Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Dr. Christine Gabriel Ishengoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. DKT. CHRISTINE G. ISHENGOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana kwa kunipatia nafasi ya kuchangia katika maazimio yote haya mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpa pole Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuondokewa na Rais wetu, na Watanzania wote pia nawapa pole kwa msiba tulioupata, msiba mkubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili naomba kusema kuwa Mheshimiwa hayati Dkt. Magufuli hakuna mtu ambaye haoni mambo aliyoyafanya. Alifanya mambo mengi mazuri na kweli inabidi tuyaenzi na tumuenzi kwa mambo yote aliyoyafanya. Amegusa kila kitu, kila Nyanja, kila sekta, kila mkoa, amefanya mambo mengi. Siwezi kuyarudia kwa sababu yote yameshasemwa, lakini afadhali niseme machache hasa kama reli ya mwendokasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa reli ya mwendokasi kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro ambayo sasahivi ujenzi umeshafika Morogoro nadhani alitamani kuiona, kuingia na yeye kuona anatembea kwenye reli hiyohiyo, lakini Mwenyezi Mungu hakupanga; lakini Watanzania ametuachia naamini Mheshimiwa Mama Samia, Rais wetu, ataendelea pamoja na wengine. Viongozi bado tunao watamalizia wataiendeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia alifanya mambo ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo na yenyewe ilikuwa imekaa kwa muda mrefu. Amefufua viwanda, ameanzisha viwanda, Mheshimiwa Rais kwa kweli Hayati Magufuli kila mmoja inabidi amuenzi, kila mmoja ameona aliyoyafanya. Hakuna kipofu kila mmoja ameona aliyoyatenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba tumuombee kwa Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Na ninamalizia kusema amina. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kusema kuwa Mheshimiwa Rais, Hayati Magufuli ameondoka lakini ametuachia viongozi, ametuachia Mheshimiwa Mama Samia, ametuachia Rais wetu Mheshimiwa Mama Samia, mama shupavu, mama mahiri, mama mtulivu, mama mnyenyekevu ambaye atatuvusha kwa yale yote ambayo yalikuwa yanafanywa Mheshimiwa Hayati Magufuli. Mheshimiwa Mama Samia alikuwa Naibu wake, Makamu wake na alikuwa anafanya mambo bega kwa bega pamoja na Hayati Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi yote iliyokuwa inaendelea Mheshimiwa Rais Samia anaifahamu vizuri sana. Mheshimiwa Rais wetu Samia ametembea nchi nzima anajua kila kitu kinachotendeka Tanzania. Kupitia kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi anaifahamu miradi pamoja na watendaji wake wa Serikali. Hatuna shaka Mheshimiwa Rais wetu atatuvusha, tuna imaninaye, tutafika mahali kule Kaanani, tutafika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Mama Samia naamini na Watanzania wanamuamini; na yeye alisema kwenye mambo ya maji ataweza kuwatua. Yeye pamoja na Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Mama Samia alikazania sana maji hasa kwa upande wa akinamama. Mheshimiwa Mama Samia tulifanya kampeni naye, wote mlikuwanaye mikoa mingi, mliona mambo mengi aliyokuwa anasisitiza sio tofauti na Mheshimiwa Hayati Magufuli aliyokuwa anayatenda kwa sababu walikuwa wanafanya kazi pamoja. Kitu cha msingi tuzidi kumuombea Watanzania wote, wananchi wote, Serikali tushikamane nao, Wabunge, kusudi tuweze kufika kule ambapo tumeanza na ambapo tunakwenda. Nani haoni ndege ambazo zinaendelea?

Mheshimiwa Naibu Spika, najua Mheshimiwa Mama Samia ataendeleza yale yote, tuna imani naye hatuna tatizo. Mnaona hata mijadala kwenye TV, wananchi wote wanamsifia Mheshimiwa Mama Samia hakuna ambaye anasema ooh. Wale ambao wanabeza hawapo, nadhani kama wapo hawajui wanalolisema, Mheshimiwa Mama Samia atafanya kila kitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Samia ni mwanamke wa kwanza kuwa Rais hapa Tanzania na Afrika Mashariki. Naamini atafanya; kama wanawake wanaweza na wanaume wanaweza hakuna tofauti. Mwenyezi Mungu alipomuumba Adam na Eva aliwaumba wote sawa. Naamini tutafanya kazi naye na tutampa ushirikiano na tutafika kila kitu kitakwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho wa yote ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, Waheshimiwa Watanzania, naomba tuzidi kumuombea Mheshimiwa Rais wetu, Mheshimiwa Samia Hassan Suluhu, azidi kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ninashukuru kwa kumpata Mheshimiwa Dokta Mpango. Tunampa pongezi Dokta Mpango, tunampa pongezi Mheshimiwa Rais wetu kwa kumpendekeza na Kamati Kuu kumpendekeza na Bunge tukampitisha kwa asilimia 100. Mheshimiwa Mpango ni mpole, mchapakazi, anaweza, Makamu anafanya kazi, tunashukuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimefurahi sana mpaka moyoni mwangu. Nilivyofurahi ndivyo Wabunge walivyofurahi. Nilivyofurahi ndivyo Watanzania walivyofurahi. Napata message nyingi kutoka kwa Watanzania. Napata message nyingi kutoka kwa wananchi wa Morogoro. Napata message nyingi kutoka wanawake wote na wanaume wote Tanzania. Mwenyezi Mungu aijenge Tanzania. Mwenyezi Mungu ambariki Rais wetu. Mwenyezi Mungu ambariki Makamu wa Rais. Na Mwenyezi Mungu awabariki Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana. Mwenyezi Mungu tubariki Bunge zima, nashukuru. (Makofi)