Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Emmanuel Adamson Mwakasaka

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. EMMANUEL A. MWAKASAKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kupata nafasi hii kuchangia Maazimio yote mawili. Ni kweli tumepata msiba mzito sana kwa nchi lakini pamoja na mataifa mengini, ni pole kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan lakini pamoja na sisi sote.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kawaida watu wakipatwa msiba hata katika familia zetu ni lazima watayumba sembuse msiba mkubwa kama huu ulioupata taifa, ndiyo maana wengine wameanguka, wengine walikosa matumaini, ni kawaida misiba inapotokea. Pia na matendo ya aliyetutoka, matendo ya Mheshimiwa Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ambayo amelitendea Taifa hili hasa katika nyanja za maendeleo, miradi mingi imetajwa pamoja na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali, ndicho kitu ambacho Watanzania wengi sana waliweza kulia na kunguka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kunukuu maneno ya Mheshimiwa Rais Kenyatta, Rais wa Kenya, wakati amekuja kutoa rambirambi na salamu za mwisho alimuambia Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu Hassan kwamba hata wao Kenya wanaona Mheshimiwa Rais hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli ameshafungua njia. Kwa hiyo, kazi yetu sisi ni kufuata njia ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sina mashaka yoyote na mama Samia Suluhu Hassan ambaye ni Rais wetu wa sasa. Tumeshaanza kuona kwa vitendo namna gani ameanza kazi. Msiba kwa sasa tunao kwa siku zile 21 lakini na kazi zinaendelea. Nampongeza sana Mheshimiwa mama Samia Suluhu Hassan kwa jinsi alivyoanza kufanya kazi zake. Ameanza kidogokidogo kutusahaulisha hata yale machungu na mashaka ambayo watu walikuwa nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sipendi sana kuongelea huyu ni mwanamke, huyu mwanaume, napenda sana kuangalia utendaji wa kazi. Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameanza kazi vizuri sana kwenye kikao kile ambacho kilikuwa cha kupokea ripoti ya CAG na wengine walitajwa kidogo baada ya kusomwa ile ripoti siwezi kusema aliondoka na mtu lakini kuna kitu alikiona hakijakaa sawasawa haraka sana aliweza kuchukua hatua na haya ni matarajio ya wananchi wengi katika utendaji wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, siyo hivyo tu, mara nyingi sana vitu vinavuja kwa viongozi mbalimbali hasa katika kazi za utendaji, kitu kinaweza kikawa ni siri lakini kinavuja. Leo hii watu waliongelea watu wa mitandao hapa, kuna mmoja akamtaja Kigogo na wengine, kwa mara ya kwanza kina Kigogo leo hawakujua hata jina ambalo litaletwa humu. Walitaja majina mbalimbali ambayo wanayajua wao siye hatukuliona humu. Pia nikipongeze Chama changu cha Mapinduzi katika hili kwa sababu Mheshimiwa mama Samia Suluhu yeye ndiye Mwenyekiti wa Chama chetu cha Mapinduzi mpaka tunaingia humu hatujui jina ni la nani litakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan ameanza vizuri mama yetu tuendelee kumuombea. Kazi hii ni ngumu na ni nzito halafu imekuja ghafla, sisi tuendelee kumuombea ili aweze kufanikiwa katika majukumu yake na aweze kuliongoza Taifa letu vizuri na mimi sina shaka hata kidogo na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba niunge mkono Maazimio yote mawili kwa asilimia mia moja, nakushukuru sana. (Makofi)