Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

Hon. Dr. Thea Medard Ntara

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Kipindi cha Miaka Mitano kuanzia mwaka 2021/2022 – 2025/2026

MHE. DKT. THEA M. NTARA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku, kwanza niungane na wenzangu kutoa pole sana kwa Watanzania kwa msiba mkubwa uliotupata wa kuondokewa na aliyekuwa Rais wa Tanzania. Lakini pili, nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais na Makamu wake kwa kuapishwa kuwa viongozi wa juu wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitajikita kwenye sekta ya elimu yenye vipengele vinne. Pamoja na ufundishaji na outreach universities pia ina kazi ya kufanya research. Azimio la AU inaitaka kila nchi itoe asilimia moja ya pato lake kwa mwaka kufadhili utafiti na maendeleo i.e RMD. Sasa kwa kufanya hivyo kutawezesha Vyuo Vikuu kufanya research na wakati mwingine tumelalamika kwamba havifanyi utafiti lakini inabidi Serikali ichangie asilimia ya pato hilo ili Vyuo Vikuu wafanye research. Mfano leo hii, kuna Chuo cha MUST wanafanya action research ya kutengeneza majokofu kwa ajili ya kuhifadhi matunda kama walivyosema wenzangu. Matunda tunayo mengi sasa wao wanataka kutengeneza majokofu ili yahifadhi hayo matunda throughout na majokofu hayo yawe ya bei nafuu kwa wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Serikali ikitoa mchango, mimi nafikiri kama mikoa Tanga, Tabora na Tunduru wanaweza wakahifadhi matunda throughout the year na wakafanya biashara na wananchi wetu wakapata kipato. Hivyo, hilo nimuombe sana Mheshimiwa Dkt. Mwigulu na Profesa Ndalichako waliangalie hilo, watoe ile asilimia moja ili kuwezesha au ku-top-up fedha ambazo zinahitajika kwa ajili ya kufanya research. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili sasa hivi kuna upungufu mkubwa sana wa ajira, i.e lecturers na waendeshaji. Waziri Mheshimiwa Prof. Ndalichako analijua hilo kwamba Serikali ilikuwa na utaratibu zamani Vyuo Vikuu wanawabakiza pale vyuoni wanafunzi waliofanya vizuri sana wanakuwa ma-TA, Tutorial Assistant, halafu baadaye wanawajenga na kupeleka kuwasomesha wanakuwa baadaye Assistant Lecturers na baadaye wanakuwa PHd. Lakini leo hii utaratibu ule haupo, kwa hiyo, ndio maana tunapata shida katika kuwa na namba ya Wahazili wa kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Serikali, irudishe utaratibu ule wa zamani wahazili wale wabobezi wanaweza kutambua wanafunzi wazuri sana wakawabakiza pale na baadaye wanawakuza na baadaye tunakuwa na Wahazili angalu wakutosha katika vyuo vyetu. Tukiwaacha waondoke, inavyotokea sasa, wale best performance wakiondoka wakatoka kipindi kile wanamaliza masomo yao hatuwezi kuwapata tena wanaenda huko nje na wanachukuliwa. Lakini palepale waka-identify na wanarusiwa kuwabakiza pale basi tutapungua hilo tatizo la Wahazili katika Vyuo vikuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, agizo la Baraza la Madaktari Afrika Mashariki, linawataka Vyuo Vikuu vyote vyenye taaluma ya Sayansi na Tiba viwe na hospitali za kufundishia tunaziita teaching hospitals. Kwa mfano UDOM inatakiwa iwe teaching hospital, MUHAS iwe na teaching hospital, UDSM iwe na teaching hospital kwasababu wana ile taaluma ya Sayansi na Tiba. Serikali iruhusu hizo teaching hospitals wapewe hawa, wapewe na wanaweza kuziendesha wakati mwingine tumekuwa tunawasiwasi hawataweza kuziendesha mbona vyuo wanaweza kuviendesha. Kwa hiyo, na zile teaching hospitals kwanza zinaweza kufanya vizuri kabisa na hivyo ndivyo wanavyofanya wenzetu katika nchi nyingine zilizoendelea. Watoto wanatoka wanaenda pale wanakuwa na hospitali yao lakini at the same time ile hospitali yao ndio inakuwa kama wanafanya pale practical’s na mara nyingi ndio zinafanya vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Suala la mikopo wenzangu wengi hapa wamelizungumza, nishauri, kwasababu kumekuwa na malalamiko mengi na Waheshimiwa Wabunge hapa wengi sana wamefuatwa na wanafunzi kuombwa pesa. Taasisi zinaenda wanafunzi wanakuwa kama ombaomba, kama wanafunzi wote hao wanastahili kupata mikopo na tunashindwa kuwapa ile asilimia, tufanye hivi tupunguze asilimia ile ili kila mwanafunzi apate ile mikopo turudi badala ya asilimia 100 wote wapate flat rate ya asilimia 70 ili kusiwe na malalamiko, tukiendelea hivi kila siku na namba ya wanafunzi inaongezeka kila mwaka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tufanye hivyo ili angalau wanafunzi wote wapate mikopo na wengi wanaokosa mikopo ni watoto wa maskini. Kwasababu watoto wote wanaokosa mikopo ni watoto wa maskini ndio waliokosa mikopo, kwasababu mtoto kama hapa wa Mheshimiwa Dkt. Ntara lazima nitajipigapiga hapa nitamlipia lakini wa wale wa maskini hawawezi, ndio maana wamekuja hapa Dodoma. Nina mzigo mzito hapa nitamkabidhi, mzigo mzito wanasema mpe Mnyamwezi, nitamkabidhi hayo majina Mheshimiwa Prof. Ndalichako abebane nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapo hapo kuna lile suala la penati, watoto tumeshindwa kuwaajiri au ajira hizi tunazijua hazipo. Mtoto anamaliza Chuo Kikuu ana kaa miaka sita unamwambia akipata ajira alipe penati, hilo mie naomba liondolewe kabisa. Yaani liondolewe, yaani hakuna ku- discuss sijui percentage nini, hili liondolewe hatuwatendei haki, sasa hivi wanahangaika wanajiajiri wenyewe, hii mikopo hata kidogo wanayopata watoto wote wanafanya umachinga badala ya kusoma sasa, hujikita kwenye kusoma, watoto wana vibanda vya chips, watoto wana pikipiki ndio maana unakuta sasa kunakuwa na vurugu tu. Ebu tuwasidie watoto tuwape asilimia inayofanana wote na baadaye wakimaliza mikopo hakuna mambo ya penati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza mambo ya penati, leo hii niwaambie kitu kingine ambacho kinasikitisha. Kuna wanafunzi wa Vyuo Vikuu wanaofanya biomedical wanapokwenda kufanya field wanadaiwa walipe pesa. Ni jambo linalosikitisha sana, wanaenda kufanya field wanaambiwa walipe pesa kwa kutumia vile vifaa wanavyovikuta pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni sawasawa na mwanafunzi ambaye anakwenda teaching practice anafika pale kwenye shule anaambiwa wewe umekuja kufundisha hapa, enhee! utulipe pesa, anakwenda pale kutoa huduma halafu anaambiwa alipe. Hilo nalo naomba muliangalia Mheshimiwa Waziri wa Elimu pamoja na Mheshimiwa Waziri wa Afya. Tunahitaji Watoto hawa waende field wakafanye kazi, mikopo wamekosa halafu mnamdai tena pesa, hilo naomba mliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana. (Makofi)Napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)