Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Vedastus Mathayo Manyinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Musoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. VEDASTUS M. MATHAYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua nafasi hii kukushukuru kwanza kwa kunipa nafasi. Vile vile nimepitia hotuba ya Mpango, umekaa vizuri pamoja na kwamba yapo marekebisho na ndiyo maana tuko hapa kwa ajili ya kuweka sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapokuwa tunapanga mipango hii, lazima ianzie kule kwetu kwa maana ya Halmashauri zetu. Wakati mwingine yako mambo ambayo yako kwenye uwezo wa Serikali, lakini kunakuwa na ukiritimba ambao unakwamisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikianzia na Jimbo langu la Musoma Mjini, huwezi kuamini lile jimbo ambalo lina wakazi wasiopungua laki mbili lakini lina ukubwa wa square kilometer zisizopungua 63. Kwa maana kutoka upande mmoja kwenda upande mwingine haizidi kilometa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya shida kubwa ambayo tumeendelea kuipata toka miaka na miaka, maana pale mimi nimekuwa Mstahiki Meya toka 2000 mpaka 2005, lakini vile vile nikawa Mbunge toka wakati huo 2005. Tumekuwa tukipambana au tukijitahidi sana kuongeza maeneo, kwa sababu kusema kweli square kilometer 63 kwenye wakazi 200,000, maana yake ni kwamba leo ukija pale Musoma unataka tu uwanja; kuna mwekezaji amekuja anataka uwanja ajenge tu hata shule. Hiyo nafasi haipo. Hakuna chochote utakachotaka kufanya kwa sababu ya eneo kuwa dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa utaratibu unasema tuzungumze na halmashauri husika. Tumezungumza lakini mwisho wa yote hawako tayari kutoa yale maeneo. Sasa athari kubwa tunazozipata ndizo hizo kwamba leo hii hatuwezi kujipanua, hatuwezi kufanya uwekezaji, kwa hiyo, hata namna ya kuongeza mapato katika Mji wetu wa Musoma imekuwa ni tatizo kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inalifahamu hili. Tumejaribu kupitia katika vikao vyote mpaka RCC lakini suala hili hadi leo tunazungumza limeshindikana. Ukiangalia, hata wale wenyewe wanaokatalia hayo maeneo, unamkuta mtu, pale tulipo kwa sababu ni kata za jirani, kuja mjini kwa maana ya Makao Makuu, anatembea, ni kama kilometa tano. Kwenda kwenye Makao Makuu ya Jimbo lake, anaenda kilometa 80. Kwa hiyo, ukiangalia kwa namna moja au nyingine, yule mwenyewe kwa maana ya mwananchi, anapata adha kubwa kwa kwenda kuhudumiwa kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokuja kwenye hizi huduma za jamii, mfano leo ukizungumza hospitali, hawa wote wanakuja wanakuja pale mjini. Anapotaka kwenda shule, anaacha shule mita 200, lakini anaenda shuleni kilometa tano mpaka saba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hizo juhudi ambazo tumezifanya, tunajikuta kwamba wale wananchi hata tulipowazungukia katika kuzungumza nao, wote wanataka kuja mjini. Pamoja na kwamba wanataka kuja mjini, ukifika tu kwenye Baraza la Halmashauri, basi mnakaa vikao lakini wanasema watawajibu, wakijibu wanasema hatukukubaliana na hilo ombi lenu. Ndiyo maana wakati mwingine tunasema, Serikali kwa sababu inayo nafasi ya ku- intervene katika kuhakikisha kwamba vile vile inatusaidia ili tupate maeneo makubwa, wawekezaji wakija wapate. Watu wakitaka viwanja wapewe. Basi hiyo itatusaidia sana katika kukuza Mji wetu wa Musoma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukiangalia Musoma, naamini umefika pale umeona, Musoma lazima ufunge safari kwamba unaenda Musoma. Yaani huwezi tu kupitia kwamba unaenda Mwanza, unaenda Sirari, lazima ufunge safari kwamba unaenda Musoma. Pale uchumi pekee tulionao, kidogo ni ziwa ambapo lile ziwa nalo liko vijijini. Kwa hiyo, hakuna uchumi ambao tunaupata kutokana na lile ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji tufanye biashara, yaani watu wetu wawe na zile biashara ndogo ndogo zinazowapa uchumi. Sasa unapotaja biashara, watu 200,000 halafu wameji-confine katika square kilometer 63, kwa hiyo, unakuta tatizo la ajira Mjini Musoma ni kubwa sana. Ndiyo maana tunasema kwamba Serikali inahitajika ku- intervene ili tuweze kupata maeneo na kwa kufanya hivyo basi tutakuwa tumewasaidia watu wetu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)