Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Miaka Mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawapongeza sana kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Mchemba pamoja na ndugu yangu Mheshimiwa Masauni kwa namna walivyoweza kuwasilisha Mpango huu. Karibu yote nakubaliana nayo, lakini yako mambo ambayo nadhani nimeona kama hayajakaa vizuri sana na tunahitaji tuone namna bora zaidi ya kuyaweka.

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, nchi yoyote ile mojawapo ya jukumu lake kubwa kushinda yote ni kuhakikisha kwamba watu wake wanapata ajira. Kwenye suala la ajira ninyi wote ni mashahidi, vijana wengi wanamaliza darasa la saba, kidato cha nne, vyuo vikuu na vyuo mbalimbali vya kati lakini ukija kwenye ajira ni tatizo. Kwa hiyo, lazima Mpango huu tunapoupanga ujielekeze namna gani utaendelea ku-solve tatizo la ajira katika nchi yetu ambalo kwa kusema kweli sasa hivi hilo ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, unapozungumzia suala la ajira lazima tuangalie kilimo, viwanda, uvuvi na ufugaji. Labda leo mimi nichukulie mfano kwa pale Musoma; pale Musoma ni kwamba vijana wetu wengi hawana ajira kabisa kwa sababu viwanda vimekufa na vingine kwa bahati mbaya sana ninyi wenyewe Serikali ndiyo mnaviuwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na kiwanda pale cha MUTEX na kilikuwa kinafanya kazi na bahati nzuri mwekezaji wake ni mkubwa ni huyu Mohamed Enterprise, lakini tulimnyang’anya kwamba ameshindwa kukiendesha vilivyo, tukasema tunampa mwekezaji mwingine. Mpaka leo hivi tunavyozungumza huu ni mwaka wa pili kile kiwanda kina makufuli, watu wetu hawana ajira na wako mtaani. Mimi niseme tu kwamba itakapofika wakati wa uwasilishaji wa bajeti ya Mheshimiwa Mwigulu, niseme ni mjukuu wangu, lakini nitalia na shilingi yake kama hatakuja na majibu kamili ni kwa kiasi gani atatusaidia ku-solve tatizo la ajira kwa watu wetu wa Musoma, hasa kuhakikisha kwamba kile kiwanda cha MUTEX kinafunguliwa lakini sambamba na viwanda vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tunapozungumza kati ya mambo tunayohitaji kuyaangalia sana katika kuwasaidia watu wetu, nimezungumzia suala la mifugo, kilimo pamoja na uvuvi. Shida yetu kubwa ni kwamba kila leo hizi fedha zinazotengwa na Wizara badala ya kwenda kwenye ukulima zinaenda kwenye kilimo. Fedha zinapoenda kwenye kilimo hizo ndizo zinaishia kwenye zile mnaita facilitation; kununua magari, computer na kwenye mambo kama hayo. Tunategemea kwenye bajeti ya sasa fedha zielekee kule kwenye ukulima, kwa maana kwamba watu waweze kupata mabwawa ya kutosha kwa ajili ya irrigation, lakini waweze kupata pembejeo nzuri na zilizo bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii unaingia kwenye duka la pembejeo za kilimo ziko bidhaa fake zinauzwa mle, matokeo yake ni kwamba mtu anakuja kunyunyizia vile viuatilifu vyote ni fake. Kwa hiyo, yeye mwenyewe amehangaika halafu anarudi kupata hasara ya pili. Tunapozungumza suala la uvuvi ni kwamba fedha ziende kwa wale wavuvi wenyewe kwa kuhakikisha kwamba walau tunaweka mikakati ya kuona watu wanakuwa na uvuvi endelevu, unaoweza kusaidia watu. Mfano, vijana wetu wa pale Musoma wamesaidiwa vizimba vingapi ili waweze kupata ajira?

