Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Azimio la Bunge la Kutambua na Kuenzi Mchango wa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa Utumishi wake Uliotukuka Pamoja na Azimio la Bunge la Kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza kabla sijaongea ninapenda kutoa pole kwa Kiti cha Spika pamoja na wewe pamoja na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi walioondokewa na kiongozi wao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nitumie nafasi hii kumpongeza Rais wa kwanza mwanamke, mama Samia Suluhu Hassan akituwakilisha wanawake ambao tunaona maono mbele ya kutetea Taifa hili la Tanzania na kwenda mbele kupambania haki za wanawake, wanaume na watoto wa nchi hii; ninampa pongezi. Yeye alipoapishwa tarehe 19 aliongea maneno ya matumaini kwa Watanzania; alisema tuache yaliyopita sasa tuijenge Tanzania mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimuombe mama Samia Suluhu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nchi yetu ni moja na sisi sote tumezaliwa Tanzania kwa kusudi la Mungu. Tunamuomba asimame kama Rais wa watu wote, Rais wa vyama vyote. Ninamuomba Mheshimiwa Rais pamoja na pongezi tunazompatia, tunaomba agange majeraha yaliyowapata Watanzania hasa wakati wa uchaguzi. Aweze kuwaachilia wafungwa wa kisiasa ambao bado wapo magerezani, hasa wale waliokuwa wamesingiziwa. Waliokosea, sheria ichukue mkondo wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais tunayempongeza leo alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Tunaomba sana Mheshimiwa Rais uanzie pale ulipoishia, Katiba ya Warioba tunaomba uanzie hapo kulisogeza mbele Taifa letu la Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba tangu ameapa kuwa Rais nchi imetulia, imeanza kupoa, watu wameanza kupata amani. Tunaomba amani hiyo yeye kama mama aisimamie, ahakikishe anasimama kama Amiri Jeshi Mkuu anayetetea pande zote bila kubagua. Tumeona viongozi baadhi ya vyama wameanza kuomba msamaha; hiyo ni dalili njema ya kujua kwamba kiongozi aliyepo sasa anasimamia haki, atasimamia Katiba na ataijenga na kuisimamia.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, ninasisitiza tena; ninakupa pongezi Mheshimiwa Rais, kwamba utasimamia haki na Katiba ya Watanzania kuhakikisha tunakwenda mbele maana safari bado ni ndefu, Tanzania bado ni imara, wewe ndiwe tunakutegeme kuijenga na kuisogeza mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya nasema ahsante sana. (Makofi)