Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia Maazimio mawili yaliyopo mbele yetu; azimio la kuenzi kazi za Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Azimio la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama Samia Suluhu Hassan.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitoe pole kwa Taifa la Tanzania kwa kuondokewa na Rais wetu, nitoe pole kwa familia ya marehemu kwamba tumeondokewa na kiongozi ambaye tulikuwa tunampenda lakini Mwenyezi Mungu amempenda zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wangu nitaongelea mambo kama mawili au matatu kumhusu Mheshimiwa Dkt. Magufuli. Mwaka 1775 -1783, Marekani walikuwa katika vita vya mapinduzi vya kujitelea uhuru. Baada ya kupata uhuru Wamarekani walifanya utafiti kupitia chuo kinaitwa National Institute of Psychology. Katika chuo kile walifanya utafiti ili kujua unapotaka kufanya mabadiliko katika nchi au katika taasisi yaani institutionalization unatakiwa kufanya vitu gani. Marekani walikuja na vitu saba ambavyo walisema lazima waviweke katika vichwa vya watu wao. Jambo la kwanza walilogundua ni kubadilisha attitude na mindset za watu wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa ambalo Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ametusaidia kama Taifa ni kubadilisha attitude na mindset zetu Watanzania ambapo ilifikia hatua tukawa tunatembea na falsafa kuwa Watanzania siyo masikini na sisi Watanzania siyo maskini na Taifa letu ni tajiri. Jambo hili limeweka msingi mkubwa ambapo imefikia kama taifa tunatumia rasilimali za ndani kuleta maendeleo. Taifa linajiendesha, tunajenga vituo vya afya, tunajenga miundombinu na kila kitu ambacho kinaweka misingi ya maendeleo katika kuhakikisha Taifa letu linasonga mbele. Kwa hiyo, katika hili tutamuenzi Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na hakika tunaendelea kutamba na kutembea kifua mbele kwa ujasiri sisi Watanzania ni matajiri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni tekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015 kwa ufanisi mkubwa sana. Katika hili hakuna ubishi. Unapoongelea Ilani ya Chama cha Mapinduzi kuna kitu kinaitwa Mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwelekeo wa Sera za Chama cha Mapinduzi wa mwaka 2010-2020 ulitaka Serikali ya Chama cha Mapinduzi itakayoingia madarakani 2015 iweke msingi wa kuhakikisha tunafikia uchumi wa kati ifikapo 2025. Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akishirikiana na Makamu wake wa kipindi kile mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa na Bunge la Kumi na Moja tulifika uchumi wa kati mwaka 2020, miaka mitano kabla. Hili ni jambo la msingi na la kuenziwa na sisi tunawashukuru mliokuwa katika safari ya Bunge la Kumi na Moja. Kwa hiyo, haya ni mambo makubwa na ya msingi ambayo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyafanya katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la tatu ambalo Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano wamelifanya ni kuhakikisha tunakuwa na mfumo wa malipo Serikalini ya kielektroniki tunasema e-payment. Tulihama kutoka mfumo wa billing system tukaenda electronic payment na tuka-establishi kitu kinaitwa Government Electronic Payment Get Way jambo ambalo leo hii tunatamba na kusema tunajitahidi kukusanya mapato lakini ni kwa sababu ya mfumo imara wa ukusanyaji ambao umehakikisha mapato yanatoka na kwenda katika chungu kimoja. Katika hili tunamshukuru Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Serikali yake ya Awamu ya Tano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo kwa upande wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, nije katika suala la kumpongeza Rais mama Samia Suluhu. Nimesimama hapa kwa niaba wananchi wa Jimbo la Igunga, Mkoa wa Tabora, tunampongeza kwa kuapishwa kuwa Rais wa Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kuwa alikuwa sehemu ya Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, tunaamini gurudumu atalipeleka vizuri, tutakwenda vizuri kama Tanzania na sisi wananchi wa Igunga tupo tayari kumuunga mkono. Walituletea maji ya Ziwa Victoria, tuna tenki kubwa la maji Igunga lenye uwezo wa kubeba maji lita milioni mbili na laki tano kwa wakati mmoja. Tunawashukuru na kuwapongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepata umeme vijiji 30 na sasa tunakwenda kupata umeme vijiji 30 vingine. Jimbo la Igunga tutakuwa na umeme jimbo zima tunawashukuru sana. Pia tumehakikishiwa na tumeendelea kujengewa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ambacho kwa mara ya kwanza kiwanja chake kilipatikana mwaka 1995. Serikali ya Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan na Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli iliyopita wametoa fedha sasa tunajengewa Chuo kikubwa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi katika Jimbo la Igunga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kifupi Jimbo la Igunga tunamtakia kheri, tupo naye tutamuunga mkono na tutapigana usiku na mchana kuhakikisha Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezwa. Ahsante sana. (Makofi)