Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Mpango wa Tano wa Maendeleo. Naomba nimtangulize Mwenyezi Mungu katika mchango wangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijachangia, kwanza kabisa nianze na kumpongeza sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kupata tuzo na kushika nafasi ya pili kwa kiongozi bora wa Marais katika Afrika, akiongozwa na Rais wa Ghana. Tuzo hiyo imetolewa na African Leadership ambayo Makao Makuu yake yako London, kwa kweli, nani kama Magufuli? (Makofi)

WABUNGE FULANI: Hakuna.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo niendelee kumpongeza pia Mheshimiwa Mpango kwa kutuletea Mpango wake ili tuweze kuuchangia hapa Bungeni. Pia, nimpongeze hata Mheshimiwa Dkt. Mwigulu kwa kuweza kuwasilisha mpango vizuri katika Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania tunaelekea kwenye uchumi wa viwanda. Katika kuelekea kwenye uchumi wa viwanda ni muhimu sana Mpango wetu ujikite kuhakikisha kwamba, barabara za kiuchumi zinapitika wakati wote, kwa sababu barabara zetu nyingi hazipitiki wakati wa mvua. Kwa hiyo, niiombe Serikali yetu ifanye upembuzi yakinifu kuhakikisha barabara zile za kiuchumi zinapitika na ikiwezekana zijengwe kwa kiwango cha lami, ili tuweze kupeleka malighafi katika viwanda vyetu. Vilevile kupunguza vifo vya akinamama na watoto katika maeneo yetu hasa ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano katika Mkoa wetu wa Iringa, zipo barabara za kiuchumi ambazo kwa kweli wakati wa masika hazipitiki. Mheshimiwa Kihenzile jana alikuwa anachangia na akataja baadhi pia ya maeneo ambayo hayapitiki kabisa na sasa hivi kuna malori yamekwama karibu wiki nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukienda kwenye baadhi ya barabara zetu za kiuchumi; kuna barabara ya Nyololo - Mtwango kama kilomita 40; ya Mafinga - Mgololo, Mafinga – Mapanda; Ipogolo – Kilolo; na Kilolo – Idete. Hizi ni baadhi tu ya barabara za kiuchumi ambazo tuna imani kabisa kama zitafanyiwa kazi vizuri pato la Taifa litaongezeka kwa sababu magari yatapita muda wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kuchangia kuhusiana na mradi wa REGROW ambao ni mradi wa kuendeleza maliasili na kukuza utalii Kusini mwa Tanzania. Mradi huu ulikuwa unatekelezwa na fedha za World Bank na utafaidisha Mikoa ya Iringa, Njombe, Mbeya, Songwe, Katavi, Rukwa pamoja na Ruvuma na Makao Makuu yake ni Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa kuutambulisha mradi huu ulikuwepo na ulikuwa mgeni rasmi lakini hatujaona maliasili na utalii katika Mikoa yetu hii ya Kusini tunafanyaje huu utalii? Tulikuwa tuna imani kabisa huu mradi ungesaidia kuleta ajira nyingi sana kupitia utalii na pato la Mikoa yetu ya Kusini na tulitegemea tuanze mashindano kati ya Mikoa ya Kaskazini na Kusini ili tuweze kupata kipato kikubwa cha taifa kupitia miradi ya utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka kujua, je, Maliasili sasa wamejipangaje? Huu mradi unaanza lini? Kabla hatujapata hizi fedha, je, wanatangaza, maana yake biashara ni matangazo, wanatangaza vivutio vilivyopo katika maeneo yetu ya Kusini? Vivutio Kusini viko vingi sana na siku ile ulishuhudia Wakuu wa Mikoa wote walieleza vivutio vizuri sana katika kila mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sasa Serikali ianze kutumia hata pato la ndani kabla ya kupata hizi fedha tuhakikishe tunatengeneza vivutio vyetu ili viweze kupitika tupate watalii wa ndani na wa nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono 100% Mpango huu wa Taifa. (Makofi)