Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Munde Abdallah Tambwe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. MUNDE T. ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ili nami niweze kuchangia Mpango wa Serikali. Niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza Serikali yote kwa ujumla, kumpongeza Mheshimiwa Rais pamoja na watendaji wote kwa mpango mzuri waliotuletea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufinyu wa muda naomba niende moja kwa moja kwenye hoja. Tuko kwenye kupambana kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa nchi ya uchumi wa kati, lakini na kuendelea Zaidi. Tuko kwenye kukusanya fedha lakini tuwe na matumizi mazuri ili nchi yetu izidi kufaidika, lakini tuendelee kupata maendeleo kama kiu aliyonayo Mheshimiwa Rais wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuingia Kamati ya Kilimo nimejifunza mambo mengi sana. Kuna miradi inaendelea kule kwenye majimbo yetu tulipotoka unakuta mradi wa bilioni nne lakini consultants hawa wanaofanya upembuzi yakinifu wanapata bilioni moja point, unashanga. Ukiangalia consultant ana ma-engineer, ana watu wa NEMC, ana Mhasibu sijui wa mradi, lakini ndani ya halmashauri zetu, ndani ya ofisi zetu za mikoa kuna ma-engineer, kuna watu wa NEMC, kwa nini kazi hizi zisifanywe na ma-engineer wetu wenyewe. Hivyo, hii bilioni moja point ambayo anaenda kupewa sasa huyu consultant ziendelee kufanya kazi kwenye halmashauri, ziendelee kuimarisha miradi mingine na kujenga miradi mingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe sana Serikali, niwaombe Mawaziri wanaohusika pamoja na watendaji wetu, sasa hivi tumefika stage ya kuionea huruma pesa ya Serikali, ma-engineer wetu wafanye hizi kazi. Unaweza ukachukua labda milioni mia mbili ama mia tatu ukasema vijana hawa tumewapa kazi hii wafanye upembuzi yakinifu, basi tutawalipa posho hii, kuliko kuchukua bilioni moja point kumpa consultant ambapo tunao uwezo, tumeajiri watu hao kwenye ofisi zetu, wanalipwa mishahara lakini unaenda kuchukua kampuni binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli unabaki pale pale hizi kampuni ni za kwao wenyewe, ni hawa hawa ma-engineer ndiyo wenye hizi kampuni. Kwa hiyo, naomba kabisa yale mambo yanayowezekana madogo madogo yafanywe na ma-engineer watu wetu wa NEMC walioajiriwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuongelea suala la kilimo. Tuko hapa tunaangalia tunavyopata shida ya mafuta, tumekuwa tukiagiza mafuta takribani milioni mia mbili themanini dola kila mwaka. Uwezo tunao wa kulima alizeti, ukiangalia mfano Wilaya ya Manyoni, Mkurugenzi huyo wa Manyoni kama humu ndani yupo kaka yangu Mheshimiwa Jafo, anastahili sifa kubwa, amefanya block farm ambayo ameweka heka elfu 30 za korosho. Leo hii heka zile za korosho wameanza kuvuna, lakini baada ya muda pato la mtu moja moja wa Manyoni litaenda kuimarika. Baada ya muda halmashauri yao itakusanya Cess zaidi ya bilioni 10 na kuhakikisha watajenga zahanati zao, watajenga madarasa yao na watatengeneza madawati yao. Hiyo ni block farm tu moja iliyowekwa na Mkurugenzi mmoja katika nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira zitapatikana, kodi italipwa, wakiuza nje Serikali Kuu itapata pesa na kadhalika, lakini mambo mengine mengi mengi yatapatikana hapo. Sasa ninachojiuliza imekuwa halmashauri nyingi kupitia Kamati zao za Fedha wanaenda kutembea pale, wanaenda kujifunza pale, lakini toka wameanza kujifunza hakuna halmashauri nyingine yoyote ambayo imeanza kuweka block farm labda ya alizeti au ya kitu gani ili kuondokana na huu umasikini wa mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza, Uganda walienda kujifunza pale Manyoni, leo Uganda wameanzisha block farm kama ya Manyoni, sisi kwa nini Tanzania tunashindwa, leo tukianzisha block farm kila wilaya katika mikoa mitano, heka elfu 10 za alizeti zikaangaliwe na Maafisa Ugani wetu, wataalam wetu wakaa pale kwenye block farm, wananchi wakapata ile ardhi kwa bei nafuu, wakapata mbegu za bure au za bei nafuu, tunaweza tukalima alizeti nyingi na tukapata mafuta ya kwetu sisi wenyewe na tukaacha kutoa pesa yetu ndogo hii ya Serikali kuagiza mafuta ambapo tunaacha kufanya huduma za muhimu tunaagiza mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufinyu wa muda niongelee kidogo umwagiliaji. Kule kwetu Tabora tumelitewa bilioni mbili kwa ajili ya kujenga bwawa la umwagiliaji, hakuna kinachoendelea bilioni mbili zimewekwa kule ndani lakini kumelimwa heka kumi na tano tu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Munde.

MHE. MUNDE TAMBWE ABDALLAH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)