Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Abeid Ighondo Ramadhani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili iweze kuchangia jioni ya leo. Awali ya yote, nianze kwa kutoa pole kwa wananchi wenzangu wa Jimbo la Singida Kaskazini kwa msiba uliowapata kwa kuondokewa na mwananchi mmoja, Mzee Salimu Isango baada ya gari waliyokuwa wanasafiria kutoka Ng’amu kundumbukia kwenye Mto katika Daraja la Mwakiti. Nawapa pole na niwaambie kwamba Mpango huu wa Taifa wa Miaka Mitano umesema kwamba utajikita katika uchumi shindani na viwanda kwa maendeleo ya watu. Kwa hivyo, daraja hilo naamini litatengenezwa na litaepusha vifo vinavyoendelea kutokea hasa kipindi hiki cha mvua maji yanapokuwa yamejaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kuzungumzia eneo la Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Msiba mkubwa uliopo kwa vijana wa Kitanzania hivi sasa pamoja na wasomi wote wanaopita vyuoni kwa kupata mkopo huu ama mikopo hii ya elimu ya vyuo vikuu ni tofauti na matarajio ambayo yaliwekwa kwenye mfuko huu. Serikali ilikuwa inalenga kuwakomboa wananchi wake maskini lakini kinachotokea hivi sasa watoto wa kimaskini wanaonufaika na mkopo wa elimu ya juu pindi wanapomaliza masomo palepale wanakabwa wanaambiwa waanze kulipa mkopo bila kujali amepata ajira pale pale anageuka kuwa mdaiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kweli kama sisi tumelenga kuwakomboa Watanzania, jana umemkopesha kwa sababu ni mtoto maskini aliyeshindwa kujisomesha. Kesho baada tu ya kumaliza masomo hajapata kazi umeshambana. Kwa maana hiyo hapa Serikali badala ya kuwasaidia watu wake imegeuka sasa inafanya nao biashara. Kitu ambacho ni hatari sana kwa maisha ya Watanzania na kwa elimu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafahamu changamoto ya ajira ilivyo kubwa hivi sasa. Tunasahau hapohapo, badala ya sisi kujikita kuwasaidia hawa vijana ili watoke waende wakafanye kazi hata kwa kushirikisha Sekta Binafsi, sisi tunawakaba hapohapo bila kujali changamoto wanazokutana nazo na mazingira magumu ya elimu tunayoyaona sisi wenyewe hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba hii bodi badala ya kujikita kwenye kuwabana watoto hawa kwa kuwadai mikopo hii warudishe pindi wanapomaliza masomo, iwape muda wa kulipa madeni yao. Pia riba zipungue, riba zimekuwa kubwa sana kwenye eneo hili.

MWENYEKITI: Jitambulishe wa taarifa. Mheshimiwa Naibu Waziri endelea.

T A A R I F A

NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji kwamba Ibara ya 178 ya Sheria ya Bodi ya Mikopo inawapa nafasi wahitimu kurejesha mikopo baada ya miaka miwili. Marekebisho hayo yalifanyika mwaka 2016 ikaondoa kipindi cha mwaka mmoja na hivi sasa marejesho yanafanyika baada ya miaka miwili na ilipitishwa na Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Ighondo, pokea taarifa hiyo.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, lakini tatizo ni riba kubwa zilizopo kwenye hii mikopo, tupunguze riba hii. Mwanafunzi anapoanza kulipa ule mkopo alipe lile deni alilokopa na huu mkopo usiwe na riba, ndiyo hoja kubwa ninayotaka kuisimamia hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kitu kinaitwa retention, ule mkopo unaongezeka kadri muda unavyokwenda, ndiyo kitu ambacho mimi nataka nikiombe hapa; badala ya huyu mtu kuja kulipishwa riba alipe ule mkopo, principle aliochukua, ndiyo hoja kubwa ambayo naiomba Serikali ichukue hili na iliangalie kwa makini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo watoto hawa wanaomaliza vyuo wapate kazi, tushirikishe sekta binafsi. Tushirikishe sekta binafsi hawa watoto waende wafanye practical, wafanye mazoezi, hata Serikali inavyotangaza ajira kile kipengele cha uzoefu wa miaka 15 mtoto huyu atafaulu.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka tu kumpa taarifa mzungumzaji kwamba licha ya riba bado muda wa miaka miwili ambao umetengwa ni wa karibu sana. Hapa asubuhi umetupa testimony ya mtoto aliyemaliza Mzumbe, ana takribani miaka sita hajapata ajira, sasa baada ya miaka miwili unaanza kumwambia atoe laki moja, anazipata wapi wakati hana ajira. Kwa hiyo hilo nalo Serikali iweze kuli-consider.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo nampa hiyo taarifa. Ahsante.

MWENYEKITI: Malizia kwa sentensi moja Mheshimiwa Ramadhani kwa sababu muda umekwisha.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Napenda pia angalau kwa uchache nizungumzie kidogo kwenye eneo la viwanda…

MWENYEKITI: Bahati mbaya umechelewa. (Kicheko)

Ahsante sana Mheshimiwa Ighondo.

MHE. ABEID R. IGHONDO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)