Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Nimesoma mapendekezo ya Mpango kwa makini na nimeona kwamba kuna maeneo mazuri kama kwa mfano maeneo ya malengo. Eneo la malengo limekaa vizuri; eneo la kazi za kufanya kufika malengo limekaa vizuri; eneo la mahitaji ya rasilimali watu na rasilimali fedha limekaa vizuri, lakini kuna tatizo kwenye maeneo mawili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo la mfumo wa ukusanyaji wa mapato, hili eneo inabidi Serikali iangalie kwa makini kwa sababu bado kuna vyanzo vingi havikusanywi. Vile vile Sheria ya TRA inaruhusu mapatano, yaani unakwenda kwa mtu unamkadiria alipe milioni mia nane, halafu akikaa kwenye mapatano unaweza ukashusha mpaka milioni mia nne. Hili ni tatizo kubwa. Hakuna utawala bora wa namna hiyo kwenye sheria. Kama sheria inaruhusu mapatano, hiyo sheria inakuwa haifai. Kwa hiyo, inatakiwa kwa kweli wafanye mapitio makubwa kwenye Sheria ya TRA ili sheria ikisema sharti hili kodi yake ni shilingi kumi na tano, iwe shilingi kumi na tano isiruhusu mapatano. Kuruhusu mapatano huo ni mwanya mbaya sana kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nimeona kwamba limefanyiwa mapitio ni mifumo ya udhibiti wa nje na ndani internal and external controls yaani ni muhimu sana kudhibiti matumizi ya fedha kama tunataka matokeo mazuri. Jambo la tatu eneo la ufuatiliaji na tadhimini, nalo halijakaa vizuri katika utekelezaji. Kwenye maandishi linaweza kukaa vizuri, lakini katika utekelezaji haijakaa vizuri, nani anawajibika pale ambapo kunakuwa na tatizo, anatakiwa a person, lazima mtu binafsi awajibike siyo taasisi kuwajibika. Kwa hiyo, hili ni eneo ambalo linatakiwa lifanyiwe mapitio ya kutosha ili tuwe na mpango mzuri hapa baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikipitia utekelezaji uliofanyika, umefanyika vizuri sana. Kwenye huduma za jamii, elimu, afya na maji, utekelezaji umefanyika vizuri sana kwa nchi nzima. Hata humu ndani walio wengi wa majimbo wamepita kwa sababu ya utekelezaji mzuri uliofanyika kwenye sekta za huduma za jamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo ningependa kulizungumzia utawala bora; sheria kama haitoi usawa, hiyo sheria ina matatizo. Kwenye eneo la utawala bora tulikuwa tunaathiriwa na upande wa sheria, sheria kwanza ni za zamani sana, zimepitwa na wakati, lakini kuna sheria hazitowi usawa. Kwa mfano, Sheria ya Trafiki, trafiki akikamata pikipiki anatoza shilingi 30,000 kwa kosa lolote lile; akikamata gari dogo shilingi 30,000; akikamata gari kubwa la mizigo shilingi 30,000. Hiyo sheria haitoi usawa, kwa mfano ingekuwa sawa pikipiki atoe shilingi 5,000; gari dogo atoe shilingi 10,000; gari nyingine yenye uzito fulani atoe shilingi 15,000 na gari kubwa atoe shilingi 30,000. Hapo ndio sasa Sheria ingetoa usawa kulingana na uzito wa matumizi ya vyombo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna eneo ambalo limefanyika vizuri sana, nalo ni la amani, usalama na utulivu wa nchi. Kwenye eneo la kukuza uchumi, nina ushauri maeneo machache. Nchi hii haitaendelea bila ardhi kupimwa. Ardhi ndiyo uchumi, ardhi ndiyo itawafanya Watanzania wapate uchumi. Kama Wizara ya Ardhi itaendelea kushugulikia migogoro midogo midogo tu na kuwasubiri watu kwamba tunamsubiri mtu ambaye atakuja kuomba kupimiwa kieneo chake badala kupima ardhi yote, mtu kama anataka ardhi aende akachukue ardhi ambayo imepimwa, kitakuwa kitu kizuri sana kwa uchumi wa nchi hii. Kwa hiyo, Serikali lazima ioneshe kwenye Mpango namna ambavyo watapima ardhi yote katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna kazi imefanyika vizuri sana kwenye maliasili, kwenye eneo la mawasiliano vijijini, barabara, madaraja makubwa, reli na bandari. Tatizo liko kwenye bajeti ya TARURA, namuunga mkono mzungumzaji, ndugu yangu Mheshimiwa Tabasamu, lazima TARURA waongezewe bajeti kama tunataka kusaidia uchumi wa nchi hii.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kakunda.

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)