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unakuta vyakula vya samaki lakini yule mfugaji anaambiwa kwamba labda baada ya miezi sita yule samaki atakuwa amefikisha nusu kilo, matokeo yake anafuga mwaka mzima kutokana na chakula anachowalisha, lakini gramu 500 au nusu kilo wale samaki hawajafikisha. Shida kama hizo ni kwa sababu fedha haziendi kwenye uvuvi badala yake zinaenda tu katika usimamizi ambao hausaidii sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini hata unapozungumza suala la ufugaji, unakuta badala ya fedha kwenda kwa wafugaji ili wapate majosho, dawa bora, waweze kuwa na unenepeshaji mzuri matokeo yake ni kwamba hata dawa za mifugo nyingi ni fake. Haya yote ni baadhi ya mambo ambayo tunahitaji tuyaangalie na tuone kwamba ni kwa kiasi gani tunavyoweza kuwasaidia watu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini leo tunapozungumzia viwanda, yawezekana tukawa tunaangalia tu vile viwanda vikubwa kama MUTEX, MWATEX na vinginevyo, lakini naamini kabisa kwamba tukilisaidia Shirika letu la SIDO ambalo ndilo linaloshughulika na viwanda vidogovidogo na bahati nzuri Baba wa Taifa aliliweka karibu katika kila mkoa, lingesaidia sana suala hili la viwanda. Kazi kubwa ya SIDO inafundisha habari ya usindikaji na packaging. Bidhaa nyingi hata tungeenda kwa wenzetu walioendelea kama China viwanda vyao ni vile vidogovidogo ambavyo kazi kubwa ni kusindika na packaging, wanaweka ile bidhaa yao katika hali nzuri ya kuvutia. Kwa kufanya hivyo basi ni rahisi watu wetu wakaweza kufanya biashara zao ndogondogo pasipokuwa na shida. Tatizo SIDO zetu zote zimekufa. Kumbe SIDO ingeweza kutoa mafunzo mbalimbali ambayo yangewasaidia sana watu wetu wa Musoma, lakini na watu wetu wa Tanzania kwa ujumla katika kuendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho nadhani hili kwangu ni suala la ushauri, ni hili suala la TRA. Kama tunavyofahamu suala la TRA ni kweli wakati mwingine wanachukua fedha kwa nguvu na wananyanyasa watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Hayati John Pombe Magufuli amelikemea sana suala hili lakini na juzi Mheshimiwa Mama Samia Suluhu naye amekuja amepigilia msumari wa mwisho kwamba kuwe na utaratibu mzuri wa ukusanyaji. Hata hivyo, kumbuka kuna bajeti ambayo tunategemea Waziri atatukusanyia, lengo ni shilingi trilioni mbili. Lengo la shilingi trilioni mbili si fedha ndogo, yaani unahitaji kwenda extra mile kuona namna ya kuweza kuzikusanya.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi ushauri wangu, ili uweze kuweka check and balance, kwa maana ya kwamba wale TRA wafanye kazi yao, ushauri wangu ebu imarisha ile Board of Appeal iwe active, ifanya kazi ipasavyo. Ili TRA wanapombana yule mlipa kodi kama anaona ameonewa basi aweze kupata mahala pa kwenda, na majibu ya pale yakitoka haraka maana yake kama anadaiwa basi, maana siamini kama TRA anaweza kumuonea mtu halafu ukaenda na kule kwenye Board of Appeal na penyewe napo ukaonewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pale huwa kuna kakipengele, kwamba kama unataka kwenda huko kwenye Board of Appeal nadhani unapaswa kulipa one third ya kile ulichokadiriwa. Sasa, nimekadiriwa bilioni tatu, one third maana yake nilipe one billion sina.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunadhani kwamba hicho kipengele mkikiondoa hicho ili hata yule ambaye anadhani kwamba ameonewa aweze kusikilizwa katika ile Board of Appeal, na itakapokuwa active sasa itamsaidia sana katika kuhakikisha kwamba haki inatendeka, unapata kodi yako lakini na huko kwa mlipa kodi anapata haki yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)