Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Anne Kilango Malecela

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Same Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kupata nafasi. Kwanza naomba nizungumze kwamba, naipongeza sana Serikali ya Chama Cha Mapinduzi. Tangu Awamu ya Tano imeanza wote tunashuhudia kazi zinazofanywa na Serikali. Nina uhakika wote ambao tuko sobber tunaona kwamba, Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi inafanya kazi kubwa sana. Naomba nichukue nafasi hii niipongeze na sio mimi na wananchi wangu wote wa Jimbo la Same Mashariki wanapongeza Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuzungumzia sehemu mbili ambazo zimeongelewa vizuri kwenye mpango, viwanda, lakini pamoja na kilimo. Naomba mimi niviunganishe hivi vitu viwili, viwanda na kilimo. Niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kusisitiza sana na kutuwezesha kufungua viwanda; viwanda vidogo, viwanda vya kati, viwanda vikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda hivi vyote vinavyofunguliwa Tanzania vinasaidia sana kilimo kwa sababu, vinachukua malighafi kutoka kwenye kilimo chetu, nafikiri hapo nimeeleweka, lakini kuna tatizo kubwa ambalo tusipoangalia vizuri tutakwenda tunajenga viwanda kwa nguvu sana baadaye vitakosa malighafi. Naomba nizungumzie kule ninakokuona, tumejenga kiwanda cha tangawizi, kile ni kiwanda kimejengwa na wananchi na Mbunge aliyekuwepo madarakani wakati huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka sasa hivi tumefika tumeungana na PSSSF ni mbia wa kiwanda cha tangawizi sio kwamba, ameleta mitambo, ni mbia wa Kiwanda cha Tangawizi cha Mambamiamba, naomba mnielewe vizuri ninalozungumza. Sasa hili jambo tuliangalie kwa nchi nzima, kiwanda kile kilipofika pale Same Mashariki nakiri kinakwenda kupanua kilimo cha tangawizi kwa sana. Wananchi watakuwa wana mahali pakuuzia tangawizi tena sio Same Mashariki tu na Same Magharibi watalima mpaka tukija Mlalo watalima, Lushoto watalima, Tanga watalima, kiwanda kiko pale. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo nililoliona maana kwa sisi viongozi tuwe tunaangalia huku na huku, tutafute kila njia Serikali, Mheshimiwa Waziri Mkuu namnyenyekea, watafute kila njia ya kwenda kuhakikisha miundombinu ya kilimo cha tangawizi inakuwa inayofanya wananchi waweze kulima kile kilimo. Sasa hivi wanaolima tangawizi kule kwangu ni wengi mno, nilianza na kata mbili, nikaja kata nne, sasa ni tarafa tatu zote za jimbo langu, wote wanalima tangawizi; miundombinu ya kilimo imekuwa haiwatoshelezi. Mifereji imekuwa ni midogo, mito imekuwa haina uwezo tena, lakini bado kuna uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kilimo kama Serikali ikija kule na kuangalia hali halisi. Kuna sehemu ambazo zinawezekana kuchimbwa mabwawa makubwa wakati wa mvua maji yakajaa, mvua zinapokuwa hazipo mito ikapata maji kutoka kwenye mabwawa yale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namnyenyekea Waziri wa Kilimo, Naibu Waziri wa Kilimo ni mwepesi sana, namkaribisha. Baada ya Bunge hili twende naye kule kwangu akaone hali halisi ya kuboresha miundombinu ya kilimo kwa ajili ya tangawizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudi kwenye mpunga ni hilohilo, nina tarafa inayolima mpunga. Tarafa ya Ndungu kuanzia Bendera, Kihurio, Ndungu, Maore ni mpunga, lakini miundombinu ya kilimo imechoka. Sijui kwa majimbo ya wenzangu, lakini miundombinu ya kilimo Same Mashariki, Same Magharibi ni jirani yangu hata yeye ana hilo tatizo. Naomba Serikali itusaidie kuja kutuangalia kwa sababu, bila ya kilimo hata hivi viwanda tunavyovizungumza itakuwa havina malighafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba kuzungumza hilo tu. Nashukuru sana na naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)