunge hawakatwi kodi kwenye mishahara yao.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Ali King aliunga mkono hoja kama wengine na yeye alisema kwamba ili ukitaka umaarufu unatakiwa uende tofauti na wenzio na hapa alisema, uende kinyume na akatoa ile mifano sikumbuki vizuri alisema nini, mchambawima ndio alitolea huo mfano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hiyo ndio hoja ya Mheshimiwa Ali King hata hapa Bungeni kama kwa mfano mtu akiamua tu kutafuta umaarufu akipanda hapa juu ya meza ataandikwa na vyombo vyote mbalimbali. Lakini atakuwa ametenda kosa ambalo sio la kawaida lakini alikuwa anatafuta umaarufu, hiyo ndio hoja ya Mheshimiwa King.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Agnes Hokororo aliunga mkono hoja kama wenzie. Aliunga mkono hoja zote mbili, lakini akaongelea Kanuni ya 85 ya Kanuni za Kudumu za Bunge za 2020 ambazo zinaongelea utovu wa nidhamu uliokithiri na akazungumzia kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka. Na hili ni kweli Waheshimiwa Wabunge hakuna uhuru ambao ni absolute timilifu kabisa, haupo hata kwenye sheria kila uhuru una mipaka yake.

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, yeye alikwenda zaidi mbali kwa ku-quote vifungu mbalimbali vya Biblia ikiwemo Marko 6, Waefeso 6:12, na akasema hata kwenye Biblia hakuna madhara ya kitu ambacho huamini hata kama utakuwa umepata chanjo, umepata tiba na kitu chochote. Na kwa kuwathibitishia hili wanakamati nadhani mliona kwenye mitandao wakati amekuja Mheshimiwa Josephat Gwajima hata kwenye Kamati kabla hajaitwa, wakati tunamuita alichelewa kidogo. Tukauliza kwa nini anachelewa kuingia wakati tumemuita? Wakasema anaona amezidiwa ghafla kabla ya kuingia kwenye Kamati ameomba akaletewe dawa kwanza anywe. Kwa hiyo, hata Mheshimiwa Josephat Gwajima anakunywa dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mchangiaji wa tisa alikuwa Mheshimiwa Mariam Ditopile yeye alinukuu maneno ya Mheshimiwa Rais kuhusu Wabunge kutulia. Ni kweli wako Wabunge wanatafuta kick kwa jinsi alivyochangia, lakini kick zenyewe za namna gani? Kwa maana nyingine isiwe kick ambazo zinaharibu hadhi, heshima ya Bunge na pia kuchonganisha.

Mheshimiwa Spika, lakini pia na suala lingine aliloongelea Mheshimiwa Mariam Ditopile ni hili suala la kwamba Viongozi wetu wamepewa fedha. Kwa kweli hii imewachanganya sana wananchi Waheshimiwa Wabunge na nyinyi mnafahamu. Wananchi wengi hawachanjwi wengine kwa imani ya kwamba waliochanjwa wamepewa fedha.

Mheshimiwa Spika, sasa maneno haya kama yanatolewa na Kiongozi ni kweli yanawachanganya wananchi na yanaleta kitu ambacho sio utulivu katika nchi. Na kwa suala la Mheshimiwa Jerry Silaa, Mheshimiwa Mariamu Ditopile kasema amesikitishwa na drama zake na ule ubishoo ambao alikuja nao kwenye Kamati yakiwemo yale mavitabu aliyokuja nayo rundo.

SPIKA: Ahsante, malizia sasa.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA – MWENYEKITI KAMATI YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Mheshimiwa Spika, ingawa uliuliza vile vitabu hakuweza kuvitumia vyote. Aliweza kutumia kitabu kimoja tu Biblia katika lile rundo lote ambalo alikuja nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na la mwisho ni la Mheshimiwa Elibariki Kingu naye ame-quote vifungu vya Biblia na amelaani yote ambayo yamekuwa yakiendelea lakini ameuliza jambo moja Waheshimiwa Wajumbe. Kwamba, je, enzi za Hayati Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa mfano vitu ambavyo anafanya Mheshimiwa Gwajima angefanya? Waheshimiwa Wabunge na hasa akina mama tunaongea mambo ya gender na kwamba sisi tunaheshimu gender. Katika muda mfupi tu, anatokea mwanaume mmoja tena Mheshimiwa Mbunge, anaanza kuzungumza jambo ambalo hata mtoto mdogo yeyote ambaye ana akili timamu atasema hivi huyu mbona anamdharau mwanamke?

WABUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, ndiyo.

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA – MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA HAKI, MAADILI NA MADARAKA YA BUNGE: Enhee! ndiyo maana yake, anamdharau mwanamke ndiyo hoja ya Mheshimiwa Kingu! kwamba je, wakati wa Mheshimiwa Hayati Magufuli angefanya haya? Maana yake kwa nini ayafanye wakati anaetawala ni mwanamke? Hii haikubaliki Waheshimiwa Wajumbe ninawaomba sana, Bunge zima liweze kuridhia maazimio yote mawili kwa ajili ya hizi hoja zote mbili ambazo tumeziwasilisha hapa kwa ajili ya majadiliano ambayo mmemaliza. Nirudie tena kuwaomba Wabunge wote waridhie maazimio yote mawili.

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Spika, naafiki.