Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuweza kuchangia jioni hii ya leo. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee naishukuru na kuipongeza sana Wizara ya TAMISEMI kwa jinsi ambavyo inasaidia kina mama kupata mikopo ya asilimia 10 ambapo ni asilimia 4 kwa vijana; asilimia 4 kwa kina mama; na asilimia 2 kwa walemavu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nimesoma na kuuelewa sana Mpango huu wa Maendeleo wa miaka mitano. Naomba sana nijikite kuishauri Serikali kuangalia namna ambavyo inaweza kuwasaidia akina mama na vijana hawa kwa kuwaboreshea kutoka kwenye asilimia zile 4:4:2 na kuwapa asilimia 10.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mnavyoelewa, kina mama ndiyo wanaoweza kuibeba jamii na ndiyo wanaobeba familia katika kuzihudumia. Hivyo naiomba sana Serikali sasa ione kuna umuhimu wa kina mama hawa ambao pia ndiyo waaminifu wakubwa katika upigaji wa kura, kina mama hawa ambao wamekibeba Chama cha Mapinduzi kwa kuwa waaminifu kwa kupiga kura nyingi sana za ndiyo kwa rahisi wetu Dkt. John Pombe Magufuli, sasa ni wakati wa Serikali yetu sikivu ione umuhimu wa kuiboreshea kina mama hawa kutoka kwenye mkopo wa asilimia 4 na kuwapa asilimia 10. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia Serikali yetu sikivu iweze kutoa elimu ya kutosha, elimu wezeshi kwa kina mama hawa ili waweze kunufaika na mikopo hii. Kuna baadhi ya maeneo kina mama kweli wamekuwa wakiomba mikopo na kupewa mikopo hii lakini mikopo imekuwa haiwanufaishi kutokana na kwamba elimu wanayopewa ni ndogo. Mfano, kina mama wanaojitolea katika kazi za za kufuga nyuki, napenda sana Serikali yetu sikivu iweze kutoa elimu wezeshi kwa kina mama hawa ni namna gani wataweza kufuga nyuki ili waweze kunufaika wao lakini waweze kutoa wigo wa ajira katika jamii zinazowazunguka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee sana napenda nijikite katika kuzungumzia Wizara ya Maliasili. Niiombe sana Serikali yetu sikivu, sisi wananchi wa Mkoa wa Katavi tunayo Katavi National Park, naiomba sana Serikali yetu sikivu ili kuendana na Mpango huu wa Maendeleo ituboreshee barabara katika maeneo yale ya hifadhi ili kuwawezesha watalii wanaokuja Katavi kuweza kupita kwa urahisi zaidi. Tumeona kipindi cha masika ambacho ndicho kipindi wanyama wanapatikana kwa wingi, kipindi ambacho utalii ungefanyika kwa wingi kule Katavi, barabara hazipitiki na hivyo kuwazuia watalii wengi kuvutiwa kuja Katavi National Park. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naiomba sana Serikali yetu sikivu kuiboresha hifadhi hii kwa ku—promote kwa kutoa matangazo mbalimbali ili watu wote duniani waweze kuifahamu Katavi National Park. Katavi National Park ni hifadhi pekee yenye Twiga mweupe. Natamani sana Watanzania na Waheshimiwa Wabunge wenzangu muifahamu Katavi National Park, ni hifadhi ambayo ina vivutio vingi sana. Hivyo, Serikali ikiboresha miundombinu katika hifadhi hii itaweza kupata mapato makubwa lakini tutaweza kwenda kutoa fursa za ajira kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi wakiwepo vijana wanaozunguka mkoa ule. Pia itawasaidia kina mama kwa kuwawezesha kutengeneza curio shop ambapo wataweza kuuza vinyago mbalimbali kwa watalii lakini kutoa fursa mbalimbali za kibiashara ikiwepo mama ntilie kupika na kuwahudumia watalii wanaokuja katika hifadhi hii ya Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sana kutoa shukrani zangu za dhati kwa jinsi Serikali inavyoendelea kutuhudumia wananchi wa Katavi kwa kutupa miundombinu katika maeneo mbalimbali lakini kutupa ulinzi na kuhakikisha hali ya amani ipo katika Mkoa wetu wa Katavi. Hivyo naipongeza sana Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kipekee naendelea sana kuwashukuru akina mama wa Mkoa wa Katavi kwa jinsi ambavyo wameniamini mimi kama mwakilishi wao kuja kuwawakilisha. Nawaahidi sitawaangusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)